The chat will start when you send the first message.
1Hapo mwanzo alikuwako Neno, naye huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
2Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.
3Vitu vyote viliumbwa kupitia kwake, na hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa pasipo yeye.
4Ndani yake kulikuwa na uzima, nao huo uzima ulikuwa nuru ya watu.
5Nuru hungʼaa gizani nalo giza halikuishinda.
6Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana.
7Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kupitia kwake watu wote waweze kuamini.
8Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru.
9Nuru halisi inayomwangazia kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni.
10Huyo Neno alikuwako ulimwenguni, na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua.
11Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea.
12Bali wote waliompokea, yaani wale walioliamini jina lake, aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu.
13Hawa hawakuzaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali wamezaliwa kwa mapenzi ya Mungu.
14Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.
15Yohana alishuhudia habari zake, akapaza sauti, akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.’ ”
16Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema.
17Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Musa, lakini neema na kweli zimekuja kupitia Yesu Kristo.
18Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba, ndiye ambaye amemdhihirisha.
19Huu ndio ushuhuda wa Yohana wakati viongozi wa Wayahudi waliwatuma makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu kumuuliza, “Wewe ni nani?”
20Yohana alikiri waziwazi pasipo kuficha, akasema, “Mimi si Kristo.”[#1:20 maana yake Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.]
21Wakamuuliza, “Wewe ni nani, basi? Je, wewe ni Eliya?”
Yeye akajibu, “Hapana, mimi siye.”
“Je, wewe ni yule Nabii?”
Akajibu, “Hapana.”
22Ndipo wakasema, “Basi tuambie wewe ni nani ili tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wewe wasemaje juu yako mwenyewe?”
23Akawajibu kwa maneno ya nabii Isaya, akisema, “Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Yanyoosheni mapito ya Bwana.’”[#1:23 Isa 40:3]
24Basi walikuwa wametumwa watu kutoka kwa Mafarisayo,
25wakamuuliza, “Kama wewe si Kristo, wala si Eliya na wala si yule Nabii, kwa nini basi unabatiza?”
26Yohana akawajibu, “Mimi ninabatiza kwa maji, lakini kati yenu yupo mtu msiyemjua.[#1:26 au ndani ya maji]
27Yeye anakuja baada yangu, nami sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake.”
28Mambo haya yote yalitukia huko Bethania, ngʼambo ya Yordani, mahali Yohana alipokuwa akibatiza.
29Siku iliyofuata, Yohana alimwona Yesu akimjia, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu!
30Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Mtu anakuja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.’
31Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini sababu ya kuja nikibatiza kwa maji ni ili yeye apate kufunuliwa kwa Israeli.”
32Kisha Yohana akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake.
33Mimi nisingemtambua, lakini yeye aliyenituma nibatize kwa maji alikuwa ameniambia, ‘Yule mtu utakayemwona Roho akimshukia na kukaa juu yake, huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’
34Mimi mwenyewe nimeona jambo hili na ninashuhudia kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu.”
35Siku iliyofuata, Yohana alikuwa huko tena pamoja na wanafunzi wake wawili.
36Alipomwona Yesu akipita, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu!”
37Wale wanafunzi wawili walipomsikia Yohana akisema haya, wakamfuata Yesu.
38Yesu akageuka, akawaona wakimfuata, akawauliza, “Mnataka nini?”
Wakamwambia, “Rabi” (maana yake “Mwalimu”), “unaishi wapi?”
39Yesu akawajibu, “Njooni, nanyi mtapaona!”
Hivyo wakaenda na kupaona mahali alipokuwa anaishi, wakakaa naye siku ile, kwa kuwa ilikuwa yapata saa kumi.
40Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliosikia yale Yohana alisema na kumfuata Yesu.
41Kitu cha kwanza Andrea alichofanya ni kumtafuta Simoni nduguye na kumwambia, “Tumemwona Masiya” (yaani Kristo).
42Naye akamleta kwa Yesu.
Yesu akamwangalia na kusema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana. Utaitwa Kefa” (ambalo limetafsiriwa Petro).
43Siku iliyofuata Yesu aliamua kwenda Galilaya. Akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.”
44Filipo alikuwa raia wa Bethsaida, mji walikotoka Andrea na Petro.
45Filipo naye akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona yeye ambaye Musa aliandika habari zake katika Sheria, na ambaye pia manabii waliandika kumhusu, yaani Yesu wa Nazareti, mwana wa Yusufu.”
46Nathanaeli akauliza, “Nazareti! Je, kitu chochote chema chaweza kutoka Nazareti?”
Filipo akamwambia, “Njoo uone.”
47Yesu alipomwona Nathanaeli anakaribia, akanena habari zake, akasema, “Tazama huyu ni Mwisraeli kweli kweli; hana hila ndani yake.”
48Nathanaeli akamuuliza, “Umenifahamuje?”
Yesu akamjibu, “Nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini, kabla hata Filipo hajakuita.”
49Nathanaeli akamwambia, “Rabi, wewe ni Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli!”
50Yesu akamwambia, “Unaamini kwa kuwa nilikuambia nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini? Basi utaona mambo makuu kuliko hilo.”
51Ndipo akawaambia, “Amin, amin nawaambia, ninyi mtaona mbingu ikifunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”