The chat will start when you send the first message.
1Ole kwa nchi ya mvumo wa mabawa,[#18:1 au wa nzige]
kando ya mito ya Kushi,
2iwapelekayo wajumbe wake kupitia bahari
kwa mashua za mafunjo juu ya maji.
Nendeni, wajumbe wepesi,
kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo,
kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu,
taifa gomvi lenye lugha ngeni,
ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito.
3Enyi mataifa yote ya ulimwengu,
ninyi mnaoishi duniani
wakati bendera itakapoinuliwa milimani,
mtaiona,
nayo tarumbeta itakapolia,
mtaisikia.
4Hili ndilo Bwana aliloniambia:
“Nitatulia kimya na kutazama
kutoka maskani yangu,
kama joto linalometameta katika mwanga wa jua,
kama wingu la umande
katika joto la wakati wa mavuno.”
5Kwa maana, kabla ya mavuno,
wakati wa kuchanua ukishapita
na maua yakawa zabibu zinazoiva,
atayakata machipukizi kwa mundu wa kupogolea matawi,
naye atakata na kuyaondoa matawi yaliyopanuka.
6Yote yataachwa kwa ajili ya ndege wawindao wa mlimani
na wanyama pori,
ndege watajilisha juu yake wakati wote wa kiangazi,
nao wanyama pori wakati wote wa masika.
7Wakati huo matoleo yataletwa kwa Bwana wa majeshi
kutoka kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo,
kutoka kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu,
kutoka taifa gomvi lenye lugha ngeni,
ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito,
matoleo yataletwa katika Mlima Sayuni, mahali pa Jina la Bwana wa majeshi.