Hesabu 9

Hesabu 9

Pasaka ya pili

1Kisha mnamo mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kutoka Misri, Mwenyezi-Mungu aliongea na Mose katika jangwa la Sinai. Alimwambia:[#9:1 Mwezi wa kwanza katika kalenda ya Wayahudi uliitwa Abibu au Nisani (kuanzia katikati ya mwezi Machi mpaka katikati ya mwezi Aprili kadiri ya kalenda yetu).]

2“Waisraeli sharti waiadhimishe sikukuu ya Pasaka wakati uliopangwa.[#9:2 Kuhusu maana ya jina Pasaka, taz Kut 12:13,23-25. Sikukuu hiyo iliadhimishwa kukumbuka jinsi Mungu alivyowaokoa Waisraeli nchini Misri.]

3Hii itakuwa siku ya kumi na nne ya mwezi huu; wakati wa jioni watafanya hivyo kufuatana na masharti na maagizo yake yote.”

4Kwa hiyo, Mose akawaambia watu kwamba wanapaswa kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka.

5Basi, wakaiadhimisha Pasaka jioni, siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, katika jangwa la Sinai. Waisraeli walifanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.

6Lakini, baadhi ya watu waliokuwapo walikuwa hawawezi kuiadhimisha sikukuu hiyo ya Pasaka kwa sababu walikuwa wamegusa maiti, wakawa najisi. Hao waliwaendea Mose na Aroni,

7wakawaambia, “Sisi tu najisi kwa kuwa tumegusa maiti, lakini kwa nini tukatazwe kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka zake kwa wakati uliopangwa pamoja na Waisraeli wengine?”

8Mose akawajibu, “Ngojeni mpaka hapo nitakapopata maagizo juu yenu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu.”

9Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

10“Mmoja wenu au mmoja wa wazawa wenu akiwa najisi kwa sababu amegusa maiti au akiwa mbali safarini, lakini akiwa anataka kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka,

11mtu kama huyo anaruhusiwa kufanya hivyo mwezi mmoja baadaye, jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Ataiadhimisha kwa kula mikate isiyotiwa chachu na mboga chungu.

12Wasibakize chakula chochote hadi asubuhi, wala wasivunje hata mfupa mmoja wa wanyama wa Pasaka. Wataiadhimisha sikukuu hii ya Pasaka kulingana na kanuni zake zote.

13Lakini mtu yeyote ambaye ni safi au hayumo safarini, asipoiadhimisha sikukuu ya Pasaka, atatengwa na watu wake kwa kuwa hakunitolea sadaka kwa wakati uliopangwa. Ni lazima aadhibiwe kwa ajili ya dhambi yake.

14“Ikiwa kuna mgeni anayeishi pamoja nanyi na anapenda kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka, mtu huyo sharti afanye hivyo kulingana na masharti na maagizo yote ya Pasaka. Kila mtu atafuata masharti yaleyale, akiwa mgeni au mwenyeji.”[#9:14 Huyo alikuwa mtu asiye Mwisraeli ambaye alihamia na kuishi kati ya Waisraeli. Wageni wanaume ambao walitaka kuadhimisha Pasaka waliruhusiwa kufanya hivyo kama walikuwa wametahiriwa (taz Kut 12:48-49).]

Wingu la moto

(Kut 40:34-38)

15Siku ambayo hema takatifu lilisimikwa, wingu lilishuka na kulifunika hema la maamuzi. Wakati wa usiku wingu hilo lilionekana kama moto mpaka asubuhi.[#9:15 Yahusu wakati ule ule unaotajwa katika Kut 40:17 na wakati wa matayarisho ya kuondoka jangwani Sinai (Hes 10:11-28).]

16Hivyo ndivyo ilivyokuwa kila siku; wingu lililifunika hema mchana, na usiku lilionekana kama moto.[#9:15-16 Moto, wingu, moshi mara nyingi katika Biblia ni matukio yanayoashiria kuweko kwake Mungu (taz pia Mwa 15:17-18; Kut 3:1-6; 16:10; 19:16-19; 24:15-18; Amu 13:20; Ufu 1:12-16). Wakati wa safari za Waisraeli jangwani Mungu alitumia wingu kuwaongoza.]

17Kila mara wingu hilo lilipoinuliwa juu ya hema, Waisraeli walivunja kambi na kupiga kambi tena mahali wingu hilo lilipotua.

18Walisafiri kwa amri ya Mwenyezi-Mungu, na kupiga kambi tena kwa amri yake. Muda wote wingu hilo lilipokuwa juu ya hema, watu walikaa katika kambi hiyo.

19Hata kama wingu hilo lilikaa juu ya hema kwa muda wa siku nyingi, Waisraeli walimtii Mwenyezi-Mungu, nao hawakuondoka.

20Wakati mwingine wingu hilo lilikaa juu ya hema kwa muda wa siku chache tu; lakini kila wakati Waisraeli walibaki kambini; walihama kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru.

21Wakati mwingine wingu lilikaa juu ya hema tangu jioni mpaka asubuhi tu; na mara tu lilipoinuliwa, hao watu pia walifunga safari. Na ikiwa lilikaa juu ya hema mchana kutwa na usiku kucha, wao waliondoka tu wingu lilipoinuliwa.

22Ikiwa ni siku mbili, mwezi, mwaka au zaidi, muda wote wingu hilo lilipokuwa juu ya hema, Waisraeli hawakuhama; lakini lilipoinuliwa, nao pia walihama.

23Kwa agizo la Mwenyezi-Mungu walipiga kambi na kwa agizo la Mwenyezi-Mungu walisafiri. Walishika agizo la Mwenyezi-Mungu kama alivyotoa amri yake kwa njia ya Mose.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania