The chat will start when you send the first message.
1Yesu alipoyaona makundi ya watu, alipanda mlimani, akaketi. Wanafunzi wake wakamwendea,[#5:1—7:27 Hii ni sehemu ya kwanza ya mafundisho marefu katika Injili hii ya Mathayo (taz utangulizi). Sehemu hii muhimu yahusu hali na tabia, wajibu na haki, faida na majaliwa ya wale walio raia wa utawala wa mbinguni, yaani wale ambao ni wafuasi wake Yesu Masiha. Sehemu hii ina muundo mmoja ambao shabaha yake ni kutoa mwongozo kwa jumuiya ya agano jipya. Mengi ya mafundisho haya yanatumia wingi: “Nyinyi …” lakini hata pale ambapo umoja unatumika, kwa mfano 6:2-4,17-18,22-23 ni dhahiri kwamba hotuba yote inamhusu kila mtu anayeyasikia maneno haya (7:24,26). Mwandishi Luka naye pia ametuachia mahubiri sambamba (taz Luka 6:20-49). Katika Luka kuna heri nne, hali hapa katika Mathayo kuna heri tisa.]
2naye akaanza kuwafundisha:
3“Heri walio maskini rohoni,[#5:3 Mtu mwenye heri ni mtu aliye katika hali bora na hapa heri latumika aghalabu kusema kwamba wahusika wamebarikiwa na Mungu, wameneemeshwa naye, wamejaliwa au wamo katika hali bora ya fanaka njema; ling Mat 13:16; 16:17; Zab 1:1.; #5:3 Maana ya maneno haya si dhahiri hasa kwa vile umaskini si jambo la heri linalopendeza; na hata mahali pengine katika Biblia umaskini ni matokeo ya ukosefu wa haki katika jumuiya n.k. (Meth 13:18,23; 20:13). Msemo huu unawataja watu ambao tegemeo lao sio katika mambo ya kidunia ila wanamtegemea Mungu kwa kila kitu (rejea Zab 22:24; 69:32-33; Isa 29:19; 61:1-2; Mat 11:5; Luka 4:18; Yak 2:5). Watu wa namna hiyo ndio wanaostahili kuwa raia wa ufalme wa mbinguni. Maneno hayo “maskini rohoni” karibu ni sawa na maana inayohusika pia katika msemo wa aya 5 na 8.]
maana ufalme wa mbinguni ni wao.
4Heri walio na huzuni,[#5:4 Au, “wanaoteseka”, au, “wanaoomboleza”; rejea Zab 126:5-6; Isa 57:18; 61:2-3. Neno watafarijiwa (kitenzi - hali ya kutendewa, hapa na katika aya 6 (watashibishwa) mwenye kufanya vitendo hivyo ni Mungu. Kwa hiyo inawezekana kutafsiri: “Mungu atawafariji”; “Mungu atawashibisha”.]
maana watafarijiwa.
5Heri walio wapole,
maana watairithi nchi.
6Heri wenye njaa na kiu ya kufanya atakavyo Mungu,[#5:6 Tafsiri ya neno kwa neno ni: “wenye njaa na kiu ya uadilifu”. Kuwa na njaa na kiu ni matumizi ya mfano: yaani kuwa na hamu kubwa. Kuhusu maneno “atakavyo Mungu”, taz Mat 3:15 maelezo.]
maana watashibishwa.
7Heri walio na huruma,[#5:7 Wenye kuona wengine wamo katika shida, wakawasaidia kwa moyo. Lakini pia kuwa na huruma ni tabia yake Mungu mwenyewe; na binadamu katika Agano Jipya wanaitwa wawe na huruma kama Mungu alivyo na huruma (taz pia 9:13; 12:7; 18:21-35).]
maana watahurumiwa.
8Heri wenye moyo safi,[#5:8 Yaani mtu aliyejitolea kwa Mungu kikamilifu na asiye na nia mbaya wala unafiki kwa Mungu na kwa binadamu. Neno “moyo” hutumika mara nyingi kama kielelezo cha kikao cha maisha ya ndani ya mtu: fikira zake, mawazo yake, matazamio yake, maamuzi yake, n.k.; ling 9:4; 11:29; 12:34; Zab 24:3-4; Isa 61:1.]
maana watamwona Mungu.
9Heri wenye kuleta amani,[#5:9 Yaani watu wale wanaojitahidi kuweka hali ya upatanisho miongoni mwa watu na kati ya watu na Mungu (2Kor 5:18). Taz pia Zab 34:14; Meth 12:20.]
maana wataitwa watoto wa Mungu.
10Heri wanaoteswa kwa sababu ya kufanya atakavyo Mungu,[#5:10 Taz 1Pet 3:14.]
maana ufalme wa mbinguni ni wao.
11“Heri yenu nyinyi watu wakiwatukana, wakiwadhulumu na kuwasingizia kila aina ya uovu kwa ajili yangu.
12Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Hivyo ndivyo walivyowadhulumu manabii waliokuwako kabla yenu.[#5:12 Wazo la kupewa tuzo hutokea mara kwa mara katika Mathayo (rejea 5:46; 6:1; 10:42).; #5:12 Mara nyingi wale watu waliokuwa wasemaji wa Mungu walidharauliwa na kuteswa. Taz 2Nya 36:16; Mat 23:34,37; Mate 7:52.]
13“Nyinyi ni chumvi ya dunia. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake itakolezwa na nini? Haifai kitu tena, ila hutupwa nje na kukanyagwa na watu.[#5:13 Matumizi ya chumvi hapa yanatokana na thamani yake: Hukoleza chakula na pia hukihifadhi kisioze (Marko 9:50; Luka 14:34-35). Chumvi ilitumika pia katika ibada mbalimbali za kidini (rejea Lawi 2:13; Hes 18:19 maelezo).]
14“Nyinyi ni mwanga wa ulimwengu! Mji uliojengwa juu ya mlima hauwezi kufichika.[#5:14 Wafuasi wa Yesu wanatajwa kuwa mwanga kama yeye Yesu alivyo mwanga wa ulimwengu. Taz Yoh 8:12; 9:5; Fil 2:15.]
15Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa debe, ila huiweka juu ya kinara ili iwaangazie wote waliomo nyumbani.[#5:15 Debe latumika hapa kutafsiri chombo kilichotumika kupimia nafaka. Mwanga wa waumini lazima uangaze (5:16; 1Pet 2:12).]
16Vivyo hivyo, ni lazima mwanga wenu uangaze mbele ya watu, ili wayaone matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
17“Msidhani kuwa nimekuja kutangua sheria na mafundisho ya manabii. Sikuja kutangua bali kukamilisha.[#5:17 Yahusu jumla ya vitabu vya Agano la Kale ambavyo vilikuwa msingi wa mafundisho ya imani katika dini ya Kiyahudi. Taz pia 7:12; 11:13; 22:40.; #5:17 Au: “kutimiza”; maana ya kwanza yaonekana kuwa dhahiri zaidi hapa.]
18Kweli nawaambieni, mpaka hapo mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata nukta moja au sehemu ndogo kabisa ya sheria itakayoondolewa, mpaka yote yametimia.[#5:18 Luka 16:17; 21:33.]
19Basi, yeyote atakayevunja hata amri moja ndogo kuliko zote, na kuwafundisha wengine wafanye hivyo, huyo atakuwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni. Lakini yule atakayezishika na kuwafundisha wengine, huyo atakuwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.
20Ndio maana nawaambieni, wema wenu usipozidi ule wa waalimu wa sheria na wa Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
21“Mmekwisha sikia ya kuwa watu wa kale waliambiwa: ‘Usiue! Atakayeua lazima ahukumiwe.’[#5:21-48 Aya hizi zahusu mwongozo kuhusu yapata visa mbalimbali katika maisha na kuonesha msimamo wanaotakiwa wanafunzi wa Yesu kuwa nao katika matendo. Haitoshi tu kushika yanayosemwa katika sheria ila inawabidi kutazama hali na nia ya ndani na tamaa zake mtu ambazo ni chanzo cha dhambi.]
22Lakini mimi nawaambieni, yeyote anayemkasirikia ndugu yake, lazima ahukumiwe. Anayemdharau ndugu yake atapelekwa mahakamani. Anayemwita ndugu yake: ‘Pumbavu’ atastahili kuingia katika moto wa Jehanamu.[#5:22 Baadhi ya hati za kale zina: “anayekasirika bila sababu”.; #5:22 Kigiriki “Gehena” jina la mahali kusini-magharibi mwa Yerusalemu ambapo kafara za binadamu zilitolewa na ambapo takataka za mji zilitupwa na moto kuwaka daima. Picha ya huo moto imetumika kuelezea adhabu ya Mungu.]
23“Basi, ukipeleka sadaka yako mbele ya madhabahu na hapo ukakumbuka kwamba ndugu yako ana ugomvi nawe,
24iache sadaka yako mbele ya madhabahu, nenda kwanza ukapatane na ndugu yako, ndipo urudi utoe sadaka yako.
25“Patana na mshtaki wako upesi mkiwa bado njiani kwenda mahakamani. La sivyo, mshtaki wako atakukabidhi kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa askari, nawe utafungwa gerezani.[#5:25 Hapa ni Baraza Kuu la hukumu. Taz Orodha ya Maneno: Baraza/Halmashauri.]
26Kweli nakuambia, hutatoka humo mpaka umelipa senti ya mwisho.
27“Mmesikia kwamba watu waliambiwa: ‘Usizini!’[#5:27 Rejea tena Kut 20:14; Kumb 5:18. Yesu hapa na katika aya 28 anaonesha jinsi sheria hiyo inavyopaswa kutekelezwa katika jamii mpya ya watu wa Mungu.]
28Lakini mimi nawaambieni, atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani, amekwisha zini naye moyoni mwake.
29Basi, kama jicho lako la kulia linakukosesha, ling'oe ukalitupe mbali. Afadhali zaidi kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote kutupwa katika moto wa Jehanamu.[#5:29-30 Mat 18:8-9; Marko 9:43-47. Msemo ulio na shabaha ya kueleza umuhimu wa kuweka kando chochote kilicho cha thamani wakati kinaposababisha dhambi.]
30Na kama mkono wako wa kulia unakukosesha, ukate ukautupe mbali. Afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote uende katika moto wa Jehanamu.
31“Ilikwisha semwa pia: ‘Anayemwacha mke wake, yampasa ampe hati ya talaka’.
32Lakini mimi nawaambieni, anayempa mkewe talaka, isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, anamfanya azini; na mwanamume akimwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini.[#5:32 Maneno haya yanapatikana tu katika Mathayo, hapa na 19:9. Kuhusu mafundisho mengine ya Yesu juu ya ndoa taz Marko 10:11-12; Luka 16:18). Wafafanuzi wengine wanafikiri kwamba hapa labda yahusu ndoa zilizokatazwa katika sheria (rejea Lawi 18:6-18; Hes 25:1).]
33“Tena mmesikia kwamba watu wa kale waliambiwa: ‘Usivunje kiapo chako, bali ni lazima utimize kiapo chako kwa Bwana.’
34Lakini mimi nawaambieni, msiape kamwe; wala kwa mbingu, maana ni kiti cha enzi cha Mungu;[#5:34 Kinachokatazwa hapa ni kutumia jina la Mungu au chochote kilicho chake au kinachotumiwa mahala pake: Yerusalemu (Zab 48:2), mbingu (Mat 23:22), au dunia (Isa 66:1) ili kuthibitisha anachosema mtu. Kinachotakiwa ni “Ndio” au “La” (Yak 5:12). Watu lazima waseme mambo yao kwa unyofu kiasi cha kutohitaji hata kidogo kuapa.]
35wala kwa dunia, maana ni kiti chake cha kuwekea miguu; wala kwa Yerusalemu, maana ni mji wa Mfalme mkuu.
36Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.
37Ukisema, ‘Ndiyo’, basi iwe ‘Ndiyo’; ukisema, ‘Siyo’, basi iwe kweli ‘Siyo’. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu.[#5:37 Taz Yak 5:12.]
38“Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘Jicho kwa jicho, jino kwa jino.’[#5:38 Kut 21:24; Lawi 24:20; Kumb 19:21. Yesu anaonesha hapa njia bora zaidi ya kutumia katika visa vya namna hiyo yaani njia ya upendo.]
39Lakini mimi nawaambieni, usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la kulia, mgeuzie pia la pili.
40Mtu akikupeleka mahakamani kutaka kukuchukulia shati lako, mwache achukue pia koti lako.
41Mtu akikulazimisha kubeba mzigo wake kilomita moja, ubebe kilomita mbili.
42Akuombaye mpe, wala usimpe kisogo anayetaka kukukopa kitu.
43“Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘Mpende jirani yako, na kumchukia adui yako.’[#5:43 Taz Lawi 19:18; lakini kuhusu sehemu ya pili “kumchukia adui yako”.]
44Lakini mimi nawaambieni, wapendeni maadui zenu na kuwaombea wale wanaowadhulumu nyinyi,
45ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu wabaya na wema, na kuwanyeshea mvua watu wanyofu na waovu.
46Je, mtapata tuzo gani kwa kuwapenda tu wale wanaowapenda nyinyi? Hakuna! Kwa maana, hata watozaushuru hufanya hivyo!
47Kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mmefanya kitu kisicho cha kawaida? Hata watu wasiomjua Mungu nao hufanya vivyo hivyo.
48Basi, muwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.[#5:48 (Lawi 19:2; Kumb 18:13). Yesu anawataka wafuasi wake wawe wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni ambaye anawapenda watu wote bila kipimo. Katika Luka 6:36, mwito huo ni wa “kuwa na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma.”]