Hosea 10

Hosea 10

Pasipo wongofu hakuna wokovu.

1Isiraeli ni mzabibu uchipukao vema, uzaao matunda mema;

lakini kama matunda yake yalivyo mengi

ndivyo, walivyojitengenezea pengi pa kutambikia,

kwa wema wa nchi yako waliulinganya wema wa vinyago.

2Mioyo yao ni midanganyifu, sasa watalipishwa!

Yeye atapavunja pao pa kutambikia, aviangamize vinyago

vyao.

3Kwani sasa husema kweli kwamba: Hatuna mfalme!

Bwana hatukumcha, naye mfalme atatufanyizia nini?

4Husema maneno tu, huapa bure wakifanya maagano;

basi, nayo mapatilizo yatakua

kama mimea yenye uchungu shambani kwenye matuta.

5Wakaao Samaria huihangaikia ng'ombe ya Beti-Aweni,

kweli watu wa huko wanaiombolezea,

nao watambikaji wake wanatetemeka kwa ajili yake,

kwa ajili ya utukufu wake, kwa kuwa umeondolewa kwao.

6Nayo yenyewe itapelekwa Asuri kuwa tunzo la mfalme

Yarebu;

ndipo, soni zitakapomshika Efuraimu,

naye Isiraeli atatwezwa kwa ajili ya shauri lake.

7Mfalme wa Samaria ataangamizwa, awe kama kibanzi majini

juu.

8Navyo vilima vya Aweni vitaangamizwa, Isiraeli

alikomkosea Mungu;

miti yenye miiba na mibigili itakulia hapo pao pa

kutambikia;

ndipo, watakapoiambia milima: Tufunikeni!

nayo machuguu: Tuangukieni!

9Kuanzia zile siku za Gibea umekosa wewe Isiraeli! Huko walisimama, vita vya kuwapiga wapotovu visiwafikie huko Gibea.[#Hos. 9:9.]

10Nitawapiga, kama itakavyonipendeza; makabila mengine yatawakusanyikia, watakapofungiwa manza zao mbili, walizozikora.

11Efuraimu anafanana na ndama aliyefundishwa, apendaye kupura; nami nitautumia uzuri wa shingo yake na kumfundisha kuvuta gari; hata Yuda atalima mahali pa ng'ombe, naye Yakobo atajipondea mwenyewe madongo.

12Kwa hiyo jipandieni yatakayoleta wongofu, mpate kuvuna yenye utu! jilimieni shamba jipya, siku zingaliko bado za kumtafuta Bwana, mpaka aje na kuwafundisha yanyokayo![#Yes. 55:6; Yer. 4:3.]

13Lakini ninyi hulimia mabaya, mkavuna mapotovu, mkala mazao ya uwongo. Kwa kuwa unajishikiza kwa njia yako na kwa wingi wa watu walio na nguvu za kupiga vita,[#Iy. 4:8.]

14kwa hiyo makelele ya vita yatatokea kwa watu wako, nayo miji yako yote yenye maboma itaangamizwa, kama Salmani alivyouangamiza Beti-Arbeli siku, walipopigana, ni hapo wamama waliposetwa na kuuawa pamoja na watoto.

15Mambo kama hayo ndiyo, Beteli utakayowapatia ninyi, kwa ajili ya ubaya wenu ulio mwingi; siku moja kutakapopambazuka, mfalme wa Isiraeli atakuwa ameangamia kabisa.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania