Waamuzi 20

Waamuzi 20

Kuvamiwa kwa Benyamini

1Ndipo wana wa Israeli walipotoka; na mkutano ukakutanika kama mtu mmoja, kutoka Dani hadi Beer-sheba, pamoja na nchi ya Gileadi wakamkusanyika mbele za BWANA huko Mispa.[#Kum 13:12; Yos 22:12; Amu 21:5; 1 Sam 11:7; 3:20; Amu 10:17; 11:11]

2Wakuu wote wa makabila yote ya Israeli, wakahudhuria huo mkutano wa watu wa Mungu, wanaume elfu mia nne waendao kwa miguu, walio na silaha.[#Amu 8:10; 2 Sam 24:9; 2 Fal 3:26]

3Basi wana wa Benyamini walipata habari ya kuwa wana wa Israeli wamekwea kwenda Mispa. Wana wa Israeli wakasema, Tuambieni huo uovu ulitendekaje?

4Huyo Mlawi, huyo mume wa mwanamke aliyeuawa, akajibu na kusema, Mimi nilifika Gibea ulio wa Benyamini mimi na suria wangu, ili tulale.[#Amu 19:15]

5Nao wanaume wa Gibea wakaniondokea, na kuizingira hiyo nyumba pande zote juu yangu wakati wa usiku; walitaka kuniua, na suria wangu wakambaka nguvu, hata akafa.[#Amu 19:22-26]

6Basi nikamtwaa huyo suria wangu, na kumkata vipande, na kumpeleka katika nchi yote ya urithi wa Israeli; kwa sababu wametenda maovu makuu na upumbavu katika Israeli.[#Amu 19:29; Mwa 34:7; Yos 7:15]

7Angalieni, ninyi wana wa Israeli nyote, sasa toeni maneno na mashauri yenu.[#Kut 19:5,6; Yos 9:14; Amu 19:30; Mit 13:10]

8Basi watu hao wote waliinuka sawia, wakisema, Hatutakwenda, hata mmoja, hemani kwake, wala hatutaondoka, hata mmoja, kwenda nyumbani kwake.

9Lakini jambo tutakalowatenda watu wa Gibea ni hili; tutakwea kuushambulia kwa kupiga kura;

10nasi tutatwaa watu kumi katika mia moja katika kabila zote za Israeli, na watu mia moja katika elfu, na watu elfu katika elfu kumi, ili waende kuwatwalia watu vyakula, ili hapo watakapofika Gibea ya Benyamini wapate kutenda mfano wa upumbavu huo wote walioutenda wao katika Israeli.

11Basi wanaume wote wa Israeli walikutana pamoja juu ya mji huo, walikuwa wanashikamana pamoja kama mtu mmoja.

12Kisha makabila ya Israeli wakatuma watu waende katika kabila yote ya Benyamini, wakasema, Je! Ni uovu gani huu uliokuwa kati yenu?[#Kum 13:14; Yos 22:13,16; Mt 18:15-18; Rum 12:18]

13Basi sasa watoeni watu hao, hao mabaradhuli walio katika Gibea, ili tuwaue, na kuuondoa uovu katika Israeli. Lakini wana wa Benyamini hawakukubali kuisikia sauti ya ndugu zao wana wa Israeli.[#Kum 13:13; Amu 19:22; 1 Sam 30:22; 2 Sam 20:1; 23:6; 1 Fal 21:13; 2 Nya 13:7; 2 Kor 6:15; Kum 13:5; 17:12; 1 Kor 5:13; 2 Nya 25:16; Rum 1:32]

14Lakini wana wa Benyamini wakakutanika huko Gibea kutoka katika miji yao, ili watoke kwenda kupigana na wana wa Israeli.

15Hao wana wa Benyamini walihesabiwa siku ile kutoka hiyo miji, wanaume elfu ishirini na sita waliokuwa na silaha, mbali na hao waliokaa Gibea, ambao walihesabiwa watu wateule mia saba.

16Katika watu hao wote walikuwako wanaume mia saba waliochaguliwa, wenye shoto; kila mmoja alikuwa anaweza kuutupia unywele mawe kwa kombeo, wala asikose.[#Amu 3:15; 1 Nya 12:2]

17Nao watu wa Israeli, mbali na hao wa Benyamini, walihesabiwa kuwa ni wanaume elfu mia nne, wenye silaha; hao wote walikuwa ni watu wa vita.

18Basi wana wa Israeli wakainuka, wakakwea kwenda Betheli, nao wakataka shauri kwa Mungu; wakasema, Ni nani atakayekwea kwenda vitani kwanza kwa ajili yetu juu ya wana wa Benyamini? BWANA akawaambia, Yuda atakwea kwanza.[#Kut 28:30; Hes 27:21; Yos 9:14; Amu 1:1; 1 Sam 23:9; Ezr 8:21]

19Basi wana wa Israeli waliondoka asubuhi, wakapanga hema zao ili kuvamia Gibea.

20Watu wa Israeli waliondoka ili wapigane na Benyamini; nao watu wa Israeli wakaviandaa vita juu yao huko Gibea.

21Wana wa Benyamini wakatoka Gibea, wakawaua watu elfu ishirini na mbili katika Israeli siku hiyo.[#Mwa 49:27; Kum 23:9; Mhu 9:1,11]

22Lakini watu hao, watu wa Israeli, walijitia nguvu, wakaviandaa vile vita mara ya pili mahali pale walipojiandaa siku ya kwanza.

23Wana wa Israeli wakakwea juu na kulia mbele za BWANA hadi jioni; wakamwuliza BWANA, wakisema, Je! Niende nikaribie tena kupiga vita juu ya wana wa Benyamini ndugu yangu? BWANA akasema, Haya, kweeni, mwende kupigana naye.[#Zab 78:34-36; Hos 5:15]

24Basi wana wa Israeli wakakaribia juu ya wana wa Benyamini siku ya pili.

25Benyamini alitoka kupigana nao kutoka Gibea siku ya pili, wakawaua watu elfu kumi na nane tena katika watu wa Israeli; hao wote walikuwa wenye kutumia upanga.[#Ayu 9:12; Zab 66:18; 97:2; Hos 10:9; Mik 3:4; Yn 9:31]

26Ndipo wana wa Israeli wote, na hao watu wote, wakakwea, wakaenda Betheli, na kulia, wakaketi hapo mbele za BWANA, wakafunga siku hiyo hadi jioni; nao wakasongeza sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za BWANA.

27Kisha wana wa Israeli wakauliza kwa BWANA (kwa sababu sanduku la Agano la Mungu lilikuwako huko siku hizo,[#Ayu 22:27; Zab 50:15; 91:15; Mit 3:6; Yos 18:1; 1 Sam 4:3,4; Zab 78:60,61; Yer 7:12]

28na Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, alikuwa anasimama mbele ya hilo sanduku siku hizo), wakasema, Je! Nitoke tena niende kupigana na wana wa Benyamini ndugu yangu, au niache? BWANA akawaambia, Haya, kweeni; kwa kuwa kesho nitamtoa na kumtia mkononi mwako.[#Kut 6:25; Hes 25:7,11; 31:6; Yos 22:13; 24:33; Zab 106:30,31; Kum 10:8; 18:5]

29Basi Israeli akaweka watu wavizie kinyume cha Gibea kuuzunguka pande zote.[#Yos 8:4; 2 Sam 5:23]

30Basi wana wa Israeli wakakwea kwenda kupigana na wana wa Benyamini siku ya tatu, wakajipanga ili kupigana na Gibea, kama walivyofanya hapo awali.

31Nao wana wa Benyamini wakatoka waende kupigana nao, wakavutwa waende mbali na huo mji; kisha wakaanza kuwapiga na kuwaua Waisraeli wapatao thelathini, kama walivyofanya hapo awali, kwa kuwaua katika hizo njia kuu, zielekeazo Betheli, na Gibea, na katika nchi tambarare.

32Wana wa Benyamini wakasema, Wamepigwa mbele yetu kama kwanza. Lakini wana wa Israeli wakasema, Haya, na tukimbie, na kuwavuta wauache mji waende katika njia kuu.

33Basi hao watu wote wa Israeli wakaondoka mahali pao wakajipanga huko Baal-tamari; na hao wenye kuvizia wa Israeli wakatoka mahali hapo walipokuwa, hata Maare-geba.

34Kisha watu elfu kumi waliochaguliwa katika Israeli wote wakavamia Gibea, na vile vita vilikuwa vikali sana; lakini Benyamini hawakujua ya kuwa maafa yalikuwa karibu nao.[#Yos 8:14; Ayu 21:13; Mit 4:19; 29:6; Mhu 8:11; Isa 3:10,11; 47:11; Mt 24:44; Lk 21:34; 1 The 5:3]

35BWANA akampiga Benyamini mbele ya Israeli; na wana wa Israeli waliangamiza wanaume elfu ishirini na tano na mia moja, wa Benyamini siku hiyo; wote hao waliokuwa wenye kutumia upanga.

36Basi wana wa Benyamini waliona kuwa wamepigwa.[#Yos 8:15]

Watu wa Israeli wakaondoka mbele ya Benyamini, kwa sababu walikuwa wanawatumaini hao wenye kuvizia waliokuwa wamewaweka kinyume cha Gibea.

37Hao wenye kuvizia wakafanya haraka, wakaurukia Gibea; na kuushambulia mji wote kwa makali ya upanga.[#Yos 8:19]

38Basi hiyo ishara iliyoaganwa kati ya watu wa Israeli na hao wenye kuvizia ilikuwa ni hii, kwamba wafanye lipande wingu kubwa la moshi kutoka katika huo mji.

39Nao watu wa Israeli walipogeuka katika ile vita, Benyamini naye akaanza kupiga na kuwaua watu wa Israeli kama watu thelathini; kwani walisema, Hakika yetu wamepigwa mbele yetu, vile vile kama katika ile vita ya kwanza.

40Lakini hapo hilo wingu lilipoanza kupanda kutoka katika mji, kama nguzo ya moshi, ndipo Wabenyamini wakaangalia nyuma, na tazama, moshi ulikuwa umetanda mji mzima kwenda mbinguni.[#Yos 8:20]

41Ndipo watu wa Israeli wakageuka, na watu wa Benyamini walishtushwa; kwa kuwa waliona ya kwamba wamefikiwa na maafa.[#Kut 15:9,10; Mit 5:22; Isa 33:14; Lk 17:27,28]

42Kwa hiyo wakageuza maungo yao mbele ya wana wa Israeli kuelekea njia ya kwenda nyikani; lakini ile vita ikawaandamia kwa kasi; na hao waliotoka katika ile miji wakawaangamiza katikati yake.

43Waliwazingira Wabenyamini pande zote na kuwafukuza, na kuwakanyagakanyaga hapo walipopumzika, hadi upande wa mashariki mwa Gibea.[#Hos 9:9; 10:9]

44Wakauawa Wabenyamini elfu kumi na nane, hao wote walikuwa ni wapiganaji hodari.

45Kisha wakageuka na kukimbilia upande wa nyika hadi katika jabali la Rimoni; nao wakaokota katika watu hao katika njia kuu wanaume elfu tano; wakawaandamia kwa kasi mpaka Gidomu, nako wakawaua wengine wao watu elfu mbili.[#Yos 15:32]

46Basi jumla ya watu wa Benyamini waliouawa siku ile walikuwa ni watu elfu ishirini na tano waliokuwa wapiganaji vita; wote hao walikuwa ni mashujaa.

47Lakini wanaume mia sita wakageuka, wakakimbilia upande wa nyika hadi katika jabali la Rimoni, wakakaa kwenye hilo jabali la Rimoni muda wa miezi minne.[#Amu 21:13; Isa 1:9; Yer 14:9,10; Omb 3:32; Hab 3:2]

48Kisha watu wa Israeli wakageuka tena kuwaendea wana wa Benyamini, wakawapiga kwa makali ya upanga, huo mji mzima, na hao wanyama wa mji, na kila kitu walichokiona; tena miji yote waliyoiona wakaiteketeza kwa moto.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania