Mathayo 22

Mathayo 22

Mfano wa Karamu ya harusi

1Yesu akajibu, akawaambia tena kwa mifano, akisema,

2Ufalme wa mbinguni unafanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe harusi.[#Lk 14:16-24; #Yn 3:29]

3Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja harusini; nao wakakataa kuja.

4Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng'ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni harusini.[#Mt 21:36]

5Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake;

6nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawadhulumu na kuwaua.

7Basi yule mfalme akaghadhibika; akatuma majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao.[#Mt 24:2]

8Kisha akawaambia watumwa wake, Harusi iko tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili.

9Basi Nendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni harusini.[#Mt 13:47; 21:43]

10Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; harusi ikajaa wageni.

11Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la harusi.

12Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la harusi? Naye akatekewa.

13Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.[#Mt 8:12; 25:30; Lk 13:28]

14Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.

Swali juu ya kulipa kodi

15Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno.[#Mk 12:13-17; Lk 20:20-26; #Yn 8:6]

16Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, tunajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu.[#Mk 3:6; Yn 3:2]

17Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo?

18Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki?

19Nionesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari.

20Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii?

21Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu.[#Rum 13:7]

22Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao.[#Yn 8:9]

Swali kuhusu ufufuo

23Siku ile Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza,[#Mk 12:18-27; Lk 20:27-40; #Mdo 23:8]

24wakisema, Mwalimu, Musa alisema, Mtu akifa, akiwa hana watoto, ndugu yake na amwoe yule mkewe, ili ampatie nduguye mzao.[#Kum 25:5,6; Mwa 38:8]

25Basi, kwetu kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akaoa, akafariki, na kwa kuwa hana mzao, akamwachia nduguye mke wake.

26Vivyo hivyo wa pili naye, na wa tatu, hata wote saba.

27Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye.

28Basi, katika kiyama, atakuwa mke wa yupi kati ya wale saba? Maana wote walikuwa naye.

29Yesu akajibu, akawaambia, Mnapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.

30Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni.

31Tena kuhusu kiyama ya wafu, hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu, akisema,

32Mimi ni Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai.[#Kut 3:6; Mt 8:11]

33Na makutano waliposikia, walishangaa kwa mafunzo yake.

Amri iliyo kuu zaidi

34Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja.[#Mk 12:28-31; Lk 10:25-28]

35Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza, akimjaribu;[#Lk 10:25-28]

36Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu?

37Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.[#Kum 6:5]

38Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.

39Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako.[#Law 19:18]

40Katika amri hizi mbili hutegemea Torati yote na vitabu vya Manabii.[#Mt 7:12; Rum 13:10; Gal 5:14]

Swali kuhusu Mwana wa Daudi

41Na Mafarisayo walipokusanyika, Yesu aliwauliza, akisema, Mnaonaje kuhusu Kristo?[#Mk 12:35-37; Lk 20:41-44]

42Ni mwana wa nani? Wakamwambia, Ni wa Daudi.[#Yn 7:42]

43Akawauliza, Imekuwaje basi Daudi katika Roho kumwita Bwana, akisema,

44Bwana alimwambia Bwana wangu,[#Zab 110:1; Mt 26:64]

Uketi katika mkono wangu wa kulia,

Hata niwawekapo adui zako

Kuwa chini ya miguu yako?

45Basi, Daudi akimwita Bwana, amekuwaje ni mwanawe?

46Wala hakuweza mtu kumjibu neno; wala hakuthubutu mtu yeyote tangu siku ile kumwuliza neno tena.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania