The chat will start when you send the first message.
1Mbingu zinatangaza utukufu wa Mungu,
anga zahubiri kazi ya mikono yake.
2Siku baada ya siku zinatoa habari,
usiku baada ya usiku zinatangaza maarifa.
3Hakuna msemo wala lugha,
ambapo sauti zao hazisikiki.
4Sauti yao imeenea duniani pote,
nayo maneno yao yameenea
hadi miisho ya ulimwengu.
Katika mbingu amepiga hema kwa ajili ya jua,
5linafanana na bwana arusi
akitoka chumbani mwake,
kama shujaa anavyofurahia
kukamilisha kushindana kwake.
6Huchomoza upande mmoja wa mbingu,
na kufanya mzunguko wake
hadi upande mwingine.
Hakuna kilichojificha joto lake.
7Sheria ya Bwana ni kamilifu,
ikihuisha nafsi.
Shuhuda za Bwana ni za kuaminika,
zikimpa mjinga hekima.
8Maagizo ya Bwana ni kamili,
nayo hufurahisha moyo.
Amri za Bwana huangaza,
zatia nuru machoni.
9Kumcha Bwana ni utakatifu,
nako kwadumu milele.
Amri za Bwana ni za hakika,
nazo zina haki.
10Ni za thamani kuliko dhahabu,
kuliko dhahabu iliyo safi sana,
ni tamu kuliko asali,
kuliko asali kutoka sega.
11Kwa hizo mtumishi wako anaonywa,
katika kuzishika kuna thawabu kubwa.
12Ni nani awezaye kutambua makosa yake?
Nisamehe makosa yangu nisiyoyajua.
13Mlinde mtumishi wako na dhambi za makusudi,
nazo zisinitawale.
Ndipo nitakapokuwa sina lawama,
niwe huru na hatia kubwa.
14Maneno ya kinywa changu
na mawazo ya moyo wangu,
yapate kibali mbele zako, Ee Bwana ,
Mwamba wangu na Mkombozi wangu.