2 Wafalme 2

2 Wafalme 2

Eliya achukuliwa mbinguni

1Bwana alipokuwa karibu kumchukua Eliya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya na Elisha walikuwa njiani wakitoka Gilgali.

2Eliya akamwambia Elisha, “Kaa hapa. Bwana amenituma Betheli.”

Lakini Elisha akasema, “Hakika kama Bwana aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Kwa hiyo wakaenda Betheli pamoja.

3Wana wa manabii waliokuwa Betheli wakamjia Elisha na kumuuliza, “Je, unajua kwamba Bwana atakuondolea bwana wako leo?”

Elisha akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze kuhusu jambo hilo.”

4Kisha Eliya akamwambia, “Baki hapa, Elisha. Bwana amenituma Yeriko.”

Naye akajibu, “Kwa hakika kama Bwana aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wakaenda Yeriko.

5Wana wa manabii waliokuwa Yeriko wakamwendea Elisha na kumuuliza, “Je, unajua kwamba Bwana atakuondolea bwana wako leo?”

Akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze juu ya jambo hilo.”

6Kisha Eliya akamwambia, “Kaa hapa. Bwana amenituma kwenda Yordani.”

Naye akamjibu, “Kwa hakika kama Bwana aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wote wawili wakaendelea pamoja.

7Wana hamsini wa manabii wakaenda na kusimama kwa mbali, kuelekea mahali Eliya na Elisha waliposimama kando ya Mto Yordani.

8Eliya akatoa vazi lake, akalikunja na kupiga maji nalo. Maji yakagawanyika upande wa kuume na upande wa kushoto, nao wawili wakavuka pakavu.

9Walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, “Niambie, nikufanyie nini kabla sijaondolewa kutoka kwako?”

Elisha akajibu, “Naomba nirithi sehemu maradufu ya roho yako.”

10Eliya akasema, “Umeomba jambo gumu. Lakini kama utaniona wakati ninapoondolewa kutoka kwako litakuwa lako. La sivyo, hutalipata.”

11Walipokuwa wakitembea pamoja na kuzungumza, ghafula gari la farasi la moto na farasi wa moto vilitokea na kuwatenganisha wao wawili, naye Eliya akapanda mbinguni katika upepo wa kisulisuli.

12Elisha aliliona hili, naye akapaza sauti, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya vita ya Israeli na wapanda farasi wake!” Naye Elisha hakumwona tena. Kisha akaishika nguo yake na kuirarua vipande viwili.

13Akaliokota lile vazi lililoanguka kutoka kwa Eliya, kisha akarudi na kusimama ukingoni mwa Yordani.

14Ndipo akalichukua lile vazi ambalo lilikuwa limeanguka kutoka kwa Eliya, naye akayapiga yale maji nalo. Akauliza, “Yuko wapi sasa Bwana , Mungu wa Eliya?” Elisha alipoyapiga maji, yakagawanyika kulia na kushoto, naye akavuka.

15Wale wana wa manabii kutoka Yeriko waliokuwa wakitazama wakasema, “Roho ya Eliya inamkalia Elisha.” Nao wakaenda kumlaki na kusujudu hadi chini mbele yake.

16Wakasema, “Tazama, sisi watumishi wako tunao watu hamsini wenye uwezo. Waruhusu waende kumtafuta bwana wako. Labda Roho wa Bwana amemtwaa na kumweka katika mlima fulani au bonde fulani.”

Elisha akajibu, “Hapana, msiwatume.”

17Lakini wakasisitiza, hata akaona aibu kuwakatalia. Hivyo akasema, “Watumeni.” Nao wakawatuma watu hamsini, wakamtafuta kwa siku tatu, lakini hawakumpata.

18Walipomrudia Elisha, aliyekuwa akingojea huko Yeriko, akawaambia, “Je, sikuwaambia msiende?”

Kuponywa kwa maji

19Watu wa mji wakamwambia Elisha, “Tazama, bwana wetu, mahali mji huu ulipojengwa ni pazuri, kama bwana wangu anavyoona, lakini maji yake ni mabaya, na nchi haina mazao.”

20Akasema, “Nileteeni bakuli mpya, mweke chumvi ndani yake.” Kwa hiyo wakamletea.

21Kisha akaenda kwenye chemchemi na kuitupa ile chumvi ndani yake, akisema, “Hili ndilo asemalo Bwana : ‘Nimeyaponya maji haya. Kamwe hayatasababisha mauti tena wala kutozaa.’ ”

22Nayo yale maji yakaponywa hadi leo, sawasawa na neno la Elisha alilokuwa amesema.

Elisha afanyiwa mzaha

23Kutoka huko Elisha akakwea kwenda Betheli. Ikawa alipokuwa akitembea barabarani, baadhi ya vijana wakatoka mjini na kumfanyia mzaha. Wakasema, “Paa, wewe mwenye upara! Paa, wewe mwenye upara!”

24Akageuka, akawatazama na kuwalaani kwa Jina la Bwana . Kisha dubu jike wawili wakatokea mwituni na kuwararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao.

25Naye akaondoka huko, akaenda Mlima Karmeli, na kutoka huko akarudi Samaria.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.