Yosua 13

Yosua 13

Mungu anamwagiza Yosua kuwagawia Waisiraeli nchi nzima ya Kanaani.

1Yosua alipokuwa mzee mwenye siku nyingi, Bwana akamwambia: Wewe umekwisha kuwa mzee mwenye siku nyingi, nazo nchi zilizosalia uchukuliwa ni nyingi bado.

2Nazo nchi zilizosalia ni hizi: majimbo yote ya Wafilisti na Gesuri nzima

3toka mto wa Sihori ulioko upande wa Misri mpaka kwenye mipaka ya Ekroni kaskazini; kwani nchi hizo huhesabiwa kuwa za Wakanaani. Nao wakuu wa Wafilisti ni hawa watano: Wa Gaza na Wa Asdodi na wa Askaloni na wa Gati na wa Ekroni.

4Tena Waawi walioko kusini, tena nchi nzima ya Wakanaani na Meara iliyo ya Wasidoni mpaka Afeki hata kwenye mipaka ya Waamori.

5Tena nchi ya Wagebali na ya Libanoni yote upande wa maawioni kwa jua toka Baali-Gadi chini ya milima ya Hermoni, mpaka ufike Hamati.

6Wote wakaao milimani toka Libanoni mpaka Misirefoti-Maimu, wale Wasidoni wote nitawafukuza wote mbele ya wana wa Isiraeli; wewe nchi hizi zigawie tu Waisiraeli na kuzipigia kura, ziwe fungu lao, kama nilivyokuagiza.[#Yos. 11:8.]

7Sasa nchi hizi zigawanyie yale mashina tisa na nusu ya Manase, ziwe mafungu yao!

8Nusu yake nyingine wamekwisha kuyachukua mafungu yao pamoja nao wa Rubeni na wa Gadi, Mose aliyowapa ng'ambo ya huko ya Yordani upande wa maawioni kwa jua; wameyachukua sawasawa, kama Mose, mtumishi wa Bwana, alivyowapa:[#Yos. 13:15-32.]

9toka Aroeri ulioko mtoni kwa Arnoni nao ule mji uliomo katikati ya mto na nchi ya tambarare yote ya Medeba mpaka Diboni.

10Nayo miji yote ya Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyetawala mle Hesiboni mpaka kwenye mipaka ya wana wa Amoni.

11Tena Gileadi nazo nchi za Gesuri na za Makati na milima yote ya Hermoni na Basani nzima mpaka Salka.

12Nchi zote za Basani zilizo za ufalme wa Ogi aliyetawala mle Astaroti na Edirei, ni yule aliyekuwa wa masao ya wale Majitu, Mose aliowapiga na kuwafukuza.

13Lakini wana wa Isiraeli hawakuwafukuza Wagesuri na Wamakati, nao Wagesuri na Wamakati wakapata kukaa katikati ya Waisiraeli hata siku hii ya leo.

14Wao na shina la Lawi tu Mose hakuwapa fungu, liwe lao, kwa maana ng'ombe za tambiko za kuchomwa motoni za Bwana Mungu wa Isiraeli ndizo zilizokuwa fungu lao, kama alivyowaambia.[#Yos. 13:33.]

Nchi za Rubeni na za Gadi na za nusu ya Manase.

15Mose aliwapa wao wa shina la Rubeni nchi ya kuzigawanyia koo zao.[#4 Mose 32.]

16Mpaka wao ulianza Aroeri ulioko kwenye kijito cha Arnoni pamoja na ule mji ulioko mtoni katikati, ukaiingia nchi yote ya tambarare karibu ya Medeba

17na Hesiboni pamoja na miji yake yote iliyoko katika nchi ya tambarare: Diboni na Bamoti-Baali na Beti-Baali-Meoni,

18na Yasa na Kedemoti na Mefati,

19na Kiriataimu na Sibuma na Sereti-Sahari ulioko juu ya mlima wa hilo bonde,

20na Beti-Peori na matelemko ya Pisiga na Beti-Yesimoti

21na miji yote ya hiyo nchi ya tambarare. Tena ufalme wote wa Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyetawala mle Hesiboni; ni yule, Mose aliyempiga pamoja na wakuu wa Wamidiani, Ewi na Rekemu na Suri na Huri na Reba, ndio wakuu wa Sihoni waliokaa katika nchi hiyo.

22Hata mwaguaji Bileamu, mwana wa Beori, wana wa Isiraeli walimwua kwa upanga pamoja na wengine waliouawa nao.[#4 Mose 22:5; 31:8.]

23Mpaka mwingine wa wana wa Rubeni ulikuwa mto wa Yordani. Huu ulikuwa mpaka wa fungu lao wana wa Rubeni la kuzigawanyia koo zao ile miji pamoja na mitaa yao.

24Nao wa shina la Gadi, wale wana wa Gadi, Mose aliwapa nchi ya kuzigawanyia koo zao.

25Mpaka wao ulikuwa huu: Yazeri na miji yote ya Gileadi na nusu ya nchi ya wana wa Amoni mpaka Aroeri unaoelekea Raba.

26Tena kutoka Hesiboni mpaka Ramati-Misipe na Betonimu, tena toka Mahanaimu kufika kwenye mpaka wa Debiri.

27Tena bondeni Beti-Haramu na Beti-Nimura na Sukoti na Safoni na kipande kilichosalia cha ufalme wa Sihoni, mfalme wa Hesiboni; hapo mto wa Yordani ulikuwa mpaka hata mwisho wa bahari ya Kinereti ng'ambo ya huko ya Yordani ya upande wa maawioni kwa jua.

28Hili ni fungu lao wana wa Gadi la kuzigawanyia koo zao.

29Nao waliokuwa nusu ya shina la Manase Mose aliwapa nchi, ikawa yao waliokuwa nusu ya wana wa Manase ya kuzigawanyia koo zao.

30Mpaka wao ulianza Mahanaimu, ukachukua Basani nzima, ndiyo nchi yote ya Ogi, mfalme wa Basani, pamoja na vijiji vyote vya Mahema ya Yairi vilivyokuwako kule Basani, pamoja ni miji 60.[#Amu. 10:3-4.]

31Tena mpaka wao ukachukua nusu ya Gileadi na Astaroti na Edirei, ile miji ya kifalme ya Ogi kule Basani. Nchi hii ilikuwa yao wana wa Makiri, mwana wa Manase, waliokuwa nusu tu ya wana wa Makiri, ya kuzigawanyia koo zao.

32Hizi ndizo nchi, Mose alizowapa, ziwe mafungu yao katika nyika za Moabu ng'ambo ya huko ya Yordani upande wa maawioni kwa jua, Yeriko ukiwa ng'ambo ya pili.

33Lakini wao wa shina la Lawi Mose hakuwapa fungu, liwe lao, kwani Bwana Mungu wa Isiraeli, yeye ni fungu lao, kama alivyowaambia.[#4 Mose 18:20-21.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania