Mhubiri 7

Mhubiri 7

Hekima

1Afadhali sifa nzuri kuliko manukato safi,

nayo siku ya kufa kuliko ya kuzaliwa.

2Afadhali kwenda kwenye nyumba ya msiba

kuliko kwenda kwenye nyumba ya karamu,

kwa kuwa kifo ni hatima ya kila mwanadamu,

imewapasa walio hai kuliweka hili mioyoni mwao.

3Huzuni ni afadhali kuliko kicheko,

kwa sababu uso wenye huzuni wafaa kwa moyo.

4Moyo wa wenye hekima uko katika nyumba ya msiba,

lakini moyo wa wapumbavu uko katika nyumba ya anasa.

5Afadhali kusikia karipio la mtu mwenye hekima,

kuliko kusikiliza wimbo wa wapumbavu.

6Kama ilivyo kuvunjika kwa miiba chini ya sufuria,

ndivyo kilivyo kicheko cha wapumbavu.

Hili nalo pia ni ubatili.

7Dhuluma humfanya mtu mwenye hekima kuwa mpumbavu,

nayo rushwa huuharibu moyo.

8Mwisho wa jambo ni bora kuliko mwanzo wake,

uvumilivu ni bora kuliko kiburi.

9Usiwe mwepesi kukasirika rohoni mwako,

kwa kuwa hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.

10Usiseme, “Kwa nini siku za kale

zilikuwa bora kuliko siku hizi?”

Kwa maana si hekima

kuuliza maswali kama hayo.

11Hekima, kama ulivyo urithi, ni kitu chema

na huwafaidia wale walionalo jua.

12Hekima ni ulinzi

kama fedha ilivyo ulinzi,

lakini faida ya maarifa ni hii:

kwamba hekima huhifadhi maisha ya aliye nayo.

13Tafakari kile Mungu alichokitenda:

Nani awezaye kunyoosha

kile ambacho yeye amekipinda?

14Nyakati zikiwa nzuri, ufurahi,

lakini nyakati zikiwa mbaya, tafakari hili:

Mungu amefanya hiyo moja;

naam, pia na hiyo nyingine.

Kwa hiyo, mwanadamu hawezi kugundua

kitu chochote kuhusu maisha yake ya baadaye.

15Katika maisha haya yangu ya ubatili nimeshaona haya mawili:

mtu mwadilifu akiangamia katika uadilifu wake,

naye mtu mwovu akiishi maisha marefu katika uovu wake.

16Usiwe mwenye haki kupita kiasi,

wala usiwe na hekima kupita kiasi:

kwa nini kujiangamiza mwenyewe?

17Usiwe mwovu kupita kiasi,

wala usiwe mpumbavu:

kwa nini kufa kabla ya wakati wako?

18Ni vyema kushika hilo moja

na wala usiache hilo jingine likupite.

Mtu amchaye Mungu ataepuka huko kupita kiasi.

19Hekima humfanya yeye aliye nayo kuwa na uwezo

kuliko watawala kumi katika mji.

20Hakuna mtu mwenye haki duniani

ambaye hufanya mambo ya haki

na kamwe asitende dhambi.

21Usitie maanani kila neno linalosemwa na watu,

la sivyo, unaweza kumsikia

mtumishi wako akikulaani:

22kwa kuwa unafahamu moyoni mwako

kwamba wewe mwenyewe mara nyingi

umewalaani wengine.

23Yote haya niliyajaribu kwa hekima, nikasema,

“Nimeamua kuwa na hekima”:

lakini hii ilikuwa nje ya uwezo wangu.

24Vyovyote hekima ilivyo,

hekima iko mbali sana na imejificha,

ni nani awezaye kuigundua?

25Nikageuza fikira zangu ili kuelewa,

kuchunguza na kuitafuta hekima

na kusudi la mambo,

na ili kuelewa ujinga wa uovu,

na wazimu wa upumbavu.

26Nimeona jambo lililo chungu kuliko mauti,

mwanamke ambaye ni mtego,

ambaye moyo wake ni wavu wa kutegea

na mikono yake ni minyororo.

Mtu ampendezaye Mungu atamkwepa,

bali mwenye dhambi atanaswa naye.

27Mhubiri anasema, “Tazama, hili ndilo nililogundua:

“Nimegundua kitu kimoja baada ya kingine nilipokuwa katika kusudi la mambo:

28ningali natafiti

lakini sipati:

nilimpata mwanaume mmoja mnyofu miongoni mwa elfu,

lakini hakuna mwanamke mmoja mnyofu miongoni mwao.

29Hili ndilo peke yake nililolipata:

Mungu amemuumba mwanadamu mnyofu,

lakini mwanadamu amebuni mambo mengi.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.