The chat will start when you send the first message.
1Katika siku ya ishirini na moja ya mwezi wa saba, neno la Bwana lilikuja kupitia nabii Hagai, kusema:
2“Sema na Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki, na mabaki ya watu. Uwaulize,
3‘Ni nani miongoni mwenu aliyebaki ambaye aliiona hii nyumba katika utukufu wake wa mwanzo? Sasa inaonekanaje kwenu? Je, haionekani kwenu kama si kitu?
4Lakini sasa uwe imara, ee Zerubabeli,’ asema Bwana . ‘Kuwa imara, ee kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Mwe imara, enyi watu wote wa nchi,’ asema Bwana , ‘na mfanye kazi. Kwa kuwa mimi nipo pamoja nanyi,’ asema Bwana wa majeshi.
5‘Hili ndilo nililoagana nanyi mlipotoka katika nchi ya Misri. Pia Roho wangu anadumu kati yenu. Msiogope.’
6“Hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi: ‘Baada ya muda kidogo kwa mara nyingine nitazitikisa mbingu na nchi, bahari na nchi kavu.
7Nitatikisa mataifa yote, nacho kile kinachotamaniwa na mataifa yote kitakuja, nami nitaujaza utukufu katika nyumba hii,’ asema Bwana wa majeshi.
8‘Fedha ni mali yangu na dhahabu ni mali yangu,’ asema Bwana wa majeshi.
9‘Utukufu wa nyumba hii ya sasa utakuwa mkubwa kuliko utukufu wa ile nyumba ya mwanzoni,’ asema Bwana wa majeshi. ‘Na mahali hapa nitawapa amani,’ asema Bwana wa majeshi.”
10Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Bwana lilikuja kwa nabii Hagai:
11“Hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi: ‘Ulizeni makuhani jinsi sheria inavyosema:
12Kama mtu akibeba nyama iliyowekwa wakfu katika pindo la vazi lake, kisha lile pindo likagusa mkate au mchuzi, divai, mafuta au chakula kingine, je, kitu hicho kitakuwa kimewekwa wakfu?’ ”
Makuhani wakajibu, “La.”
13Kisha Hagai akasema, “Je, kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti akigusa mojawapo ya vitu hivi, kitu hicho kitakuwa kimetiwa unajisi?”
Makuhani wakajibu, “Ndiyo, huwa kimenajisiwa.”
14Kisha Hagai akasema, “ ‘Basi ndivyo walivyo machoni pangu hawa watu na taifa hili,’ asema Bwana . ‘Lolote wafanyalo na chochote watoacho hapo ni najisi.
15“ ‘Sasa fikirini kwa uangalifu kuanzia leo na kuendelea: tafakarini jinsi mambo yalivyokuwa kabla halijawekwa jiwe moja juu ya lingine katika Hekalu la Bwana .
16Mtu alipoendea lundo la nafaka la vipimo ishirini, kulikuwa na vipimo kumi tu. Mtu alipoendea pipa la mvinyo ili kuchota vipimo hamsini, kulikuwa na vipimo ishirini tu.
17Kazi zenu zote za mikono nilizipiga kwa ukame, ukungu na mvua ya mawe, lakini hata hivyo, hamkunigeukia mimi,’ asema Bwana .
18‘Tangu leo na kuendelea, kuanzia siku hii ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, tafakarini siku ambayo msingi wa Hekalu la Bwana uliwekwa. Tafakarini:
19Je, bado kuna mbegu iliyobakia ghalani? Hadi sasa, hakuna mzabibu au mtini, mkomamanga wala mzeituni uliozaa tunda.
“ ‘Kuanzia leo na kuendelea, nitawabariki.’ ”
20Neno la Bwana likamjia Hagai kwa mara ya pili katika siku ya ishirini na nne ya mwezi kusema:
21“Mwambie Zerubabeli mtawala wa Yuda kwamba nitazitikisa mbingu na nchi.
22Nitapindua viti vya falme, na kuziharibu kabisa nguvu za falme za kigeni. Nitapindua magari ya vita pamoja na waendeshaji wake; farasi na wapanda farasi wataanguka, kila mmoja kwa upanga wa ndugu yake.
23“ ‘Katika siku ile,’ asema Bwana wa majeshi, ‘nitakuchukua wewe, mtumishi wangu Zerubabeli mwana wa Shealtieli,’ asema Bwana . ‘Nitakufanya kama pete yangu ya muhuri, kwa kuwa nimekuchagua,’ asema Bwana wa majeshi.”