The chat will start when you send the first message.
1Ee Mungu, uniokoe na adui zangu,
unilinde kutokana na hao wanaoinuka dhidi yangu.
2Uniponye na watu watendao maovu,
uniokoe kutokana na wanaomwaga damu.
3Tazama wanavyonivizia!
Watu wakali wananifanyia hila,
ingawa Ee Bwana , mimi sijakosea
wala kutenda dhambi.
4Sijatenda kosa; hata hivyo wako tayari kunishambulia.
Inuka unisaidie, uone hali yangu mbaya!
5Ee Mungu, Bwana wa majeshi,
uliye Mungu wa Israeli,
zinduka uyaadhibu mataifa yote;
usioneshe huruma kwa wasaliti waovu.
6Hurudi wakati wa jioni,
wakibweka kama mbwa,
wakiuzurura mji.
7Tazama yale wanayotema kutoka vinywa vyao,
hutema panga kutoka midomo yao,
nao husema, “Ni nani atakayetusikia?”
8Lakini wewe, Bwana , uwacheke;
unayadharau mataifa hayo yote.
9Ee nguvu yangu, ninakutazama wewe,
wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,
10Mungu wangu unayenipenda.
Mungu atanitangulia,
naye atanifanya niwachekelee
wale wanaonisingizia.
11Lakini usiwaue, Ee Bwana, ngao yetu,
au sivyo watu wangu watasahau.
Katika uwezo wako wafanye watangetange
na uwashushe chini.
12Kwa ajili ya dhambi za vinywa vyao,
kwa ajili ya maneno ya midomo yao,
waache wanaswe katika kiburi chao.
Kwa ajili ya laana na uongo wanaotamka,
13wateketeze katika ghadhabu,
wateketeze hadi wasiwepo tena.
Ndipo itakapofahamika katika miisho ya dunia
kwamba Mungu anatawala katika Yakobo.
14Hurudi jioni,
wakibweka kama mbwa,
wakiuzurura mji.
15Wanatangatanga wakitafuta chakula,
wasipotosheka hubweka kama mbwa.
16Lakini mimi nitaziimba nguvu zako,
asubuhi nitaimba kuhusu upendo wako;
kwa maana wewe ndiwe ngome yangu
na kimbilio langu wakati wa shida.
17Ee uliye Nguvu zangu, ninakuimbia sifa.
Wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,
Mungu unayenipenda.