Zaburi 139

Zaburi 139

Mungu ajua yote, aongoza yote

1Ee Mwenyezi-Mungu, wewe umenichunguza;

wewe wanijua mpaka ndani.

2Nikiketi au nikisimama, wewe wajua;

wajua kutoka mbali kila kitu ninachofikiria.

3Watambua nikienda au nikipumzika;

wewe wazijua shughuli zangu zote.

4Kabla sijasema neno lolote,

wewe, ee Mwenyezi-Mungu, walijua kabisa.

5Uko kila upande wangu, mbele na nyuma;

waniwekea mkono wako kunilinda.

6Maarifa yako yapita akili yangu;

ni makuu mno, siwezi kuyaelewa.

7Nikimbilie wapi ambako roho yako haiko?

Niende wapi ambako wewe huko?

8Nikipanda juu mbinguni, wewe upo;

nikijilaza chini kuzimu, wewe upo.

9Nikiruka hadi mawio ya jua,

au hata mipakani mwa bahari,

10hata huko upo kuniongoza;

mkono wako wa kulia utanitegemeza.

11Kama ningeliomba giza linifunike,

giza linizunguke badala ya mwanga,

12kwako giza si giza hata kidogo,

na usiku wangaa kama mchana;

kwako giza na mwanga ni mamoja.

13Wewe umeniumba, mwili wangu wote;

ulinitengeneza tumboni mwa mama yangu.

14Nakusifu maana nimefanywa kwa namna ya ajabu,

matendo yako ni ya ajabu;

wewe wanijua kabisakabisa.

15Umbo langu halikufichika kwako

nilipotungwa kwa siri na ustadi ndani ya dunia.

16Wewe uliniona hata kabla sijazaliwa,

uliandika kila kitu kitabuni mwako;

siku zangu zote ulizipanga,

hata kabla ya kuweko ile ya kwanza.

17Ee Mungu, mawazo yako ni makuu mno;

hayawezi kabisa kuhesabika.

18Ningeyahesabu yangekuwa mengi kuliko mchanga.

Niamkapo, bado nipo pamoja nawe.

19Laiti, ee Mungu, ungewaua watu waovu!

Laiti watu wauaji wangeondoka kwangu!

20Wanasema vibaya juu yako;

wanasema maovu juu ya jina lako!

21Ee Mwenyezi-Mungu, nawachukia wanaokuchukia;

nawadharau sana wale wanaokuasi!

22Maadui zako ni maadui zangu;

ninawachukia kabisakabisa.

23Unichunguze, ee Mungu, unijue moyo wangu,

unipime, uyajue mawazo yangu.

24Uangalie kama mwenendo wangu ni mbaya,

uniongoze katika njia ya milele.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania