Yudithi 4

Yudithi 4

Waisraeli wanajihami

1Watu wa Yuda walisikia jinsi Holoferne, kamanda wa majeshi ya mfalme Nebukadneza wa Waashuru, alivyoyatenda mataifa mengine. Walisikia jinsi alivyoteka na kuyabomolea mbali mahekalu yao.

2Hivyo, wakashikwa na woga, wakihofia itakuwaje kwa mji wa Yerusalemu na hekalu la Bwana Mungu wao.

3Wakati huu, walikuwa ndio wamerudi nyumbani Yuda kutoka uhamishoni. Walikuwa wametoka kulitakasa hekalu, vifaa vyake pamoja na madhabahu yaliyokuwa yametiwa unajisi.

4Hivyo, wakapeleka onyo kwenye eneo la Samaria, miji ya Kona, Beth-horoni, Belmaini, Yeriko, Koba, Esora, na bonde la Salemu.

5Walizishika upesi sehemu za milimani, wakajenga ngome milimani na kuhifadhi chakula tayari kwa vita. Walikuwa na bahati nzuri, kwani walikuwa wametoka kuvuna mashamba yao.

6Kuhani mkuu Yoakimu, aliyekuwa mjini Yerusalemu wakati huo, akawaandikia watu walioishi katika miji ya Bethulia na Betomesthaimu, karibu na Esdreloni penye tambarare karibu na mji wa Dothaimu.

7Akawaagiza wazishike njia zote za milimani zinazoelekea nchini Yuda. Wakiwa huko ingalikuwa rahisi kwao kuzuia shambulio lolote, kwani njia hizo hazikuruhusu watu wengi kupita, ila watu wawili tu kwa wakati mmoja.

8Waisraeli wakazitekeleza amri walizopewa na kuhani mkuu Yoakimu pamoja na baraza la wazee lililokutana mjini Yerusalemu.

Sala kabla ya vita

9Wanaume wote Waisraeli wakamlilia Mungu, wakijinyenyekeza mbele zake na kufunga.

10Wao, wake zao, watoto wao, mifugo yao, kila mgeni miongoni mwao, kibarua na mtumwa aliyenunuliwa, wote wakavaa mavazi ya gunia.[#Taz Yona 3:7-8; Esta 4:1-3]

11Wanaume wote walioishi mjini Yerusalemu, wanawake wote pamoja na watoto, wakasujudu mbele ya hekalu wakiwa wamejipaka majivu kichwani na kutandaza mavazi yao ya gunia mbele za Bwana.

12Wakiwa wamevaa mavazi ya gunia waliizunguka madhabahu wakimwomba Mungu wa Israeli kwa moyo wote ili asiruhusu watoto wao watekwe, wake zao kuchukuliwa mateka na miji yao kuangamizwa. Wakamsihi Mungu asiwaruhusu watu wa mataifa kutekeleza nia yao ya kuliangamiza hekalu na hivyo kulitia unajisi.

13Bwana akazisikia sala zao na kuyaona mateso yao. Alifanya hivyo kwa sababu watu wa Yuda na Yerusalemu waliendelea kufunga wakiwa mbele ya hekalu la Mwenyezi-Mungu kwa muda wa siku nyingi.[#Taz Esta 4:16]

14Kuhani mkuu Yoakimu, makuhani pamoja na wahudumu wote wa hekalu la Mungu wakiwa wamejifunga mavazi ya gunia viunoni, wakatoa tambiko za kuteketezwa kila siku, matoleo ya hiari ya watu na tambiko zilizoletwa ili kutekeleza nadhiri.[#Taz Yoe 2:17]

15Wakatia majivu kwenye mavazi yao kumlilia Bwana, wakimwomba alihurumie taifa zima la Israeli.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania