Zaburi 62

Zaburi 62

Zaburi 62

Mungu kimbilio la pekee

1Nafsi yangu inapata pumziko kwa Mungu peke yake;

wokovu wangu watoka kwake.

2Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu;

yeye ni ngome yangu, sitatikisika kamwe.

3Mtanishambulia hadi lini?

Je, ninyi nyote mtanitupa chini:

Mimi niliye kama ukuta ulioinama,

kama uzio unaotikisika?

4Walikusudia kikamilifu kumwangusha

toka mahali pake pa fahari;

wanafurahia uongo.

Kwa vinywa vyao hubariki,

lakini ndani ya mioyo yao hulaani.

5Ee nafsi yangu, upumzike, kwa Mungu peke yake,

tumaini langu latoka kwake.

6Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu;

ndiye ngome yangu, sitatikisika.

7Wokovu wangu na heshima yangu viko kwa Mungu,

ndiye mwamba wangu wenye nguvu

na kimbilio langu.

8Enyi watu, mtumainini yeye wakati wote,

miminieni mioyo yenu kwake,

kwa kuwa Mungu ni kimbilio letu.

9Binadamu wa ngazi ya chini ni pumzi tu,

nao wa ngazi ya juu ni uongo tu;

wakipimwa kwenye mizani, si chochote;

wote kwa pamoja ni pumzi tu.

10Usitumainie udhalimu,

wala ujivune kwa vitu vya wizi;

ingawa utajiri wako utaongezeka,

usiuweke moyoni mwako.

11Jambo moja Mungu amelisema,

mambo mawili nimeyasikia:

kwamba, Ee Mungu,

wewe una nguvu,

12na kwamba, Ee Bwana,

wewe ni mwenye upendo.

Hakika utampa kila mtu thawabu

kwa kadiri ya alivyotenda.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.