The chat will start when you send the first message.
1Baada ya hayo nikawaona malaika wanne wamesimama katika pembe nne za dunia, wakishika pepo nne za dunia ili upepo usivume hata kidogo: wala katika nchi, wala baharini, wala kwenye miti.[#7:1 Kulingana na pande nne za dunia na kwa maana ya ulimwengu wote.; #7:1-17 Sura hii inatenga kufunguliwa mhuri wa sita na wa saba ambayo yaonesha jinsi Mungu anavyohakikisha kwamba watu wake wanaokolewa.]
2Kisha, nikamwona malaika mwingine akipanda juu kutoka mashariki, akiwa na mhuri wa Mungu aliye hai. Akapaza sauti na kuwaambia hao malaika wanne waliokabidhiwa jukumu la kuiharibu nchi na bahari,
3“Msiharibu nchi, wala bahari, wala miti, mpaka tutakapokwisha wapiga mhuri watumishi wa Mungu wetu katika paji la uso.”[#7:3 Eze 9:4-6; ling Ufu 2:17; 22:4. Hapa mhuri ni alama wanayowekewa wale walio wake Mungu ambaye anawalinda wakati wa majaribu (taz 3:10; 9:4). Ling 2Kor 1:22; Efe 1:13; 4:30.]
4Kisha, nikasikia idadi ya hao waliopigwa mhuri: Watu 144,000 wa makabila yote ya watu wa Israeli.[#7:4 Idadi au tarakimu 144,000 inamaanisha kwa mfano jumla ya watu wote wa Mungu. Labda hapa ni marejeo ya halaiki ile inayotajwa katika 7:9-17.]
5Kabila la Yuda, watu 12,000; kabila la Reubeni, 12,000; kabila la Gadi, 12,000;[#7:5-8 Orodha ya makabila kumi na mawili ya Israeli inatumika kama mfano, nayo yahitilafiana na orodha nyingine katika A.K. (Mwa 49; Eze 48). Hapa makabila ya Dani na Efraimu hayatajwi badala yake ni makabila ya Yosefu na mwanae Manase.]
6kabila la Asheri, 12,000; kabila la Naftali, 12,000; kabila la Manase, 12,000;
7kabila la Simeoni, 12,000; kabila la Lawi, 12,000; kabila la Isakari, 12,000;
8kabila la Zebuluni, 12,000; kabila la Yosefu, 12,000; na kabila la Benyamini, 12,000.
9Kisha, nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu wasiohesabika: watu wa kila taifa, ukoo, jamaa na lugha. Nao walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo, wamevaa mavazi meupe na kushika matawi ya mitende mikononi mwao.[#7:9 Ishara au mfano wa ushindi (Yoh 12:13).]
10Wakapaza sauti: “Ukombozi wetu watoka kwa Mungu wetu aketiye juu ya kiti cha enzi, na kutoka kwa Mwanakondoo!”
11Malaika wote wakasimama kukizunguka kiti cha enzi, wazee na wale viumbe hai wanne. Wakaanguka kifudifudi mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu,
12wakisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, uwezo na nguvu viwe kwa Mungu wetu, milele na milele! Amina!”[#7:12 Taz maelezo ya 1:6.]
13Mmoja wa hao wazee akaniuliza, “Hawa waliovaa mavazi meupe ni watu gani? Na wametoka wapi?”
14Nami nikamjibu, “Mheshimiwa, wewe wajua!” Naye akaniambia, “Hawa ni wale waliopita salama katika ule udhalimu mkuu. Waliyaosha mavazi yao katika damu ya Mwanakondoo, yakawa meupe kabisa.[#7:14 Dan 12:1; Mat 24:21; Marko 13:19; ling Ufu 3:10.; #7:14 Maneno yanayotumika kama mfano kutaja kutakaswa kwa hao watu kutoka dhambi ni kwa kifo cha Kristo chenye kuwakomboa watu. Ling Yoh 1:29; 1Yoh 1:7 na pia Ufu 1:5; 3:5; 6:11.]
15Ndiyo maana wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Humtumikia Mungu mchana na usiku katika hekalu lake; naye aketiye juu ya kiti cha enzi atatandaza hema lake juu yao kuwalinda.
16Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena,[#7:16 Isa 49:10; ling Zab 121:6. Aya 16-17 zinanukua makala kadhaa kutoka A.K.]
17kwa sababu Mwanakondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uhai. Naye Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao.”[#7:17 Kutokana na kifo chake Mwanakondoo, kifo ambacho kinawakomboa watu, huyo Mwanakondoo pia ni Mchungaji Mwema mwenye kuwaongoza kondoo, kuwalinda na kuwatawala kutoka kwenye kiti chake cha enzi (Ling Eze 34:23; Yoh 10:1-16; Ebr 13:20; 1Pet 2:25 na pia Ufu 22:1-5).; #7:17 Zab 23:1-2; Isa 49:10 ling Yoh 4:10; 7:37-38.; #7:17 Isa 25:8; Ufu 21:4.]