Yoshua 4

Yoshua 4

Ukumbusho wa kuvuka Yordani

1Taifa lote lilipokwisha kuvuka Mto Yordani, Bwana akamwambia Yoshua,

2“Chagua watu kumi na wawili miongoni mwa watu, kila kabila mtu mmoja,

3uwaambie wachukue mawe kumi na mbili katikati ya Mto Yordani, pale makuhani waliposimama, wayachukue na kuyaweka mahali mtakapokaa usiku huu.”

4Basi Yoshua akawaita watu kumi na wawili ambao alikuwa amewachagua miongoni mwa Waisraeli, mtu mmoja kutoka kila kabila,

5naye akawaambia, “Mtangulie mbele ya Sanduku la Bwana Mungu wenu, mwende katikati ya Mto Yordani. Kila mmoja wenu atainua jiwe begani mwake, kulingana na idadi ya makabila ya Israeli,

6kuwa ishara miongoni mwenu. Siku zijazo, watoto wenu watakapowauliza, ‘Ni nini maana ya mawe haya?’

7waambieni kwamba maji ya Mto Yordani yaliyokuwa yakitiririka, yalitindika mbele ya Sanduku la Agano la Bwana . Sanduku lilipovuka Yordani, maji ya Yordani yalitindika. Mawe haya yatakuwa kumbukumbu kwa watu wa Israeli milele.”

8Hivyo Waisraeli wakafanya kama Yoshua alivyowaagiza. Wakachukua mawe kumi na mbili kutoka katikati ya Mto Yordani, kulingana na idadi ya makabila ya Israeli, kama Bwana alivyomwambia Yoshua, nao wakayabeba hadi kambini mwao, mahali walipoyatua chini.

9Yoshua akayasimamisha yale mawe kumi na mbili yaliyokuwa katikati ya Mto Yordani, mahali miguu ya makuhani waliobeba Sanduku la Agano iliposimama. Nayo yako huko hadi leo.

10Makuhani waliobeba lile Sanduku walibakia wakiwa wamesimama katikati ya Mto Yordani hadi kila kitu Bwana alichomwamuru Yoshua kilipokuwa kimekamilishwa na watu, sawasawa na vile Musa alivyokuwa amemwamuru Yoshua. Watu wakafanya haraka kuvuka,

11na mara tu watu wote walipokwisha kuvuka, Sanduku la Bwana na makuhani wakavuka watu wakiwa wanatazama.

12Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakavuka mbele ya Waisraeli, wakiwa wamejiandaa kwa vita, kama Musa alivyowaamuru.

13Idadi ya wanaume elfu arobaini waliojiandaa kwa vita walivuka mbele za Bwana hadi nchi tambarare za Yeriko kwa ajili ya vita.

14Siku ile Bwana akamtukuza Yoshua mbele ya Israeli yote, nao wakamheshimu siku zote za maisha yake, kama vile walivyomheshimu Musa.

15Basi Bwana akamwambia Yoshua,

16“Waamuru hao makuhani wanaolibeba Sanduku la Ushuhuda wapande kutoka ndani ya Mto Yordani.”

17Kwa hiyo Yoshua akawaamuru hao makuhani akisema, “Pandeni kutoka ndani ya Mto Yordani.”

18Nao makuhani wakapanda kutoka ndani ya Mto Yordani wakilibeba hilo Sanduku la Agano la Bwana . Mara tu walipoiweka miguu yao ukingoni mwa mto, maji ya Yordani yakarudi kufurika kama ilivyokuwa kabla.

19Siku ya kumi ya mwezi wa kwanza watu walipanda kutoka Yordani na kupiga kambi huko Gilgali, kwenye mpaka wa mashariki wa Yeriko.

20Naye Yoshua akayasimamisha huko Gilgali yale mawe kumi na mbili waliyokuwa wameyachukua katikati ya Mto Yordani.

21Akawaambia Waisraeli, “Wazao wenu watakapowauliza baba zao siku zijazo wakisema, ‘Mawe haya maana yake ni nini?’

22Basi waambieni, ‘Israeli ilivukia mahali pakavu katika Mto Yordani.’

23Kwa maana Bwana Mungu wenu alikausha maji ya Yordani mbele yenu, hadi mlipomaliza kuvuka. Bwana Mungu wenu alifanya haya kwa Mto Yordani sawasawa na kile alichoifanyia Bahari ya Shamu alipoikausha mbele yetu hadi tulipomaliza kuvuka.

24Alifanya hivi ili mataifa yote ya dunia yapate kujua kuwa mkono wa Bwana ni wenye nguvu, na ili kila wakati mpate kumcha Bwana Mungu wenu.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.