The chat will start when you send the first message.
1“Jihadharini msije mkafanya matendo yenu mema mbele ya watu kusudi mwonekane nao. La sivyo, Baba yenu aliye mbinguni hatawapeni tuzo.[#6:1-18 Aya hizi zahusu aghalabu matendo yajulikanayo kama matendo ya kidini: kusaidia maskini (2-4), kusali (5-15), na kufunga (16-18). Haya Yesu anatuambia yabidi yafanyike kwa nia na moyo mwema wa utumishi kwa ndugu na kwa Mungu mwenyewe.]
2“Basi, unapomsaidia maskini, usijitangaze. Usifanye kama wanafiki wafanyavyo katika masunagogi na njiani ili watu wawasifu. Kweli nawaambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao.[#6:2 Yaani sifa walizopata kutoka kwa watu ndizo tuzo lao peke yake na hawataambulia lingine. Taz pia 6:5,16.]
3Lakini wewe unapomsaidia maskini, fanya hivyo kwamba hata mwandani wako asijue ufanyalo.
4Toa msaada wako kwa siri, na Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza.
5“Mnaposali, msifanye kama wanafiki. Wao hupenda kusimama na kusali katika masunagogi na katika pembe za njia ili watu wawaone. Kweli nawaambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao.[#6:5 Nyakati za hapo kale kusimama ilikuwa hali ya kawaida ya kusali.; #6:5 Mat 23:5; Luka 18:10-14.]
6Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango, kisha umwombe Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza.[#6:6 Taz Mat 5:12 maelezo.]
7“Mnaposali, msipayuke maneno kama watu wasiomjua Mungu. Wao hudhani kwamba Mungu atawasikiliza ati kwa sababu ya maneno mengi.
8Msiwe kama wao. Baba yenu anajua mnayoyahitaji hata kabla ya kumwomba.
9Basi, hivi ndivyo mnavyopaswa kusali:[#6:9-13 Ni wazi kwamba sala hii ambayo Yesu aliwafundisha wanafunzi wake ni muhimu sana na inajumuisha mahitaji ya kiroho na kimwili ya jumuiya hiyo mpya ya watu wa Mungu. Sala yenyewe ina sehemu mbili za maombi saba. Maombi matatu ya kwanza yamhusu Mungu (jina lako; ufalme wako; utakalo). Mengine manne yanamhusu binadamu yakiwa katika muundo na maana ya kijumuiya “sisi” na sio mmojammoja. Rejea Luka 11:2-4.]
‘Baba yetu uliye mbinguni:
Jina lako litukuzwe.
10Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni.
11Utupe leo chakula chetu cha kila siku.[#6:11 Tafsiri ya aya hii ni ngumu kidogo “chakula chetu cha kila siku”, au: “tunachohitaji”, au: “cha leo” au “cha kesho”. Rejea Kut 16:4; Meth 30:8-9; zingatia pia nadharia ya mkate katika Yoh 6:32-35. Ni dhahiri lakini kwamba Yesu aliwataka wafuasi wake waombe chakula chao au mahitaji yao ya siku kwa siku.]
12Utusamehe makosa yetu,[#6:12 Au, “madeni yetu” neno ambalo lilitumika hapo kale katika utamaduni wa Wayahudi kwa maana ya aliyowiwa mtu au dhambi zilizotendwa (rejea Mat 18:23-25).]
kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea.
13Usitutie katika majaribu,[#6:13 Hati nyingine za kale zinaongeza hapa maneno: “Kwa kuwa ufalme ni wako na nguvu na utukufu milele. Amina.”; #6:13 Hapa Mungu anaombwa atuokoe katika majaribu yanayoweza kuhatarisha uhusiano wetu naye. Rejea Mat 26:41; 1Kor 10:13. Katika Mat 4:1-11; 16:1 tuna namna nyingine za majaribu au vishawishi. Tazama pia Yak 1:12-14.]
lakini utuokoe na yule Mwovu.’
14“Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi pia.
15Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe nyinyi makosa yenu.
16“Mnapofunga, msiwe na huzuni kama wanafiki. Wao hukunja nyuso zao wapate kuonekana na watu kuwa wanafunga. Nawaambieni kweli, hao wamekwisha pata tuzo lao.
17Wewe lakini unapofunga, paka kichwa chako mafuta, nawa uso wako,
18ili mtu yeyote asijue kwamba unafunga, ila ujulikane tu kwa Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza.
19“Msijiwekee hazina hapa duniani ambako nondo na kutu huharibu, na wezi huingia na kuiba.
20Jiwekeeni hazina mbinguni ambako nondo na kutu hawawezi kuiharibu, wala wezi hawaingii wakaiba.
21Maana pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.
22“Jicho ni taa ya mwili. Kama basi jicho lako ni zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga.
23Lakini ikiwa jicho lako ni bovu, mwili wako wote utakuwa katika giza. Basi, ikiwa mwanga uliomo ndani yako ni giza, basi, hilo ni giza la kutisha mno!
24“Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili. Maana atamchukia mmoja na kumpenda huyo wa pili; au ataambatana na mmoja na kumdharau huyo mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali pamoja.[#6:24 Kigiriki: “Mamon” neno ambalo lina maana ya mali, picha ya nguvu inayotawala ulimwengu.]
25“Ndiyo maana nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula na kinywaji mnavyohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. Je, maisha ni chakula tu au zaidi? Na mwili, je, si zaidi ya mavazi?
26Waangalieni ndege wa mwituni: hawapandi, hawavuni, wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, nyinyi si wa thamani kuliko hao?
27Ni nani miongoni mwenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuuongeza muda wa maisha yake?[#6:27 Tafsiri nyingine: “kimo chake”.]
28“Na kuhusu mavazi, ya nini kuwa na wasiwasi? Tazameni maua ya porini jinsi yanavyostawi. Hayafanyi kazi wala hayasokoti.
29Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo.[#6:29 1Fal 10:4—7:23. Solomoni alijulikana kwa Wayahudi wa wakati wake kuwa mtu mwenye fahari kuliko wote duniani]
30Ikiwa basi, Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, si atawafanyia nyinyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba!
31“Basi, msiwe na wasiwasi: ‘Tutakula nini, tutakunywa nini, tutavaa nini!’
32Maana hayo yote yanahangaikiwa na watu wasiomjua Mungu. Baba yenu wa mbinguni anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo vyote.
33Bali, shughulikeni kwanza juu ya ufalme wa Mungu na matakwa yake, na hayo yote mtapewa kwa ziada.[#6:33 Taz Mat 3:15.; #6:33 Zab 37:4.]
34Basi, msiwe na wasiwasi juu ya kesho; kesho inayo yake. Matatizo ya siku moja yanawatosheni kwa siku hiyo.