The chat will start when you send the first message.
1Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu mwenye kulipiza kisasi,
ewe Mungu mlipiza kisasi, ujitokeze!
2Usimame, ee hakimu wa watu wote;
uwaadhibu wenye kiburi wanavyostahili!
3Waovu wataona fahari hata lini?
Watajisifia mpaka lini, ee Mwenyezi-Mungu?
4Hata lini waovu watajigamba kwa maneno?[#94:4 Mwanazaburi hapa anamsihi Mwenyezi-Mungu akomeshe kufanikiwa kwa hao waovu.]
Waovu wote watajivuna mpaka lini?
5Wanawaangamiza watu wako, ee Mwenyezi-Mungu,
wanawakandamiza hao walio mali yako.
6Wanawaua wajane na wageni;
wanawachinja yatima!
7Wanasema: “Mwenyezi-Mungu haoni,[#94:5-7 Kuhusu mawazo ya hao waovu kwamba Mungu haoni, taz pia 10:11; 14:1.]
Mungu wa Yakobo hajui!”
8Enyi wajinga wa mwisho, fikirini kidogo!
Enyi wapumbavu, mtapata lini maarifa?
9Aliyefanya sikio, je, hawezi kusikia?
Aliyeumba jicho, je, hawezi kuona?
10Mwenye kutawala mataifa, je, hawezi kuadhibu?[#94:10 Mungu ambaye huadhibu mataifa mengine hakika atawaadhibu viongozi dhalimu wa Israeli. Ni dhahiri kwamba maswali yanayoulizwa hapa si maswali ya kujibu ila yana shabaha ya kutilia mkazo jambo linalohusika na kwa namna nyingine kuwakebehi hao wanaofikiri hivyo.]
Mkufunzi wa wanadamu, je, hana maarifa?
11Mwenyezi-Mungu ayajua mawazo ya watu;[#94:11 Aya hii inanukuliwa katika 1Kor 3:20 (kulingana na tafsiri ya Kigiriki ya Septuajinta-LXX) ambapo Paulo anaitumia kwa watu ambao kidunia walifikiriwa kuwa wenye hekima.]
anajua kwamba hayafai kitu.
12Heri mtu unayemfunza nidhamu, ee Mwenyezi-Mungu,
mtu unayemfundisha sheria yako,
13ili siku ya taabu apate utulivu,
hadi waovu wachimbiwe shimo.
14Mwenyezi-Mungu hatawaacha watu wake;
hatawatupa hao walio mali yake.
15Maana hukumu zitatolewa kwa haki tena,
na wanyofu wote wa moyo wataizingatia.
16Nani aliyenisaidia kumpinga mtu mwovu?
Nani aliyekuwa upande wangu dhidi ya wabaya?
17Mwenyezi-Mungu asingalinisaidia,
ningalikwisha kwenda kwenye nchi ya wafu.
18Nilipohisi kwamba ninateleza,
fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, zilinitegemeza.
19Mahangaiko ya moyo wangu yanapozidi,
wewe wanifariji na kunifurahisha.
20Wewe huwezi kushirikiana na mahakimu dhalimu,[#94:20 Kwa kujisingizia kuheshimu sheria, hao viongozi dhalimu wanawatesa watu wasio na hatia. Manabii wa Israeli waliwalaumu vikali watawala ambao walipuuza matakwa ya Mungu kuhusu haki za watu na kuwaonea maskini (taz Isa 1:21-23; 5:8-24; Amo 2:6-7; 5:10-12; Mika 2:1-2).]
wanaotunga kanuni za kutetea maovu.
21Wao wanaafikiana kuwaangamiza waadilifu,
na kuwahukumu watu wasio na hatia wauawe.
22Lakini Mwenyezi-Mungu ni ngome yangu;
Mungu wangu ni mwamba wa usalama wangu.
23Uovu wao atawarudishia wao wenyewe,
atawafutilia mbali kwa sababu ya ubaya wao.
Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, atawafutilia mbali!