2 Wafalme 1

2 Wafalme 1

Eliya amshutumu Ahazia

1Ikawa, baada ya kufa kwake Ahabu, Moabu wakawaasi Israeli.[#2 Sam 8:2; 2 Fal 3:5]

2Na Ahazia akaanguka kutoka dirisha la chumba chake ghorofani, katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia, Nendeni mkaulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kama nitapona ugonjwa huu.[#1 Sam 5:10]

3Lakini malaika wa BWANA akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni?[#Isa 8:19; Yer 2:10-13; Yon 2:8]

4Basi sasa, BWANA asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka.[#Mit 11:19; Mhu 8:13; Isa 3:11; Rum 6:23; Yak 1:15]

5Wale wajumbe wakarudi, na mfalme akawaambia, Mbona mmerudi?

6Wakamwambia, Mtu alitokea, akaonana nasi, akatuambia, Nendeni, rudini kwa mfalme yule aliyewatuma, mkamwambie, BWANA asema hivi Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi kwa ajili ya hayo hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa.[#Mit 14:32]

7Akawaambia, Je! Mtu yule aliyetokea, akaonana nanyi, akawaambia maneno hayo, alikuwa mtu wa namna gani?

8Wakamwambia, Alikuwa amevaa vazi la manyoya, tena amejifunga shuka ya ngozi kiunoni mwake. Naye akasema, Ndiye yule Eliya Mtishbi.[#Zek 13:4; Mt 3:4]

9Ndipo mfalme akatuma kamanda wa askari hamsini pamoja na hamsini wake, wamwendee Eliya. Akamwendea, na tazama, ameketi juu ya kilima. Akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka.[#2 Fal 6:13,14; Zab 105:15; Amo 7:12; Mt 27:29]

10Eliya akajibu, akamwambia yule kamanda wa hamsini, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto ukashuka, ukamteketeza, yeye na hamsini wake.[#Hes 11:1; Lk 9:54]

11Akatuma tena kiongozi wa hamsini mwingine pamoja na hamsini wake, wamwendee. Akajibu, akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka upesi.[#Isa 26:11]

12Eliya akajibu, akamwambia, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza, yeye na hamsini wake.

13Tena akatuma kamanda wa hamsini wa tatu, pamoja na hamsini wake. Yule kamanda wa hamsini wa tatu akapanda, akaenda akapiga magoti mbele ya Eliya, akamsihi sana, akamwambia, Ee mtu wa Mungu, nakusihi, roho yangu, na roho za watumishi wako hawa hamsini, ziwe na thamani machoni pako.[#Mit 27:22; Mhu 9:3; Isa 1:5; Yer 5:3; 1 Sam 26:21; Zab 72:14]

14Tazama, moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawateketeza wale kamanda wa hamsini wawili wa kwanza pamoja na hamsini wao; laiti sasa roho yangu na iwe na thamani machoni pako.

15Malaika wa BWANA akamwambia Eliya, Shuka pamoja naye; usimwogope. Akaondoka, akashuka pamoja naye hadi kwa mfalme.[#Isa 51:12; Yer 1:17; Eze 2:6]

16Akamwambia, BWANA asema hivi, Kwa kuwa umetuma wajumbe waulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, je! Ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli, uulize neno lake? Kwa hiyo hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa.

Kifo cha Ahazia

17Basi akafa, sawasawa na neno la BWANA alilolinena Eliya. Na Yoramu alianza kutawala mahali pake katika mwaka wa pili wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda; kwa kuwa yeye hakuwa na mwana.[#1:17 Au, Yehoramu; au, Yoramu nduguye.]

18Na mambo yote yaliyosalia aliyoyafanya Ahazia, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli?

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania