Yosua 3

Yosua 3

Waisiraeli wanauvuka Yordani na kupita pakavu katikati ya maji.

1Yosua akaamka asubuhi na mapema, wakaondoka kule Sitimu, wakaja Yordani, yeye na wana wote wa Isiraeli, wakalala huko kabla ya kuvuka.[#4 Mose 25:1.]

2Siku tatu zilipopita, wenye amri wakazunguka makambini,

3wakawaagiza watu kwamba: Mtakapoliona Sanduku la Agano la Bwana Mungu wenu, watambikaji Walawi wakilichukua, nanyi mtaondoka mahali penu, mlifuate.

4Mtaangalia tu, hapo katikati yenu nalo hilo Sanduku pawe mahali penye urefu wa mikono elfu mbili, msilikaribie zaidi, mpate kuijua njia yenu ya kuishika, kwani hamtavuka katika njia ya siku zote.

5Kisha Yosua akawaambia watu: Jieueni! Kwani kesho Bwana atafanya vioja kwenu.[#2 Mose 19:10.]

6Kisha Yosua akawaambia watambikaji kwamba: Lichukueni Sanduku la Agano, mwatangulie watu! Ndipo, walipolichukua Sanduku la Agano, wakawatangulia watu.[#Yos. 6:6.]

7Ndipo, Bwana alipomwambia Yosua: Siku hii ya leo nitaanza kukukuza machoni pa Waisiraeli wote, kwa kuwa watajua, ya kama nitakuwa na wewe, kama nilivyokuwa na Mose.[#Yos. 1:5,17; 4:14.]

8Nawe uwaagize watambikaji wanaolichukua Sanduku la Agano kwamba: Mtakapofika ukingoni penye maji ya Yordani mtasimama.

9Yosua akawaambia wana wa Isiraeli: Fikeni karibu, myasikie maneno ya Bwana Mungu wenu!

10Kisha Yosua akawaambia: Hapo ndipo, mtakapojua, ya kuwa Mungu Mwenye usima yuko katikati yenu, atakapowafukuza kabisa mbele yenu Wakanaani na Wahiti na Wahiwi na Waperizi na Wagirgasi na Waamori na Wayebusi.

11Nanyi mtaliona sanduku la Agano la Bwana wa nchi zote, likiwatangulia kuuvuka Yordani.

12Kwa hiyo jichagulieni watu kumi na wawili katika mashina ya Waisiraeli, katika kila shina moja mtu mmoja!

13Itakuwa hapo, nyayo za miguu ya watambikaji wanaolichukua Sanduku la Agano la Bwana wa nchi zote zitakapoyagusa maji ya Yordani, ndipo, maji ya Yordai yatakapojitenga, hayo maji yanayoshuka nayo yanayotoka juu, haya yasimame kuwa kama boma moja tu.

14Watu walipoondoka mahemani kwao, wauvuke Yordani, watambikaji wakalichukua Sanduku la Agano kuwatangulia watu;

15basi, wachukuzi wa hilo Sanduku walipofika Yordani, nayo miguu yao watambikaji waliolichukua hilo Sanduku ilipojichovya ukingoni katika maji, kwani siku zote za mavuno Yordani hujaa maji mpaka juu ukingoni pande zote mbili,

16ndipo, maji yaliyotoka upande wa juu yaliposimama, yakafurika juu kuwa kama boma moja tu, yakafika mbali sana mpaka mji wa Adamu ulioko upande wa Sartani; nayo maji yaliyoshuka kuingia katika bahari ya nyikani, ile Bahari ya Chumvi, yakapwa yote pia; kwa hiyo watu wakapata kuvuka na kuuelekea mji wa Yeriko.[#2 Mose 14:21; Sh. 114:3.]

17Nao watambikaji waliolichukua Sanduku la Agano la Bwana wakasimama katikati ya mto wa Yordani na kuishikiza miguu pakavu penyewe, nao Waisiraeli wote wakapitia pakavu; vikawa hivyo, hata watu wote wakaisha kuuvuka Yordani.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania