Esteri 8

Esteri 8

Mordekai anapata macheo.

1Siku hiyo mfalme Ahaswerosi akampa Esteri, mkewe mfalme, nyumba ya Hamani, aliyekuwa mpingani wao Wayuda. Mordekai akaja kwa mfalme, kwani Esteri alimsimulia mfalme, udugu wao ulivyo.

2Ndipo, mfalme alipoondoa kidoleni pete yake yenye muhuri, aliyomvua Hamani, akampa Mordekai. Naye Esteri akamkalisha Mordekai katika nyumba ya Hamani.[#Est. 3:10.]

3Esteri akaendelea kusema mbele ya mfalme, akamwangukia miguuni na kulia machozi na kumlalamikia, autangue ule ubaya wa Hamani wa Agagi nayo mashauri yake, aliyowatakia Wayuda.

4Mfalme alipompungia Esteri kwa bakora yake ya dhahabu, Esteri akainuka, asimame mbele ya mfalme,[#Est. 5:2.]

5akasema: Vikiwa vema kwake mfalme, nami nikiwa nimeona upendeleo mbele yake, nalo neno hili likifaa mbele yake mfalme, mimi nikiwa mwema machoni pake, basi, na ziandikwe barua za kuzitangua zile barua zenya lile shauri baya la Hamani, mwana wa Hamedata wa Agagi, alizoziandika za kuwaangamiza Wayuda wote walioko katika majimbo yote ya mfalme.

6Kwani nitawezaje kuyatazama hayo mabaya yatakayowapata wenzangu wa ukoo? Tena nitawezaje kuutazama mwangamizo wa ukoo wangu?

7Ndipo, mfalme Ahaswerosi alipomwambia Esteri, mkewe mfalme, na Myuda Mordekai: Tazameni, nyumba ya Hamani nimempa Esteri, naye mwenyewe wamemtundika katika ule mti, kwa kuwa aliunyosha mkono wake, awaue Wayuda.

8Basi, ninyi andikeni barua kwa Wayuda katika jina la mfalme, kama mnavyoona kuwa vema, kisha zitieni zile barua muhuri kwa hiyo pete ya mfalme! Kwani barua iliyoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme haitanguki.

Agizo jipya la mfalme la kuwaponya Wayuda.

9Wakaitwa waandishi wa mfalme wakati huo wa mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani, siku ya ishirini na tatu, yote Mordekai aliyoyaagiza yakaandikwa baruani kwa Wayuda na kwa wenye amri na kwa watawala nchi na kwa wakuu wa majimbo kuanzia nchi ya Uhindi kuifikisha hata nchi ya Nubi, majimbo yote ni 127; yakaandikwa kwa kila jimbo katika maandiko ya kwao na kwa kila kabila katika msemo wa kwao, hata kwa Wayuda katika maandiko ya kwao na katika msemo wa kwao.[#Est. 1:22.]

10Naye akaziandika hizo barua katika jina la mfalme Ahaswerosi, akazitia muhuri kwa ile pete ya mfalme yenye muhuri, kisha akawapa wapiga mbio waliopanda farasi, wazipeleke; nao hao farasi waliowapanda walikuwa wa wakuu, walizaliwa katika makundi yaliyochaguliwa.

11Yaliyoandikwa ni haya: Mfalme amewapa ruhusa Wayuda waliomo katika miji yote, wakusanyike katika kila mji mmoja kujisimamia wenyewe na kujiokoa, wakiwatowesha kwa kuwaua na kwa kuwaangamiza vikosi vyote vya watu wa kila kabila na wa kila jimbo watakaowashambulia, hata watoto na wanawake, kisha waziteke nazo mali zao.

12Yafanyike siku moja katika majimbo yote ya mfalme Ahaswerosi, ndio siku ya kumi na tatu katika mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari.

13Mwandiko wa pili wa hizo barua ukatangazwa katika kila jimbo moja kuwa amri iliyotolewa na mfalme, watu wote pia wakaelezwa vema, Wayuda wapate kuwa tayari siku hiyohiyo kujilipiza kwa adui zao.

14Wapiga mbio waliopanda farasi wale wepesi wa wakuu wakatoka upesi na kujihimiza kwa ajili ya lile neno la mfalme. Namo mjini mwa Susani, mlimokuwa na jumba la mfalme, ile amri ya mfalme ikatangazwa.

15Kisha Mordekai akatoka usoni pa mfalme, akawa amevaa vazi la kifalme la nguo ya kifalme nyeusinyeusi na nyeupe, napo kichwani amevaa kilemba kikubwa cha kifalme cha dhahabu, tena amevaa joho la bafta lenye nguo nyekundu za kifalme. Nao mji wa Susani ukajaa vigelegele na mashangilio.

16Hivyo ndivyo, Wayuda walivyopata machangamko na furaha na macheko na macheo.

17Katika kila jimbo na katika kila mji mmoja mahali po pote, lile neno la mfalme lilipotangazwa, pakawa na furaha na macheko kwa Wayuda, hata karamu na sikukuu, nao watu wengi wa hizo nchi wakajigeuza kuwa Wayuda, kwa kuguiwa na woga wa kuwaogopa Wayuda.[#2 Mose 15:14-16.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania