The chat will start when you send the first message.
1Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,
kwa maana nafsi yangu inakukimbilia.
Chini ya uvuli wa mabawa yako nitakimbilia
hadi maafa yapite.
2Namlilia Mungu Aliye Juu Sana,
Mungu anayetimiza makusudi yake kwangu.
3Hutumana msaada kutoka mbinguni na kuniokoa,
akiwakemea wale wanaonifuatilia vikali;
Mungu huutuma upendo wake na uaminifu wake.
4Niko katikati ya simba;
nimelala katikati ya wanyama wenye njaa kali,
watu ambao meno yao ni mikuki na mishale,
ambao ndimi zao ni panga kali.
5Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,
utukufu wako na uenee duniani kote.
6Waliitegea miguu yangu nyavu,
nikachoshwa na dhiki.
Wamechimba shimo katika njia yangu,
lakini wametumbukia humo wao wenyewe.
7Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti,
moyo wangu ni thabiti;
nitaimba na kusifu kwa nyimbo.
8Amka, nafsi yangu!
Amka, kinubi na zeze!
Nitayaamsha mapambazuko.
9Nitakusifu wewe, Ee Bwana, kati ya mataifa;
nitaimba habari zako, kati ya jamaa za watu.
10Kwa maana upendo wako ni mkuu, waenea hadi mbinguni,
uaminifu wako unazifikia anga.
11Ee Mungu, utukuzwe juu mbinguni,
utukufu wako na uwe duniani pote.