The chat will start when you send the first message.
1Ndugu zangu, shauku ya moyo wangu na maombi yangu kwa Mungu ni kwa ajili ya Waisraeli, kwamba waokolewe.
2Kwa maana ninaweza nikashuhudia wazi kwamba wao wana juhudi kubwa kwa ajili ya Mungu, lakini juhudi yao haina maarifa.
3Kwa kuwa hawakuijua haki ya Mungu, wakatafuta kuweka haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.
4Kwa maana Kristo ni ukomo wa sheria ili kila mtu aaminiye ahesabiwe haki.
5Musa anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.”[#10:5 Law 18:5]
6Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’” (yaani ili kumleta Kristo chini)[#10:6 Kum 30:12]
7“au ‘Ni nani atashuka kwenda Kuzimu?’” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu).[#10:7 Kuzimu hapa kwa Kiyunani ni Abyss , yaani mahali pa wafu.; #10:7 Kum 30:13]
8Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani lile neno la imani tunalolihubiri.[#10:8 Kum 30:14]
9Kwa sababu, ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka.
10Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu.
11Kama Maandiko yanavyosema, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.”[#10:11 Isa 28:16]
12Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na mtu wa Mataifa, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao.
13Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”[#10:13 Yoe 2:32]
14Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria?
15Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri Habari Njema!”[#10:15 Isa 52:7]
16Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?”[#10:16 Isa 53:1]
17Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.
18Lakini nauliza: Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana:
“Sauti yao imeenea duniani pote,
nayo maneno yao yameenea
hadi miisho ya ulimwengu.”
19Nami nauliza tena: Je, Waisraeli hawakuelewa? Kwanza, Musa asema,
“Nitawafanya mwe na wivu
kwa watu wale ambao si taifa.
Nitawakasirisha kwa taifa
lile lisilo na ufahamu.”
20Naye Isaya kwa ujasiri mwingi anasema,
“Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta.
Nilijifunua kwa watu
wale ambao hawakunitafuta.”
21Lakini kuhusu Israeli anasema,
“Mchana kutwa nimewanyooshea
watu wakaidi na wasiotii mikono yangu.”