The chat will start when you send the first message.
1Kisha nikamsikia Mwenyezi-Mungu akisema kwa sauti kubwa: “Njoni karibu nyinyi mtakaouadhibu mji huu. Njoni na silaha zenu za kuangamiza.”
2Watu sita wakaja kutoka upande wa lango la juu linaloelekea kaskazini, kila mmoja na silaha yake ya kuangamiza mkononi mwake. Pamoja nao, alikuwapo mtu mmoja ambaye alikuwa amevaa mavazi ya kitani, naye ana kidau cha wino. Wakaingia ndani ya hekalu, wakasimama pembeni mwa madhabahu ya shaba.[#9:2 Jumla ya hao watu ni saba, tarakimu ambayo mara kwa mara hutumika katika Biblia kama mfano wa ukamilifu wa jambo au kitu. “Mavazi ya kitani”: Hiyo ilikuwa aghalabu sera ya makasisi au makuhani (Kut 28:42; Lawi 16:23; 1Sam 2:18; 2Sam 6:14) na pia malaika waangamizi (Ufu 15:6).]
3Kisha utukufu wa Mungu wa Israeli uliondoka pale juu ya kiumbe chenye mabawa na kupanda juu mpaka kizingiti cha nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa mavazi ya kitani, mwenye kidau cha wino,[#9:3 Hii ni hatua ya kwanza ya Mungu kuondoka hekaluni (taz sura ya 10). “Juu ya kiumbe chenye mabawa”: Hapo juu ya hicho kiumbe (sanamu) chenye mabawa palifikiriwa kuwa ni kiti cha enzi cha Mungu duniani (rejea Kut 25:18-22; 1Fal 6:23-28).]
4akamwambia, “Pita katikati ya mji wa Yerusalemu, ukatie alama kwenye vipaji vya nyuso za watu wanaohuzunika na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayotendeka katika mji huu.”
5Kisha akawaambia wale wengine mimi nikiwa nasikia, “Piteni mjini mkimfuata, mkaue watu; msimwachie yeyote wala msiwe na huruma.
6Waueni wazee papo hapo, wavulana kwa wasichana, watoto na wanawake; lakini kila mmoja mwenye alama, msimguse. Anzeni katika maskani yangu.” Basi, wakaanza na wazee waliokuwa mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.[#9:6 Taz Ufu 7:3-4; 9:4.]
7Akawaambia, “Tieni unajisi nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa kuzijaza nyua zake maiti. Songeni mbele.” Basi, wakaenda, wakawaua watu mjini.
8Wakati walipokuwa wakiwaua, mimi niliachwa peke yangu, nikaanguka kifudifudi, nikalia, “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, je, utaangamiza watu wote wa Israeli waliobaki, ukitimiza ghadhabu yako juu ya Yerusalemu?”
9Naye akaniambia, “Uovu wa watu wa Israeli na watu wa Yuda ni mkubwa sana. Nchi imejaa umwagaji damu na mjini hakuna haki, kwani wanasema: ‘Mwenyezi-Mungu ameiacha nchi; Mwenyezi-Mungu haoni.’
10Kwa upande wangu, sitawaachia wala kuwahurumia; nitawatenda kadiri ya matendo yao.”
11Kisha mtu yule aliyevaa mavazi ya kitani, mwenye kidau cha wino, akarudi na kutoa taarifa: “Nimefanya kama ulivyoniamuru.”[#9:11 Aya hii inakumbusha Kut 24:8.]