Zaburi 16

Zaburi 16

Zaburi 16

Sala ya matumaini

1Ee Mungu, uniweke salama,

kwa maana kwako nimekimbilia.

2Nilimwambia Bwana , “Wewe ndiwe Bwana wangu;

pasipo wewe sina jambo jema.”

3Kuhusu watakatifu walio duniani,

hao ndio wenye fahari,

na ninapendezwa nao.

4Huzuni itaongezeka kwa wale

wanaokimbilia miungu mingine.

Sitazimimina sadaka za damu kwa miungu kama hiyo,

au kutaja majina yao mdomoni mwangu.

5Bwana umeniwekea fungu langu na kikombe changu;

umeyafanya mambo yangu yote yawe salama.

6Alama za mipaka zimeniangukia mahali pazuri,

hakika nimepata urithi mzuri.

7Nitamsifu Bwana ambaye hunishauri,

hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha.

8Nimemweka Bwana mbele yangu daima.

Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume,

sitatikisika.

9Kwa hiyo moyo wangu unafurahia,

na ulimi wangu unashangilia;

mwili wangu nao

utapumzika salama,

10kwa maana hutaniacha Kuzimu,[#16:10 Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol , yaani Shimo lisilo na mwisho.]

wala hutamwacha Mtakatifu Wako

kuona uharibifu.

11Umenijulisha njia ya uzima;

utanijaza na furaha mbele zako,

pamoja na furaha ya milele

katika mkono wako wa kuume.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.