2 Mose 25

2 Mose 25

Mchango wa kulijenga Hema Takatifu.

1Bwana akamwambia Mose kwamba:

2Waambie wana wa Isiraeli, wanichangie vipaji vya tambiko, mtoze kila mtu, kama moyo wake unavyomtuma.[#2 Mose 35:5,22.]

3Navyo vipaji vya tambiko, mtakavyowatoza, ni hivi: dhahabu na fedha na shaba,

4na nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na nguo za bafta na nywele za mbuzi,

5na ngozi nyekundu za madume ya kondoo na ngozi za pomboo na migunga,

6mafuta ya taa, manukato ya kutengeneza mafuta ya kupaka na mavukizo yanukayo vizuri;

7vito vya oniki na vito vingine vya kutia katika kisibau cha mtambikaji mkuu na katika kibati chake cha kifuani.

8Wanitengenezee Patakatifu, nipate kukaa katikati yao.

9Kwa mfano, mimi nitakaokuonyesha wa hilo kao na wa vyombo vyake vyote, mvifanye vyote pia, viwe vivyo hivyo.[#2 Mose 25:40.]

Sanduku la Agano.

(10-22: 2 Mose 37:1-9.)

10Tengenezeni sanduku la mbao za migunga, urefu wake uwe mikono miwili na nusu, nao upana wake uwe mkono mmoja na nusu, nao urefu wake wa kwenda juu uwe mkono mmoja na nusu.

11Ulifunikize lote dhahabu tupu, upande wa ndani na wa nje uufunikize hivyo, kisha uzungushe juu yake taji la dhahabu.

12Tena utengeneze mapete manne kwa kuyeyusha dhahabu, uyatie penye pembe zake nne, mapete mawili upande wake mmoja, tena mapete mawili upande wake wa pili.

13Kisha utengeneze mipiko miwili ya migunga, nayo ifunikize dhahabu,

14kisha hiyo mipiko itie katika yale mapete pande zote mbili za sanduku, iwe ya kulichukulia hilo sanduku.

15Namo katika hayo mapete ya sanduku mipiko sharti ikae humo, isitoke humo.

16Namo sandukuni uuweke Ushahidi, nitakaokupa.[#2 Mose 25:21.]

Kiti cha Upozi.

17Kisha utengeneze kifuniko cha dhahabu tupu kuwa Kiti cha Upozi, urefu wake uwe mikono miwili na nusu, nao upana wake uwe mkono mmoja na nusu.[#Ebr. 4:16.]

18Kisha utengeneze Makerubi mawili ya dhahabu, nayo uyatengeneze kwa kuzifuafua hizo dhahabu, uyaweke pande zote mbili za mwisho wa kifuniko.

19Kerubi moja uweke upande wa mwisho wa huku, nalo la pili upande wa mwisho wa huko. Hivyo myaweke hayo Makerubi pande zake zote mbili za mwisho wa kifuniko.

20Nayo Mkerubi yawe yameyakunjua mabawa juu, yakifunike hicho kifuniko kwa mabaa yao, nazo nyuso zao ziwe zimeelekeana, hayo Mkerubi yakikitazama kifuniko kwa nyuso zao.

21Kisha kifuniko kiweke juu ya lile sanduku, namo sandukuni uuweke Ushahidi, nitakaokupa.[#2 Mose 34:29; 1 Fal. 8:9; Ebr. 9:4.]

22Mahali hapo ndipo, nitakapokutana na wewe, niseme na wewe nikiwa hapo juu ya hicho Kiti cha Upozi katikati ya hayo Makerubi mawili yaliyoko juu ya Sanduku la Ushahidi, nikuambie yote, nitakayokuagiza ya kuwaambia wana wa Isiraeli.

Meza ya kumwekea Bwana mikate.

(23-29: 2 Mose 37:10-16.)

23Tena tengeneza meza kwa mbao za migunga, urefu wake uwe mikono miwili, nao upana wake uwe mkono mmoja, nao urefu wake wa kwenda juu uwe mkono mmoja na nusu.

24Nayo uifunikize dhahabu tupu, kisha uzungushe juu yake taji la dhahabu.

25Kisha uzungushe kando yake kibao cha kukingia chenye upana wa shibiri, nacho hicho kikingio ukizungushie taji la dhahabu.

26Kisha itengenezee mapete manne ya dhahabu, nayo hayo mapete uyatie penye pembe zake nne zilizoko penye miguu yake minne.

27Hayo mapete sharti yawe papo hapo chini ya kikingio, wapate kutia humo mipiko ya kuichukulia hiyo meza.

28Hiyo mipiko uitengeneze nayo kwa migunga na kuifunikiza dhahabu, itumike ya kuichukulia hiyo meza.

29Hata vyano vyake na vijiko vyake na vitungi vyake na vikombe vyake vinavyotumikia vinywaji vya tambiko sharti uvitengeneze kwa dhahabu tupu.

30Napo hapo mezani sharti uweke pasipo kukoma mikate ya kuw usoni pangu.[#3 Mose 24:5.]

Kinara kikubwa.

(31-39: 2 Mose 37:17-24.)

31Tena utengeneze kinara cha dhahabu tupu! Hiki kinara na kitengenezwe kwa kufuafua dhahabu, ipate kutoka shina lake na mti wake, navyo vikombe vyake na vifundo vyake na maua yake, vyote pia viwe vimetoka katika dhahabu iyo hiyo moja.

32Matawi sita na yatoke penye mbavu zake, matawi matatu ya kinara na yatoke penye ubavu mmoja, tena matawi matatu ya kinara na yatoke penye ubavu wa pili.

33Vikombe vitatu vinavyofanana na maua ya mlozi viwe katika kila tawi moja, yaani vifundo pamoja na maua yao. Vivyo hivyo katika matawi yote sita yanayotoka katika mti wa kinara.

34Lakini katika mti wa kinara viwe vikombe vinne vinavyofanana na maua ya mlozi, yaani vifundo pamoja na maua yao.

35Tena kila mahali, matawi mawili yanapotoka katika huo mti wake, chini yake kiwe kifundo kimoja. Viwe vivyo hivyo kila mahali, matawi mawili yanapotoka. Nayo matawi yanayotoka katika kinara yawe sita.

36Vifundo na matawi yao sharti yote yawe kazi moja iliyoyatokeza yote pamoja kwa kuifuafua dhahabu iyo hiyo moja, nayo yawe dhahabu tupu.

37Kisha utengeneze taa zake saba, nazo hizo taa zake uziweke juu yake, zipaangaze mahala palipo mbele yake.

38Nazo koleo zake na makato yake yawe ya dhahabu tupu.

39Sharti ukitengeneze pamoja na hivi vyombo vyake vyote kwa kipande cha dhahabu chenye uzito wa mizigo miwili.

40Angalia, uyafanye yote kwa mfano, niliokuonyesha mlimani![#2 Mose 26:30; Tume. 7:44; Ebr. 8:5.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania