The chat will start when you send the first message.
1Ee Mwenyezi-Mungu,
umeifadhili nchi yako;
umemjalia Yakobo bahati nzuri tena.
2Umewasamehe watu wako kosa lao;
umezifuta dhambi zao zote.
3Umeizuia ghadhabu yako yote;
umeiacha hasira yako kali.
4Uturekebishe tena, ee Mungu mwokozi wetu;
uiondoe chuki uliyo nayo juu yetu.
5Je, utatukasirikia hata milele?[#85:5 Kuhusu lugha kama hiyo taz 74:1; 79:5.]
Je, utadumisha ghadhabu yako kwa vizazi vyote?
6Je, hutatujalia tena maisha mapya,
ili watu wako wafurahi kwa sababu yako?
7Utuoneshe, fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu,
utujalie wokovu wako.
8Hebu nisikie anachosema Mwenyezi-Mungu;
maana anaahidi kuwapa watu wake amani,
watu wake mwenyewe wasiporudia upuuzi wao
9Hakika yu tayari kuwaokoa wanaomheshimu,
na utukufu wake utadumu nchini mwetu.
10Fadhili zake na uaminifu vitakutana;
uadilifu na amani vitaungana.
11Uaminifu utachipuka katika nchi;
uadilifu utashuka toka mbinguni.
12Naam, Mwenyezi-Mungu atatuletea fanaka,
na nchi yetu itatoa mazao yake mengi.
13Uadilifu utamtangulia Mungu
na kumtayarishia njia yake.