Yesaya 34

Yesaya 34

Mapatilizo ya adui za Waisiraeli.

1Karibuni, ninyi wamizimu, msikie!

Nanyi makabila ya watu, angalieni!

Nchi na isikilize nayo yote yaliyoko!

Nao ulimwengu nayo yote yachipukako!

2Kwani Bwana amewachafukia wamizimu wote,

makali yake yawatokee vikosi vyao vyote;

akawatia mwiko, wasiwepo tena, akawatoa, wachinjwe.

3Watakaouawa kwao watatupwa tu,

mnuko wa mizoga yao utaenea,

nayo milima italegezwa kwa damu zao.

4Hata vikosi vyote vya mbinguni vitayeyuka,

nazo mbingu zitazingwa kama kizingo cha karatasi,

vikosi vyake vyote vitanyauka,

kama majani yanavyonyauka

kwenye mizabibu nako kwenye mikuyu.

Mapatilizo ya Waedomu.

5Kwani upanga wangu ukilewa mbinguni,

mtauona, unavyowashukia Waedomu;

nimewatia mwiko wa kuwapo, wapatilizwe.

6Bwana yuko na upanga uliojaa damu, ukapakwa mafuta:

ni damu za wana kondoo na za madume,

ni mafuta ya mafigo ya madume;

kwani iko sikukuu ya tambiko ya Bwana huko Bosira,

liko chinjo kubwa katika nchi ya Edomu.

7Pamoja nao hata nyati wataanguka,

nayo madume na manono ya ng'ombe,

nchi yao italewa kwa kuzinywa damu zao,

nao mchanga utapata nguvu kwa mafuta yao.

8Kwani hiyo ni siku ya Bwana ya kulipiza,

ni mwaka wa kuvilipisha vita, walivyoupelekea Sioni.

9Mito yake itageuzwa kuwa lami,

nayo mavumbi yake yatakuwa viberiti,

hivyo nchi yao itakuwa lami iwakayo moto.

10Usiku na mchana hautazima,

moshi wake utapanda kale na kale;

kwa vizazi na vizazi itakuwa jangwa,

siku zote za kale na kale hapataonekana atakayepapita.

11Watakaoitwaa ni korwa na nungu,

hata mabundi na makunguru watakaa huko;

Bwana atatanda juu yake kamba ya kuipimia, iwe peke yake,

ataweka nayo mawe ya kuipimia, iwe tupu kabisa.

12Hakuna wakuu wake watakaoiita kuwa nchi ya kifalme,

wote walioitawala watakuwa wametoweka.

13Miti yenye miiba itamea majumbani mwao,

namo mabomani viwawi na mangugi;

namo ndimo, watakaamo mbweha na mbuni.

14Huko vimburu watakutana na mbwa wa mwitu,

shetani atamwita shetani mwenziwe;

tena ndiko, mzuka wa kike wa usiku utakakotua

na kujipatia pa kupumzikia.

15Naye nyoka wa mamba atatengeneza kuko shimo lake,

atage mayai, apate watoto, awatunze kuvulini pake,

Tena ndiko, mwewe watakakokusanyikana,

kila mmoja na mwenziwe.

16Tafuteni katika kitabu cha Bwana, msome!

Hawa nyama hakuna hata mmoja wao asiyepatikana,

wote hakuna hata mmoja amkosaye mwenziwe;

kwani kinywa chake mwenyewe ndicho kilichowaagiza,

nayo Roho yake ndiyo inayowakusanya.

17Yeye ndiye aliyewapigia kura,

nao mkono wake ndio uliowagawia mafungu yao,

naye aliyapima kwa kamba ya kupimia,

wayatwae, yawe yao ya kale na kale,

wakae huko vizazi na vizazi.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania