Zaburi 16

Zaburi 16

Kuomba usalama

1Unilinde ee Mungu;

maana kwako nakimbilia usalama.

2Namwambia Mungu: “Wewe u Bwana wangu;

sina jema lolote ila wewe.”

3Ni bora sana hao watakatifu walioko nchini,

kukaa nao ndiyo furaha yangu.

4Lakini wanaoabudu miungu mingine,

watapata mateso mengi.

tambiko ya damu sitaitolea kamwe,

na majina ya miungu hiyo sitayataja.

5Wewe ee Mwenyezi-Mungu ndiwe riziki yangu kuu,

majaliwa yangu yamo mikononi mwako.

6Umenipimia sehemu nzuri sana;

naam, urithi wangu ni wa kupendeza.

7Namsifu Mwenyezi-Mungu kwa kuniongoza,

usiku dhamiri yangu yanionya.

8Namweka Mwenyezi-Mungu mbele yangu daima;

yuko pamoja nami, wala sitatikisika.

9Kwa hiyo nitafurahi kwa moyo wote na kushangilia,

nami nitakaa salama salimini.

10Naam wewe hutaiacha nafsi yangu kuzimu,

hutaniacha mimi mwaminifu wako nipate kuoza.

11Wanionesha njia ya kufikia uhai;

kuwako kwako kwanijaza furaha kamili,

katika mkono wako wa nguvu mna mema ya milele.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania