The chat will start when you send the first message.
1Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyokamilika pamoja na vitu vyote vilivyomo.
2Siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyofanya; siku hiyo ya saba Mungu akapumzika baada ya kazi yake yote aliyofanya.[#2:2 Neno la Kiebrania linalotafsiriwa hapa kwa kitenzi “akapumzika” lina maana: “akaacha” au “akamaliza”. Kwa kusema kwamba Mungu alipumzika haina maana ya kwamba yeye aliacha kutenda ila ina maana kwamba yote aliyotenda yalifana kulingana na yale aliyokusudia. Taz Yoh 5:17-18 maelezo.]
3Mungu akaibariki siku ya saba na kuitakasa, kwa kuwa siku hiyo Mungu alipumzika baada ya kazi yake yote ya kuumba.[#2:3 Katika Biblia namba au idadi saba inatumika mara nyingi kuelezea ukamilifu wa kitu. Taz Mwa 4:18 maelezo.]
4Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyoumbwa.[#2:4 Hapa wazo la Mwa 1:1 linarudiwa ili kuonesha kwamba simulizi la kuumbwa ulimwengu limekamilika. Tafsiri au fafanuzi mbalimbali zimetolewa kuhusu tamko hili. Katika Kiebrania, neno kwa neno, ni: Hivi ni vizazi vya mbingu na dunia zilipoumbwa. Lakini “vizazi” hapa, yamkini ni msemo unaokusudia kutaja vitu vyote vya ulimwengu. Kwa hiyo si vizazi vya binadamu. Tafsiri nyingine zimejaribu kuleta maana kwa kusema: “Hii ndiyo historia ya mbingu na dunia zilipoumbwa”. Tafsiri nyingine pia hufikiri kwamba mwandishi alitaka kusema “jinsi zilivyoumbwa”, lakini mwandishi hana nia ya kusema juu ya “namna”, bali anasema tu wakati “zilipoumbwa” hivyo ndivyo vitu vyake vya awali, vizazi vyake au historia yake. Mtendaji wa “zilipoumbwa” bila shaka ni Mungu, na tafsiri nyingine ni “wakati Mungu alipoziumba”. Kwa namna hii tamko hili linaifunga sehemu iliyotangulia kwa kurudia tena ile mada ya 1:1.]
Siku ile Mwenyezi-Mungu alipoziumba mbingu na dunia,
5Hapakuwa na mimea juu ya nchi wala miti haikuwa imechipua kwani Mwenyezi-Mungu hakuwa ameinyeshea nchi mvua, wala hapakuwa na mtu wa kuilima.
6Hata hivyo, maji yalitoka ardhini yakainywesha ardhi yote.
7Basi, Mwenyezi-Mungu akamfanya mwanamume kwa mavumbi ya udongo, akampulizia puani pumzi ya uhai, na huyo mwanamume akawa kiumbe hai.[#2:7 Kiebrania kinatumia mchezo wa maneno hapa: “adam” neno ambalo lina maana ya “mtu” (binadamu) na “adama” neno ambalo lina maana ya “udongo.” (Mtindo huohuo unatumiwa katika Mwa 3:19). Yahusu uhusiano uliopo kati ya binadamu na nchi au udongo.; #2:7 Kutaja kitendo hiki cha pekee cha Mungu kunakumbusha tofauti iliyopo baina ya kuumbwa viumbe vingine na binadamu (taz lugha inayotumiwa katika Mwa 1:27). Rejea Isa 45:9-11; Yer 18:1-6; Rom 9:21 ambapo kitendo kikuu cha Mungu kinafananishwa na mfinyanzi anayefinyanga vyombo vyake.]
8Kisha Mwenyezi-Mungu akapanda bustani huko Edeni, upande wa mashariki, na humo akamweka huyo mwanamume aliyemuumba.[#2:8 Jina hili Kiebrania maana yake ni “enye kupendeza sana” au, “anasa” (rejea Isa 51:3; Eze 31:8-9). Wengine wanahusisha jina hilo na neno la lugha ya Asiria lenye maana ya tambarare, nyika au mbuga.]
9Mwenyezi-Mungu akaotesha kutoka ardhini kila aina ya miti mizuri izaayo matunda yafaayo kwa chakula. Katikati ya bustani hiyo kulikuwa na mti wa uhai na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.[#2:9 Au, “Mti ambao matunda yake huleta uhai”. Rejea Mwa 3:22; Ufu 2:7; 22:2,14.; #2:9 Ili kuweza kuelewa vizuri maana ya maneno haya yafaa kukumbusha tena desturi katika lugha ya Kiebrania ya kutaja jumla ya kitu au ukamilifu wa kitu kwa kutaja maneno mawili yanayoonesha pande mbili za hicho kitu ambazo zinakabiliana (taz k.m. maelezo ya 1:1). Fungu hili la maneno halina maana ya ujuzi wa akili peke yake, ila laweza pia kujumlisha wazo la utambuzi, upambanuzi na hata pia wazo la kumiliki. Kujua mema na mabaya aghalabu ni sawa na kuweza kuamua kwa hiari na bila kumtegemea mwingine kilicho chema au kilicho kibaya; kwa maneno mengine ni sawa na kuwa na mamlaka kamili kuhusu jambo la uadilifu. Rejea Mwa 3:22.]
10Kulikuwa na mto huko Edeni uliotiririka maji na kuinywesha hiyo bustani; kutoka huko mto huo uligawanyika kuwa mito minne.
11Jina la mto wa kwanza ni Pishoni; huo waizunguka nchi yote ya Hawila ambako kuna dhahabu.
12Dhahabu ya nchi hiyo ni safi kabisa. Huko pia kuna marashi yaitwayo bedola na vito viitwavyo shohamu.
13Jina la mto wa pili ni Gihoni; huo waizunguka nchi yote ya Kushi.[#2:10-14 Si wazi, dhahiri ni mahali gani hasa panapohusika katika simulizi hili. Kushi ni eneo la Afrika ya kaskazini (ambapo sasa ni Misri, Ethiopia mpaka hata Sudani) na mto Gihoni unadhaniwa kuwa ni Nili, hali Tigri na Eufrate ni mito ya huko Mesopotamia.]
14Jina la mto wa tatu ni Tigri, nao watiririkia upande wa mashariki wa nchi ya Ashuru; na jina la mto wa nne ni Eufrate.
15Basi, Mwenyezi-Mungu akamtwaa huyo mwanamume, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.[#2:15 Hapa, kazi sio matokeo ya adhabu kwa dhambi ila ni shughuli inayomwezesha mtu kutekeleza wajibu katika kuhifadhi maendeleo ya dunia na pia kujiendeleza yeye mwenyewe (rejea Mwa 1:28). Ni kutokana tu na dhambi ndipo jambo la kazi limechukua hali yake ya bughudha, jasho na taabu (Mwa 3:17,19).]
16Mwenyezi-Mungu alimwamuru huyo mwanamume, “Waweza kula matunda ya mti wowote katika bustani;
17lakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, usile, maana siku utakapokula matunda ya mti huo, hakika utakufa.”[#2:17 Kwa kumpa amri hiyo Mungu anatambua kwamba huyo mtu ni kiumbe anayewajibika kwa vitendo vyake; na kwa upande mwingine pia Mungu anaonesha ukuu wake juu ya binadamu na kumtaka atambue mpaka wake yeye mwenyewe na mazingira yake ya kibinadamu (Eze 28:2; rejea Isa 14:13-14).]
18Kisha Mwenyezi-Mungu akasema, “Si vizuri huyu mwanamume kuwa peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.”[#2:18 Tafsiri nyingine yamkini ni “mwenzi”.]
19Basi, kutoka katika udongo, Mwenyezi-Mungu akaumba kila mnyama wa porini na kila ndege wa angani, halafu akamletea huyo mwanamume aone atawapa majina gani; na majina aliyowapa viumbe hao, yakawa ndio majina yao.[#2:19-20 Jina la kitu, kwa fikira za watu wa Mashariki ya Kati ya Kale, halikuwa tu jambo la nje nje tu, ila lilikuwa sehemu ya maumbile ya mtu au kitu hicho kinachopewa jina hilo. Kuitia jina au kubadili jina ilimaanisha pengine kuwa na mamlaka kiasi fulani juu ya huyo mtu au kitu (taz k.m. 2Fal 23:34).]
20Basi, huyo mwanamume akawapa majina wanyama wote wa kufugwa, wanyama wa porini na ndege wote wa angani. Lakini hakupatikana msaidizi yeyote wa kumfaa.
21Basi, Mwenyezi-Mungu akamletea huyo mwanamume usingizi mzito, na alipokuwa usingizini, akatwaa ubavu wake mmoja na kupafunika mahali pale kwa nyama.
22Na huo ubavu Mwenyezi-Mungu alioutoa kwa yule mwanamume akaufanya kuwa mwanamke, akamleta kwa huyo mwanamume.
23Ndipo huyo mwanamume akasema,
“Naam! Huyu ni mfupa kutoka mifupa yangu,
na nyama kutoka nyama yangu.
Huyu ataitwa ‘Mwanamke’,
kwa sababu ametolewa katika mwanamume.”
24Ndiyo maana mwanamume humwacha baba yake na mama yake, akaambatana na mkewe, nao wawili huwa mwili mmoja.[#2:24 Mat 19:5; Marko 10:7-8; 1Kor 6:16; Efe 5:31. Aya hii inatilia mkazo ubora na maana ya ndani kabisa ya ndoa.]
25Huyo mwanamume na mkewe wote walikuwa uchi, lakini hawakuona haya.[#2:25 Kuwa uchi hapa bila kuona haya ni maelezo ya hali timilifu isiyo na kasoro au hisia ya hatia; hali ya amani wao kwa wao, na wao wenyewe na Mungu. Baadaye lakini, kama matokeo ya dhambi, inakuwa hali ya haya na aibu.]