Zekaria 1

Zekaria 1

Wito wa kumrudia Bwana

1Katika mwezi wa nane wa mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Bwana lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia, mwana wa Ido, kusema:

2“Bwana aliwakasirikia sana baba zako wa zamani.

3Kwa hiyo waambie watu: Hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi: ‘Nirudieni mimi,’ asema Bwana wa majeshi, ‘nami nitawarudia ninyi,’ asema Bwana wa majeshi.

4Msiwe kama baba zenu, ambao manabii waliotangulia waliwatangazia: Hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi: ‘Geukeni, mziache njia zenu mbaya na matendo yenu maovu.’ Lakini hawakunisikiliza wala kufuata maelekezo yangu, asema Bwana .

5Wako wapi baba zako sasa? Nao manabii, je, wanaishi milele?

6Je, maneno yangu na amri zangu nilizowaagiza manabii watumishi wangu, hayakuwapata baba zenu?

“Kisha walitubu na kusema, ‘Bwana wa majeshi ametutenda sawasawa na njia zetu na matendo yetu yalivyostahili, kama alivyokusudia kufanya.’ ”

Maono ya kwanza: Mtu katikati ya miti ya mihadasi

7Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Bwana lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia mwana wa Ido.

8Wakati wa usiku nilipata maono, na tazama, mbele yangu palikuwa na mtu akiendesha farasi mwekundu! Alikuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi kwenye bonde. Nyuma yake walikuwepo farasi wekundu, wa kikahawia, na weupe.

9Nikauliza, “Hivi ni vitu gani bwana wangu?”

Malaika aliyekuwa akizungumza na mimi akanijibu, “Nitakuonesha kuwa ni nini.”

10Kisha yule mtu aliyesimama katikati ya miti ya mihadasi akaeleza, “Ni wale ambao Bwana amewatuma waende duniani kote.”

11Nao wakatoa taarifa kwa yule malaika wa Bwana , aliyekuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi, “Tumepita duniani kote na kukuta ulimwengu wote umepumzika kwa amani.”

12Kisha malaika wa Bwana akasema, “Bwana wa majeshi, utazuia hadi lini rehema kutoka Yerusalemu na miji ya Yuda, ambayo umeikasirikia kwa miaka hii sabini?”

13Kwa hiyo Bwana akazungumza maneno ya upole na ya kufariji kwa malaika aliyezungumza nami.

14Kisha malaika yule aliyekuwa akizungumza nami akasema, “Tangaza neno hili: Hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi: ‘Nina wivu sana kwa ajili ya Yerusalemu na Sayuni,

15lakini nimeyakasirikia sana mataifa yanayojisikia kuwa yako salama. Nilikuwa nimewakasirikia Israeli kidogo tu, lakini mataifa hayo yaliwazidishia maafa.’

16“Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo Bwana : ‘Nitairudia Yerusalemu kwa rehema na huko nyumba yangu itajengwa tena. Nayo kamba ya kupimia itanyooshwa juu ya Yerusalemu,’ asema Bwana wa majeshi.

17“Endelea kutangaza zaidi kwamba: Hivi ndivyo asemavyo Bwana wa majeshi: ‘Miji yangu itafurika tena ustawi na Bwana atamfariji tena Sayuni na kumchagua Yerusalemu.’ ”

Maono ya pili: Pembe nne na mafundi wanne

18Kisha nikatazama juu, na pale mbele yangu nikaona pembe nne!

19Nikamuuliza yule malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Ni nini hizi?”

Akanijibu, “Hizi ni zile pembe zilizowatawanya Yuda, Israeli na Yerusalemu.”

20Kisha Bwana akanionesha mafundi wanne.

21Nikauliza, “Hawa wanakuja kufanya nini?”

Akanijibu, “Hizi ndizo pembe zilizowatawanya Yuda ili asiwepo atakayeweza kuinua kichwa chake, lakini mafundi wamekuja kuzitia hofu na kuzitupa chini hizi pembe za mataifa ambayo yaliinua pembe zao dhidi ya nchi ya Yuda na kuwatawanya watu wake.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.