Yeremia 42

Yeremia 42

Yeremia anawakataza Wayuda kwenda Misri.

1Wakuu wote wa vikosi na Yohana, mwana wa Karea, na Yezania, mwana wa Hosaya, nao watu wote wa ukoo huu, wadogo kwa wakubwa, wakamjia

2mfumbuaji Yeremia, wakamwambia: Malalamiko yetu na yakuangukie, utuombee kwa Bwana Mungu wako sisi sote tuliosazwa huku! Kwani tumesalia wachache tu kwa wale wengi, kama macho yako yanavyotuona sisi.[#Yer. 37:3.]

3Bwana Mungu wako atuonyeshe njia, tutakayoishika, na jambo, tutakalolifanya.

4Mfumbuaji Yeremia akawaambia: Nimesikia; sasa hivi nitawaombea kwa Bwana Mungu wenu kwa ajili ya njia yenu; kila neno, Bwana atakalowajibu, nitawaambia, sitawanyima neno kamwe.

5Nao wakamwambia Yeremia: Bwana na awe kwetu shahidi mkweli na mtegemevu kwamba: Kila neno, Bwana Mungu wako atakalokutuma, litakavyotuambia, ndivyo, tutakavyofanya.

6Kama ni jema au kama ni baya, sauti ya Bwana Mungu wetu tutaisikia, kwa kuwa tunakutuma kwake, kusudi tuone mema tukiisikia sauti ya Bwana Mungu wetu.

7Siku kumi zilipopita, neno la Bwana likamjia Yeremia,

8akamwita Yohana, mwana wa Karea, nao wakuu wote wa vikosi waliokuwa naye, nao watu wote wa ukoo huu, wadogo kwa wakubwa,

9akawaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema, kwa kuwa mmenituma kwake, kumpelekea malalamiko yenu, yamwangukie,

10akasema: Mtakapokaa tu katika nchi hii, nitawajenga, nisiwabomoe tena, nitawapanda, nisiwang'oe tena, kwani nitageuza moyo, nisiyafanye yale mabaya, niliyowawazia.

11Msimwogope mfalme wa Babeli, mnayemwogopa ninyi! Ndivyo, asemavyo Bwana: Msimwogope, kwani mimi niko pamoja nanyi, niwaokoe na kuwaponya mikononi mwake!

12Nami nitawapatia huruma, awahurumie na kuwarudisha katika nchi yenu.

13Lakini ninyi mkisema: Hatutakaa katika nchi hii, msiisikie sauti ya Bwana Mungu wenu;

14mkisema: Hivi sivyo, sharti tuende Misri, maana hatutaona huko vita, wala sauti za mabaragumu hazitasikilika huko, wala hatutaona njaa kwa kukosa chakula, kwa hiyo tunataka kukaa huko;

15basi, sasa lisikieni neno la Bwana, ninyi mlio masao ya Yuda: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Kama mnazielekeza nyuso zenu kwenda Misri, mkaja kukaa ugenini huko,

16ndipo, panga, ninyi mnazoziogopa, zitakapowafikia katika nchi ya Misri, nayo njaa inayowatisha itawafuata huko Misri na kugandamana nanyi, kwa hiyo ndiko, mtakakofia.

17Itakuwa hivyo: Watu wote waliozielekeza nyuso zao kwenda Misri, wakae ugenini huko, watauawa huko kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya; hawataona pa kuponea wala pa kuyakimbilia mabaya, mimi nitakayowaletea.[#Yer. 29:17-18.]

18Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Kama makali yangu yenye moto yalivyomwagiwa wakaao Yerusalemu, ndivyo, mtakavyomwagiwa makali yangu nanyi, mtakapokwenda Misri. Nanyi mtaapizwa kwa kustukiwa, mtazomelewa na kutukanwa, lakini mahali hapa hamtapaona tena.

19Bwana anawaambia ninyi mlio masao ya Yuda: Msiende Misri! Yajueni kabisa, ya kuwa nimewashuhudia leo!

20Msiposikia mtazipoteza roho zenu, kwani ninyi wenyewe mmenituma kwa Bwana Mungu wenu kwamba: Tuombee sisi kwa Bwana Mungu wetu! Nayo yote, Bwana Mungu wetu atakayotuambia, tutayafanya vivyo hivyo, kama atakavyotujulisha.[#Yer. 42:5.]

21Nikawajulisha leo, lakini hamwisikii sauti ya Bwana Mungu wenu na kuyafanya yote, aliyonituma kuwaambia.

22Kwa hiyo jueni sasa: Panga na njaa na magonjwa mabaya ndiyo yatakayowaua mahali hapo panapowapendeza kupaendea na kukaa ugenini kuko huko.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania