Yoeli 2

Yoeli 2

Jeshi la nzige

1Pigeni tarumbeta katika Sayuni;

pigeni mbiu katika mlima wangu mtakatifu.

Wote wanaoishi katika nchi na watetemeke,

kwa kuwa siku ya Bwana inakuja. Iko karibu,

2siku ya giza na huzuni,

siku ya mawingu na utusitusi.

Kama mapambazuko yanavyosambaa

toka upande huu wa milima

hata upande mwingine,

jeshi kubwa na lenye nguvu linakuja.

Jambo kama hili halijakuwepo tangu zamani,

wala halitakuwepo tena kamwe

kwa vizazi vijavyo.

3Mbele yao moto unateketeza,

nyuma yao miali ya moto

inawaka kwa nguvu.

Mbele yao nchi iko kama bustani ya Edeni,

nyuma yao ni jangwa lisilofaa:

hakuna kitu kinachowaepuka.

4Wanaonekana kama farasi;

wanaenda mbio

kama askari wapanda farasi.

5Wanatoa sauti kama magari ya vita,

wanaporukaruka juu ya vilele vya milima,

kama mlio wa miali ya moto ilayo mabua,

kama jeshi kubwa lililojipanga kwa ajili ya vita.

6Wanapoonekana, mataifa yanakuwa katika maumivu makuu;

kila uso unabadilika rangi.

7Wanashambulia kama mashujaa;

wanapanda kuta kama askari.

Wote wanatembea katika safu,

hawapotoshi safu zao.

8Hakuna anayemsukuma mwenzake;

kila mmoja anaenda mbele moja kwa moja.

Wanapita katika vizuizi

bila kuharibu safu zao.

9Wanaenda kasi kuingia mjini;

wanakimbia ukutani.

Wanaingia ndani ya nyumba;

kwa kuingilia madirishani kama wezi.

10Mbele yao dunia inatikisika,

anga linatetemeka,

jua na mwezi vinatiwa giza,

na nyota hazitoi mwanga wake tena.

11Bwana anatoa mshindo wa ngurumo

mbele ya jeshi lake;

majeshi yake hayana idadi,

ni wenye nguvu nyingi

wale ambao hutii agizo lake.

Siku ya Bwana ni kuu,

ni ya kutisha.

Ni nani anayeweza kuistahimili?

Rarueni mioyo yenu

12“Hata sasa,” asema Bwana ,

“nirudieni kwa mioyo yenu yote,

kwa kufunga, kwa kulia na kuomboleza.”

13Rarueni mioyo yenu

na siyo mavazi yenu.

Mrudieni Bwana Mungu wenu,

kwa maana yeye ndiye mwenye neema

na mwingi wa huruma,

si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo,

huona huruma, hujizuia kuleta maafa.

14Ni nani ajuaye? Yeye aweza kugeuka na kuwa na huruma

na kuacha baraka nyuma yake:

sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji

kwa ajili ya Bwana Mungu wenu.

15Pigeni tarumbeta katika Sayuni,

tangazeni saumu takatifu,

liiteni kusanyiko takatifu.

16Wakusanyeni watu,

wekeni wakfu kusanyiko;

waleteni pamoja wazee,

wakusanyeni watoto,

wale wanyonyao maziwa.

Bwana arusi na atoke chumbani mwake

na bibi arusi naye atoke katika chumba chake.

17Makuhani, ambao wanahudumu mbele za Bwana ,

na walie katikati ya ukumbi

wa Hekalu na madhabahu.

Waseme, “Wahurumie watu wako, Ee Bwana .

Usifanye urithi wako kitu cha kudharauliwa,

neno la dhihaka kati ya mataifa.

Kwa nini wasemezane miongoni mwao,

‘Yuko wapi Mungu wao?’ ”

Jibu la Bwana

18Kisha Bwana atakuwa na wivu kwa ajili ya nchi yake

na kuwa na huruma juu ya watu wake.

19Bwana atawajibu:

“Ninawapelekea nafaka,

mvinyo mpya na mafuta,

vya kuwatosha ninyi

hadi mridhike kabisa;

kamwe sitawafanya tena

kitu cha kudharauliwa na mataifa.

20“Nitafukuza jeshi la kaskazini likae mbali nanyi,

nikilisukuma ndani ya jangwa,

askari wa safu za mbele wakienda

ndani ya bahari ya mashariki

na wale wa safu za nyuma

katika bahari ya magharibi.

Uvundo wake utapaa juu;

harufu yake itapanda juu.”

Hakika ametenda mambo makubwa.

21Usiogope, ee nchi;

furahi na kushangilia.

Hakika Bwana ametenda mambo makubwa.

22Msiogope, enyi wanyama pori,

kwa kuwa mbuga za malisho yenu

zinarudia ubichi.

Miti nayo inazaa matunda,

mtini na mzabibu inatoa utajiri wake.

23Furahini, enyi watu wa Sayuni,

shangilieni katika Bwana Mungu wenu,

kwa kuwa amewapa mvua za vuli

kwa kipimo cha haki.

Anawapelekea mvua nyingi,

mvua ya vuli na ya masika, kama mwanzoni.

24Sakafu za kupuria zitajaa nafaka,

mapipa yatafurika mvinyo mpya na mafuta.

25“Nitawalipa kwa ajili ya miaka ile iliyoliwa na nzige:

parare, madumadu na tunutu,

jeshi langu kubwa ambalo

nililituma kati yenu.

26Mtakuwa na wingi wa vyakula hadi mshibe,

na mtalisifu jina la Bwana Mungu wenu,

ambaye amefanya maajabu kwa ajili yenu;

kamwe watu wangu hawataaibishwa tena.

27Ndipo mtajua kuwa mimi niko katika Israeli,

kuwa mimi ndimi Bwana Mungu wenu,

na kwamba hakuna mwingine;

kamwe watu wangu hawataaibika tena.

Siku ya Bwana

28“Hata itakuwa, baada ya hayo,

nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili.

Wana wenu wa kiume na wa kike watatabiri,

wazee wenu wataota ndoto,

na vijana wenu wataona maono.

29Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake,

katika siku zile nitamimina Roho wangu.

30Nami nitaonesha maajabu katika mbingu

na duniani:

damu, moto na mawimbi ya moshi.

31Jua litageuzwa kuwa giza

na mwezi kuwa mwekundu kama damu,

kabla ya kuja siku ya Bwana

ile kuu na ya kutisha.

32Na kila mtu atakayeliitia

jina la Bwana ataokolewa.

Kwa maana juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu

kutakuwa na wokovu,

kama Bwana alivyosema,

miongoni mwa walionusurika

ambao Bwana awaita.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.