The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa sita, siku ya tano ya mwezi wa sita, nilikuwa nyumbani kwangu pamoja na wazee wa Yuda. Basi, ghafla nikakumbwa na nguvu ya Mwenyezi-Mungu.[#8:1 Mfalme Yehoyakini alipelekwa uhamishoni mnamo mwaka wa 597 K.K.; kwa hiyo mwaka unaohusika hapa ni mwaka wa 591 K.K.; #8:1—11:25 Ono kuu la pili katika kitabu hiki cha Ezekieli (ono la kwanza lilikuwa 1:1—3:15) nalo, kama lile la kwanza limewekewa tarehe na kutanguliwa na maneno yale muhimu “Mwenyezi-Mungu akaniwekea mkono wake.]
2Nilipotazama, nikaona maono: Kitu kilichofanana na binadamu. Sehemu yake ya chini, iliyoonekana kama ndio kiuno chake, ilikuwa kama moto. Toka kiuno chake kwenda juu alikuwa na mng'ao kama wa shaba ing'aayo.[#8:2 Kadiri ya makala ya kale ya Kigiriki. Kiebrania: “kilichofanana na moto”.]
3Basi, akanyosha kitu kama mkono, akanishika kwa nywele zangu. Roho ya Mungu ikaninyanyua kati ya ardhi na mbingu, ikanipeleka mpaka Yerusalemu nikiwa katika maono hayo ya Mungu. Nikafika kwenye kiingilio cha lango la ukumbi wa ndani linaloelekea upande wa kaskazini, mahali palipowekwa sanamu iliyomchukiza Mungu.
4Utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwapo hapo; nao ulikuwa kama utukufu ule niliouona katika maono kule bondeni.
5Kisha Mungu akaniambia, “Wewe mtu, tazama upande wa kaskazini.” Nami nikatazama upande wa kaskazini, na huko upande wa kaskazini wa lango la madhabahu, niliona ile sanamu iliyomchukiza Mungu.[#8:5 Haijulikani ni sanamu ya mungu yupi ambayo ilikuwa chukizo kwa Mwenyezi-Mungu; labda ilikuwa sanamu ya mungu Tamuzi wa Mesopotamia; taz aya ya 14.]
6Basi, Mungu akaniambia, “Wewe mtu, je, waona mambo wanayofanya, machukizo makubwa wanayofanya Waisraeli ili wapate kunifukuza kutoka maskani yangu? Tena utaona machukizo mengine makubwa zaidi.”[#8:6 Mungu anamtangazia nabii nia yake ya kuliacha hekalu, na kwa kweli Mungu anaondoka hekaluni kama inavyosemwa katika sura ya 10.]
7Kisha akanipeleka mpaka lango la ua. Nilipoangalia nikaona tundu ukutani.
8Naye akaniambia, “Wewe mtu, toboa ukuta huu.” Nami, nikatoboa, nikaona kulikuwa na mlango.[#8:8 Kitendo hiki ni cha ishara. Mungu mwenyewe ndiye anayeona kinachofanyika, na anamwonesha nabii ambaye inambidi kutoboa shimo ukutani.]
9Naye akaniambia, “Ingia ndani ukaangalie machukizo mabaya wanayofanya humo.”
10Basi, nikaingia, nikaona sanamu za wadudu na za wanyama wa kila aina ya kuchukiza na vinyago vyote vya miungu ya Waisraeli, vimechorwa kuuzunguka ukuta.
11Na mbele ya sanamu hizo walisimama wazee sabini wa watu wa Israeli pamoja na Yaazania mwana wa Shafani. Kila mmoja alikuwa na chetezo mkononi, na moshi wa ubani ulipanda juu.[#8:11 Makosa mawili yanahusika hapa: kuabudu miungu mingine kinyume na Kumb 4:16-18 na kujichukulia wadhifa wa makuhani wa kutambika ubani (taz Hes 16).]
12Kisha Mungu akaniambia, “Wewe mtu, umeona wanayotenda wazee wa Waisraeli gizani, kila mtu katika chumba chake cha sanamu. Wanadai ati Mwenyezi-Mungu hatuoni. Mwenyezi-Mungu ameiacha nchi.”
13Tena akaniambia, “Bado utaona machukizo makubwa zaidi wanayotenda.”
14Kisha akanichukua mpaka lango la kaskazini la nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Huko kulikuwa na wanawake wameketi wakimwombolezea Tamuzi.
15Mungu akaniambia: “Wewe mtu, umeyaona hayo? Bado utaona machukizo mengine makubwa kuliko hayo.”
16Kisha akanipeleka mpaka ua wa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Huko mlangoni mwa hekalu, kati ya ukumbi na madhabahu, walikuwapo wanaume wapatao ishirini na watano, wakilipa kisogo hekalu, na nyuso zao zimeelekea upande wa mashariki. Walikuwa wanaabudu jua wakielekea upande wa mashariki.
17Mungu akaniambia, “Wewe mtu, je umeyaona mambo hayo? Hata hivyo, watu wa Yuda wanaona machukizo hayo kuwa ni kidogo. Wanaijaza nchi dhuluma na kuzidi kunikasirisha. Angalia jinsi wamekaa hapo, wananiudhi kupita kiasi.[#8:17 Au: “Wametia tawi puani mwao”, msemo ambao maana yake halisi haijulikani na huenda ulimaanisha matukano mabaya.]
18Kwa sababu ya mambo hayo watasikia uzito wa ghadhabu yangu. Sitamwacha hata mmoja aponyoke wala sitamwonea huruma mtu yeyote. Hata wakinililia kwa sauti kubwa mimi sitawasikiliza.”