Esteri 6

Esteri 6

Hamani hana budi kumheshimu Mordekai.

1Usiku ule mfalme hakupata usingizi, akaagiza, wamletee hicho kitabu cha mambo ya siku yapasayo kukumbukwa. Ikawa, yaliposomwa masikioni pa mfalme,

2zikaoneka zile habari zilizoandikwa za kwamba: Mordekai ameumbua watumishi wa nyumbani mwa mfalme, Bigitana na Teresi, waliokuwa walinda mlango, waliotafuta njia ya kumwua mfalme Ahaswerosi kwa mikono yao.[#Est. 2:21-23.]

3Mfalme akauliza: Mordekai amepata tunzo gani au ukuu gani kwa tendo hilo? Vijana wa mfalme waliomtumikia wakajibu: Hakuna alichofanyiziwa.

4Mfalme akauliza tena: Uani yuko nani? Naye Hamani alikuwa ameingia katika ua wa nje wa nyumba ya mfalme, aje kumwambia mfalme, wamtundike Mordekai katika ule mti, aliomsimikia.[#Est. 5:14.]

5Vijana wa mfalme walipomwambia: Tazama, ni Hamani anayesimama uani, mfalme akasema: Aje!

6Hamani alipokuja, mfalme akamwuliza: Mfalme akipendezwa kumheshimu mtu, atafanyiziwa nini huyo mtu? Hamani akawaza moyoni mwake kwamba: Yuko nani, mfalme apendezwaye naye, amheshimu, nisipokuwa mimi?

7Kwa hiyo Hamani akamwambia mfalme: Kama yuko mtu, mfalme apendezwaye naye, amheshimu,

8na walete nguo ya kifalme, mfalme aliyoivaa, na farasi, mfalme aliyempanda, aliyevikwa kichwani pake kilemba cha kifalme!

9Kisha mkuu mmoja wa mfalme mwenye macheo apewe hiyo nguo na huyo farasi, wamvike huyo mtu, mfalme apendezwaye naye, amheshimu, kisha wampandishe huyo farasi uwanjani mwa mji na kupiga mbiu mbele yake kwamba: Hivi ndivyo, mtu anavyofanyiziwa, mfalme akipendezwa naye, amheshimu.

10Ndipo, mfalme alipomwambia Hamani: Nenda upesi sasa hivi kuichukua hiyo nguo na huyo farasi, kama ulivyosema, umfanyizie vivyo hivyo Myuda Mordekai akaaye langoni kwa mfalme! Lakini usisahau hata neno moja katika hayo, uliyoyasema!

11Basi, Hamani akaichukua hiyo nguo na huyo farasi, akamvika Mordekai, kisha akampandisha uwanjani mwa mji, akapiga mbiu mbele yake kwamba: Hivi ndivyo, mtu anavyofanyiziwa, mfalme akipendezwa naye, amheshimu.

12Kisha Mordekai akarudi langoni pake kwa mfalme, lakini Hamani akaikimbilia nyumba yake kwa kusikitika, akawa amejifunika kichwa.

13Hamani akamsimulia mkewe na wapenzi wake yote yaliyomtukia. Rafiki zake waliokuwa werevu wa kweli na mkewe Zeresi wakamwambia: Kama huyu Mordekai, uliyeanza kumwangukia, ni wa kizazi cha Wayuda, hutamshinda, ila utaendelea kumwangukia.

14Walipokuwa wangali wakisema naye, wakafika watumishi wa nyumbani wa mfalme, wakamhimiza Hamani, aje upesi kula karamu, Esteri aliyoifanya.[#Est. 5:8.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania