Wagalatia 1

Wagalatia 1

1Mimi Paulo niliye mtume si kwa mamlaka ya binadamu, wala si kwa nguvu ya mtu, bali kwa uwezo wa Yesu Kristo na wa Mungu Baba aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu,[#1:1 Paulo anajitambulisha hivyo kama ilivyo katika barua zake nyingine, na kuhakikisha kwamba walengwa wake wameelewa vizuri kwamba aliitwa na Yesu na Mungu Baba (Mate 9:3-6; 26:15-18); na hivyo ujumbe anaoutangaza si wa bandia au wa kibinadamu. Rejea pia Gal 1:11-12.; #1:1-5 Paulo, kama kawaida ya nyakati hizo, anaanza kwa salamu (taz Rom 1:1-7 maelezo na pia Utangulizi kwa Barua za A.J.).]

2na ndugu wote walio pamoja nami tunayasalimu makanisa ya Galatia.[#1:2-4 “Galatia” ilikuwa eneo la Asia Ndogo ambalo sasa ni Uturuki. Makanisa hayo yalianzishwa na Paulo (Gal 3:1; 4:13-14); na Wakristo wake walikuwa kwa wingi wasio Wayahudi, yaani watu wa mataifa mengine (Gal 4:8). Taz pia utangulizi kwa barua za A.J.]

3Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.[#1:3 Paulo anatumia maneno haya mara kwa mara katika barua zake (Gal 1:2-3; Fil 1:2).]

4Kristo alijitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na mapenzi ya Mungu wetu na Baba, ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu mbaya wa sasa.[#1:4 Yaani ulimwengu mbaya wa sasa ambao ni tofauti kabisa na ulimwengu ujao ambao utaanza kwa kurudi kwake Yesu Kristo.]

5Kwake yeye uwe utukufu milele na milele! Amina.

Habari Njema kamili

6Nashangaa kwamba muda mfupi tu umepita, nanyi mnamwasi Mungu aliyewaita kwa neema ya Kristo, na mnafuata injili ya namna nyingine.[#1:6-9 Paulo hakufuata mtindo wa barua za kawaida hapa ambapo kungekuwa na tamko la kutoa shukrani na kuwaamkia waumini (taz tena Utangulizi kwa Barua za A.J.). Badala yake Paulo anakwenda moja kwa moja kuwakosoa Wagalatia kwa kumwasi Mungu upesi hivyo na kufuata Habari Njema ya namna nyingine. Zaidi ya hayo Paulo alikuwa amesikia kwamba kulikuwa na Wakristo wengine hasa waliokuwa Wayahudi ambao waliwalazimisha waumini wasio Wayahudi kutahiriwa na kushika mapokeo mengine ya Kiyahudi (Mate 15:1). Paulo anaona kufanya hivyo ni kukana nguvu ya kitendo cha ukombozi cha Yesu Kristo (rejea Gal 5:2-6; 6:12-15).]

7Lakini hakuna injili nyingine. Ukweli ni kwamba wako watu wanaowavurugeni, watu wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo.[#1:7 Taz maneno karibu kama hayo hayo katika Mate 15:24 katika ile barua ya Mitume kule Yerusalemu kwa Wakristo wasio Wayahudi.]

8Lakini, hata kama mmoja wetu au malaika kutoka mbinguni, atawahubirieni injili tofauti na ile tuliyowahubirieni sisi, basi huyo na alaaniwe![#1:8-9 1Kor 16:22 maelezo.]

9Tulikwisha sema, na sasa nasema tena: kama mtu yeyote anawahubirieni injili ya aina nyingine, tofauti na ile mliyokwisha pokea, huyo na alaaniwe!

10Sasa nataka kibali cha nani: cha binadamu, ama cha Mungu? Au je, nataka kuwapendeza watu? Kama ningefanya hivyo, mimi singekuwa kamwe mtumishi wa Kristo.[#1:10 1Thes 2:4. Maswali haya ni ya mtindo wa ufasaha yasiyotaka majibu; yanatumika kutilia mkazo, n.k.]

Paulo alivyopata wito wake

11Ndugu, napenda mfahamu kwamba ile Injili niliyoihubiri si ujumbe wa kibinadamu.

12Wala mimi sikuipokea kutoka kwa binadamu, wala sikufundishwa na mtu. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyenifunulia.[#1:12 Paulo anagusia mambo yale yaliyompata njiani kwenda Damasko (Mate 9:3-6; 22:8-10; 26:13-18) mambo ambayo anayaona kuwa ni ufunuo na mwito wake (rejea aya ya 6).]

13Bila shaka mlikwisha sikia jinsi nilivyokuwa ninaishi zamani kwa kuzingatia dini ya Kiyahudi, na jinsi nilivyolitesa kanisa la Mungu kupita kiasi na kutaka kuliharibu kabisa.

14Naam, mimi niliwashinda wengi wa wananchi wenzangu wa rika langu katika kuizingatia dini ya Kiyahudi, nikajitahidi sana kuyashika mapokeo ya wazee wetu.

15Lakini Mungu, kwa neema yake, alikuwa ameniteua hata kabla sijazaliwa, akaniita nimtumikie.

16Mara tu alipoamua kunifunulia Mwanawe kusudi niihubiri Habari Njema yake kwa watu wa mataifa mengine, bila kutafuta maoni ya binadamu,[#1:16 Kwa maneno mengine: “Kunifanya nimjue Mwanawe” kwa maana ya kumjua kikamilifu (Mate 9:1-6 na sambamba zake).]

17na bila kwenda kwanza Yerusalemu kwa wale waliopata kuwa mitume kabla yangu, nilikwenda kwanza Arabia, kisha nikarudi tena Damasko.[#1:17 Yamkini ni eneo la utawala wa Kiarabu wa Wanabatea, eneo ambalo liilienea kutoka Kusini-Mashariki ya Palestina mpaka Kaskazini. Wakati mmoja mji wa Damasko ulikuwa pia sehemu yake. Rejea Mate 9:18-25; taz 2Kor 11:32-33.]

18Ilikuwa tu baada ya miaka mitatu, ndipo nilipokwenda Yerusalemu kuonana na Kefa; nilikaa kwake siku kumi na tano.[#1:18 Hili ni Kiaramu cha jina la Kigiriki “Petros” lenye maana hiyohiyo; taz Mat 16:18 maelezo na 1Kor 1:12 maelezo.]

19Lakini sikuwaona mitume wengine isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana.[#1:19 Hakuwa mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Lakini alikuwa mtu maarufu katika Kanisa la Yerusalemu (Mate 12:17 maelezo). Na kuhusu Yakobo kuwa ni “ndugu yake Bwana” taz Mat 12:46 maelezo; rejea Marko 6:3.]

20Haya ninayowaandikieni, Mungu anajua; sisemi uongo.

21Baadaye nilikwenda katika tarafa za Siria na Kilikia.[#1:21 Mkoa wa Kiroma upande wa Kusini mwa Asia Ndogo; mji wake mkuu ulikuwa Tarso, mji alimozaliwa Paulo (Mate 22:3). Rejea Mate 9:30; 11:25.]

22Wakati huo, mimi binafsi sikujulikana kwa jumuiya za Wakristo kule Yudea.

23Walichokuwa wanajua ni kile tu walichosikia: “Mtu yule aliyekuwa akitutesa hapo awali, sasa anaihubiri imani ileile aliyokuwa anajaribu kuiangamiza.”

24Basi, wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania