The chat will start when you send the first message.
1Yesu Kristo alikuwa wa ukoo wa Daudi, wa ukoo wa Abrahamu. Hii ndiyo orodha ya ukoo wake:[#1:1 Miongoni mwa mababu katika nasaba au ukoo wa Yesu wanatajwa hapa hawa wawili ambao ni maarufu zaidi: Kwa Abrahamu Mungu alikuwa ameweka ahadi ya baraka kwa wazawa wake na kwa mataifa yote (rejea Mwa 12:3; 17:4-9; 22:15-18; Mat 28:19; Gal 3:16). Hali kadhalika na zile ahadi alizopewa Daudi katika 2Sam 7:16 zilichochea matumaini kwamba kutakuwa na Masiha au Kristo atakayewaokoa watu. Orodha hii ya wazee wa Yesu Kristo yahitilafiana kiasi fulani na ile ya Luka (3:23-38). Mathayo anaanza orodha hii na Abrahamu ambaye alijulikana kuwa babu maarufu wa Waisraeli na ambaye kwake Mungu atawabariki watu wote, hali Luka anaanza orodha yake kuanzia Yesu hadi Adamu ambaye alikuwa babu wa kwanza wa watu wote. Kama ilivyosemwa katika utangulizi, tofauti hii kubwa yadhihirisha kwamba wasomaji wa Mathayo ni hasa Wayahudi walioongokea dini ya Kikristo - kwa hiyo kwao kumtaja Yesu kama wa ukoo wa Abrahamu kungeeleweka na kupokelewa vizuri zaidi. Aghalabu Wayahudi kama vile na makabila mengi katika nchi zetu za Afrika ukoo wa mtu ni jambo muhimu na hutumiwa kuhalalisha mambo mengi. Yesu ana uhusiano na taifa teule la watu wa Mungu. Nasaba hii basi ina madhumuni ya kuonesha kwamba Yesu ni Masiha, mfalme wa Wayahudi, ambaye kwake Mungu ametekeleza matakwa yake kuhusu watu wote.; #1:1—2:2 Sura hizi kwa jumla lengo lake ni kuonesha tangu mwanzo kwamba Yesu ndiye mteule wa Mungu au Masiha ambaye Mungu aliwaahidi Waisraeli, na ambaye ni Mwana wa Mungu na Mwokozi. Wayahudi walimtambua lakini viongozi wao walimkataa.]
2Abrahamu alimzaa Isaka,
Isaka alimzaa Yakobo,
Yakobo alimzaa Yuda na ndugu zake,
3Yuda alimzaa Peresi na Zera (mama yao alikuwa Tamari),
Peresi alimzaa Hesroni,
Hesroni alimzaa Rami,
4Rami alimzaa Aminadabu,
Aminadabu alimzaa Nashoni,
Nashoni alimzaa Salmoni,
5Salmoni alimzaa Boazi (mama yake Boazi alikuwa Rahabu)
Boazi na Ruthu walikuwa wazazi wa Obedi,
Obedi alimzaa Yese,
6naye Yese alimzaa Mfalme Daudi.
Daudi alimzaa Solomoni (mama yake Solomoni alikuwa Bath-Sheba mke wa Uria).
7Solomoni alimzaa Rehoboamu,
Rehoboamu alimzaa Abiya,
Abiya alimzaa Asa,
8Asa alimzaa Yehoshafati,
Yehoshafati alimzaa Yoramu,
Yoramu alimzaa Uzia,
9Uzia alimzaa Yothamu,
Yothamu alimzaa Ahazi,
Ahazi alimzaa Hezekia,
10Hezekia alimzaa Manase,
Manase alimzaa Amoni,
Amoni alimzaa Yosia,
11Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake.
Huo ulikuwa wakati Wayahudi walipopelekwa uhamishoni Babuloni.
12Baada ya Wayahudi kupelekwa uhamishoni Babuloni,
Yekonia alimzaa Shealtieli,
Shealtieli alimzaa Zerubabeli,
13Zerubabeli alimzaa Abiudi,
Abiudi alimzaa Eliakimu,
Eliakimu alimzaa Azori,
14Azori alimzaa Zadoki,
Zadoki alimzaa Akimu,
Akimu alimzaa Eliudi,
15Eliudi alimzaa Eleazari,
Eleazari alimzaa Mathani,
Mathani alimzaa Yakobo,
16Yakobo alimzaa Yosefu, mumewe Maria mama yake Yesu aitwaye Kristo.
17Basi, kulikuwa na vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi mpaka Wayahudi walipochukuliwa mateka Babuloni, na vizazi kumi na vinne tangu kuchukuliwa mateka mpaka wakati wa Kristo.[#1:17 Hapa mwandishi Mathayo anatupatia picha ya mfululizo wa vizazi kumi na vinne, nambari ya mfano ambayo msingi wake ni tarakimu ya saba ambayo katika Biblia ni nambari ya mfano.; #1:17 Jina la sifa la Kigiriki ambalo ni tafsiri ya jina la Kiebrania “Masiha”. Majina hayo (katika Kigiriki na katika Kiebrania) yanamaanisha “mtu aliyepakwa mafuta” yaani, aliyewekwa wakfu au kuteuliwa na Mungu kwa ajili ya wadhifa au kazi maalumu. Taz pia Fahirisi.]
18Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.[#1:18-19 Taz Luka 1:26-27. Kwa mila na desturi za Wayahudi vijana walioahidi rasmi kuoana walichukuliwa kama vile wangekuwa mume na mke hata kama hawajaishi pamoja na jambo la kuachana liliwezekana tu kwa kutoa talaka kisheria (taz Kumb 24:1).]
19Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri.
20Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, “Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mjamzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.[#1:20 Taz pia 2:13,19.]
21Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye ndiye atakayewaokoa watu wake katika dhambi zao.”[#1:21 Jina la Kigiriki linatokana na jina la Kiebrania “Yoshua”, maana yake “Mwenyezi-Mungu ni Mwokozi” au, “Mwenyezi-Mungu huokoa”. Rejea Zab 130:8; Luka 1:31; 2:11,21. Majina ya Kiyahudi kama vile na majina mengi ya watoto katika makabila mbalimbali katika Afrika Mashariki, mara nyingi yalijaa maana za pekee. Hapa maana ya kidini ni muhimu: Yesu ndiye atakayewaokoa watu wake katika dhambi zao.]
22Basi, haya yote yalitukia ili litimie lile neno Bwana alilosema kwa njia ya nabii:[#1:22 Jambo la kawaida na la pekee katika Injili hii ni lile la kutaja kwamba kitu au tukio fulani lilifanyika “ili litimie …” Mathayo anasema hivyo mara 14 katika Injili hii, mara nyingi zaidi ili kuonesha uhalali wa nafsi yake Yesu na kazi yake, yaani kwa maisha yake na matendo yake, ahadi za Mungu za kuwaokoa watu wake zimetimia kama Mungu alivyotangaza kwa njia ya manabii wake (taz 2:15,17,23; 4:14; 8:17; 12:17; 13:35; 21:4; 27:9). Sehemu zote hizo zina karibu maneno yale yale.]
23“Bikira atachukua mimba,
atamzaa mtoto wa kiume,
nao watampa jina Emanueli”
(maana yake, “Mungu yuko nasi”).
24Hivyo, Yosefu alipoamka usingizini alifanya kama malaika huyo alivyomwambia, akamchukua mke wake nyumbani.
25Lakini hakulala naye hata Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu.[#1:25 Msemo wa Kibiblia ambao hapa una maana ya kitendo cha ndoa cha mume na mke. Lengo au shabaha ya mwandishi hapa ni kusisitiza kwamba Yesu hakuwa mtoto wa Yosefu.; #1:25 Kwa kufanya hivyo Yosefu anajichukulia kuwa baba wa huyo mtoto kisheria. Luka (2:21) hasemi ni nani anayempa huyo mtoto jina. Katika Luka 1:31 malaika anamwambia Maria amwite hivyo.]