Mhubiri 11

Mhubiri 11

Mkate juu ya maji

1Tupa mkate wako juu ya maji,

kwa maana baada ya siku nyingi

utaupata tena.

2Wape sehemu watu saba, naam hata wanane,

kwa maana hujui ni baa gani

litakalokuwa juu ya nchi.

3Kama mawingu yamejaa maji,

hunyesha mvua juu ya nchi.

Kama mti ukianguka kuelekea kusini

au kuelekea kaskazini,

mahali ulipoangukia,

hapo ndipo utakapolala.

4Yeyote atazamaye upepo hatapanda,

yeyote anayeangalia mawingu hatavuna.

5Kama vile usivyofahamu njia ya upepo,

au jinsi mwili uumbwavyo

ndani ya tumbo la mama,

vivyo hivyo huwezi kufahamu kazi ya Mungu,

Muumba wa vitu vyote.

6Panda mbegu yako asubuhi,

nako jioni usiruhusu mikono yako ilegee,

kwa maana hujui ni ipi itakayofanikiwa,

kwamba ni hii au ni ile,

au kwamba zote zitafanikiwa sawasawa.

Mkumbuke Muumba wako ukiwa bado kijana

7Nuru ni tamu,

tena inafurahisha macho kuona jua.

8Mtu akiishi miaka mingi kiasi gani,

na aifurahie yote.

Lakini akumbuke siku za giza,

kwa maana zitakuwa nyingi.

Kila kitu kitakachokuja ni ubatili.

9Furahi ewe kijana, ukiwa bado kijana,

moyo wako na ukupe furaha

siku za ujana wako.

Fuata njia za moyo wako

na chochote macho yako yanaona,

lakini ujue kwamba kwa ajili ya haya yote

Mungu atakuleta hukumuni.

10Kwa hiyo, ondoa wasiwasi moyoni mwako

na utupilie mbali masumbufu ya mwili wako,

kwa kuwa ujana na nguvu ni ubatili.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.