The chat will start when you send the first message.
1Katika siku za mwisho
mlima wa Hekalu la Bwana utaimarishwa
kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote;
utainuliwa juu ya vilima,
na watu wa mataifa watamiminika humo.
2Mataifa mengi yatakuja na kusema,
“Njooni, twendeni kwenye mlima wa Bwana ,
kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo.
Atatufundisha njia zake,
ili tuweze kuenenda katika mapito yake.”
Sheria itatoka Sayuni,
neno la Bwana litatoka Yerusalemu.
3Atahukumu kati ya mataifa mengi,
na ataamua migogoro ya mataifa
yenye nguvu na yaliyo mbali.
Watafua panga zao ziwe majembe,
na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi.
Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine,
wala hawatajifunza vita tena.
4Kila mtu ataketi chini ya mzabibu wake
na chini ya mtini wake,
wala hakuna mtu atakayewaogopesha,
kwa kuwa Bwana wa majeshi amesema.
5Mataifa yote yanaweza kutembea
katika jina la miungu yao;
sisi tutatembea katika jina la Bwana
Mungu wetu milele na milele.
6“Katika siku hiyo,” asema Bwana ,
“nitawakusanya walemavu;
nitawakusanya walio uhamishoni
na wale niliowahuzunisha.
7Nitawafanya walemavu kuwa mabaki,
wale waliofukuzwa kuwa taifa lenye nguvu.
Bwana atawatawala katika Mlima Sayuni
kuanzia siku hiyo na hata milele.
8Lakini kwako wewe, ee mnara wa ulinzi wa kundi,
ee ngome ya Binti Sayuni,
milki ya awali itarudishwa kwako,
ufalme utakuja kwa Binti Yerusalemu.”
9Kwa nini sasa unalia kwa nguvu:
kwani huna mfalme?
Je, mshauri wako amekufa, hata maumivu yakukamate
kama ya mwanamke
aliye na uchungu wa kuzaa?
10Gaagaa kwa uchungu, ee Binti Sayuni,
kama mwanamke mwenye uchungu wa kuzaa,
kwa kuwa sasa ni lazima uuache mji
ukapige kambi uwanjani.
Utaenda Babeli;
huko utaokolewa.
Huko Bwana atakukomboa
kutoka mikononi mwa adui zako.
11Lakini sasa mataifa mengi
yamekusanyika dhidi yako.
Wanasema, “Mwache anajisiwe,
macho yetu na yatazame Sayuni kwa furaha!”
12Lakini hawayajui
mawazo ya Bwana ;
hawauelewi mpango wake,
yeye awakusanyaye kama miganda
kwenye sakafu ya kupuria.
13“Inuka upure, ee Binti Sayuni,
kwa kuwa nitakupa pembe za chuma;
nitakupa kwato za shaba
na utavunja vipande vipande mataifa mengi.”
Utatoa mapato yao waliopata kwa udanganyifu kwa Bwana ,
utajiri wao kwa Bwana wa dunia yote.