The chat will start when you send the first message.
1Ee Mungu, umetukataa na kutokea ghafula juu yetu,
umekuwa na hasira; sasa turejeshe!
2Umetetemesha nchi na kuipasua;
uiponye mavunjiko yake, kwa maana inatetemeka.
3Umewaonesha watu wako nyakati za kukata tamaa;
umetunywesha mvinyo unaotuyumbisha.
4Kwa wale wanaokucha wewe,
umewainulia bendera,
ili iweze kutwekwa dhidi ya upinde.
5Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume,
ili wale uwapendao wapate kuokolewa.
6Mungu amenena kutoka patakatifu pake:
“Nitaigawa Shekemu kwa ushindi
na kulipima Bonde la Sukothi.
7Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu;
Efraimu ni chapeo yangu,
nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala.
8Moabu ni sinia langu la kunawia,
juu ya Edomu natupa kiatu changu;
nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.”
9Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome?
Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu?
10Ee Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi,
na hutoki tena na majeshi yetu?
11Tuletee msaada dhidi ya adui,
kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu.
12Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi,
naye atawaponda adui zetu.