The chat will start when you send the first message.
1Maneno hayo nimewaambia, msije mkakwazwa.[#Yn 14:29]
2Watawatenga na masinagogi; naam, saa inakuja kila mtu awauaye atakapodhania ya kuwa anamfanyia Mungu ibada.[#Yn 9:22; Mt 5:11; 24:9; Lk 6:22]
3Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi.[#Yn 15:21]
4Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi niliwaambia.[#Lk 22:53; Yn 17:12]
Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nilikuwapo pamoja nanyi.
5Lakini sasa mimi naenda zangu kwake yeye aliyenituma, wala hakuna mmoja wenu aniulizaye, Unakwenda wapi?[#Yn 7:33]
6Ila kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu.
7Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitamtuma kwenu.[#Yn 14:16,26]
8Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.[#1 Kor 14:24; Ebr 4:12]
9Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi;[#Yn 3:18; Rum 1:18]
10kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena;[#Mdo 5:31; Rum 4:25]
11kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.[#Yn 12:31; 14:30]
12Hata bado ningali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamuwezi kuyastahimili hivi sasa.[#1 Kor 3:1]
13Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.[#Yn 14:26; 1 Yoh 2:27]
14Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.
15Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nilisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari.[#Yn 17:10]
16Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni; na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona.[#Yn 14:19]
17Basi baadhi ya wanafunzi wake wakasemezana, Neno gani hilo asemalo, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? Na hilo, Kwa sababu naenda zangu kwa Baba?
18Basi walisema, Neno gani hilo asemalo; hilo, Bado kitambo kidogo? Hatujui asemalo.
19Yesu alifahamu ya kwamba wanataka kumwuliza, akawaambia, Ndilo hilo mnaloulizana, ya kuwa nilisema, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona?
20Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.
21Mwanamke azaapo, ana huzuni kwa kuwa saa yake imefika; lakini akiisha kuzaa mwana, haikumbuki tena ile dhiki, kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtu ulimwenguni.[#Isa 26:17]
22Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye.[#Isa 66:14]
23Tena siku ile hamtaniuliza neno lolote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lolote atawapa kwa jina langu.[#Yn 14:13,14,20; 1 Yoh 5:14; Mt 7:7; Mk 11:24]
24Hata sasa hamjaomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.[#Yn 15:11]
25Hayo nimesema nanyi kwa mithali; saa inakuja ambapo sitasema nanyi tena kwa mithali, lakini nitawapa waziwazi habari ya Baba.[#Yn 10:6]
26Na siku ile mtaomba kwa jina langu, wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba;
27kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nilitoka kwa Baba.[#Yn 14:21]
28Nilitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba.
29Basi wanafunzi wake wakasema, Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yoyote.[#Yn 16:25]
30Sasa tumejua ya kuwa wewe wafahamu mambo yote, wala huna haja ya mtu akuulize; kwa hiyo twasadiki ya kwamba ulitoka kwa Mungu.[#Yn 2:25]
31Yesu akawajibu, Je! Mnasadiki sasa?
32Tazama, saa inakuja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; lakini mimi siko peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami.[#Zek 13:7; Mt 26:31,45; Mk 14:27,50; Yn 8:29]
33Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.[#Yn 14:27; Rum 5:1; 1 Yoh 5:4]