The chat will start when you send the first message.
1Bwana ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana,
katika mji wa Mungu wetu,
mlima wake mtakatifu.
2Ni mzuri katika kuinuka juu kwake,
furaha ya dunia yote.
Kama vilele vya juu vya Safoni ni Mlima Sayuni,
mji wa Mfalme Mkuu.
3Mungu yuko katika ngome zake;
amejionesha mwenyewe kuwa ngome yake.
4Wafalme walipounganisha nguvu,
waliposonga mbele pamoja,
5walimwona, wakashangaa,
wakakimbia kwa hofu.
6Kutetemeka kuliwashika huko,
maumivu kama ya mwanamke
mwenye uchungu wa kuzaa.
7Uliwaangamiza kama meli za Tarshishi
zilizovunjwa na upepo wa mashariki.
8Kama tulivyokuwa tumesikia,
ndivyo tulivyoona
katika mji wa Bwana wa majeshi,
katika mji wa Mungu wetu:
Mungu ataufanya uwe salama milele.
9Ee Mungu, hekaluni mwako
tunatafakari upendo wako usiokoma.
10Ee Mungu, kama jina lako lilivyo,
sifa zako zinafika hadi miisho ya dunia,
mkono wako wa kuume umejazwa na haki.
11Mlima Sayuni unashangilia,
vijiji vya Yuda vinafurahi
kwa sababu ya hukumu zako.
12Tembeeni katika Sayuni,
uzungukeni mji,
hesabuni minara yake;
13yatafakarini vyema maboma yake,
angalieni ngome zake,
ili mpate kusimulia habari zake
kwa kizazi kijacho.
14Kwa kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu milele na milele;
atakuwa kiongozi wetu hata mwisho.