Yosua 8

Yosua 8

Mji wa Ai unatekwa.

1Kisha Bwana akamwambia Yosua: Usiogope, wala usiingiwe na vituko! Wachukue watu wote kwenda vitani pamoja na wewe! Kisha ondoka kuupandia Ai! Tazama, nimemtia mfalme wa Ai mkononi mwako pamoja na watu wake na mji wake na nchi yake.

2Nawe uufanyizie Ai na mfalme wake, kama ulivyoufanyizia Yeriko na mfalme wake, vitu vyake tu mtakavyoviteka pamoja na nyama wao wa kufuga mtajichukulia, viwe mateka yenu. Jipatie penye kuuvizia mji upande wake wa nyuma![#Yos. 6:21.]

3Ndipo, Yosua alipoondoka pamoja na watu wote kwenda vitani kwa kuupandia Ai. Yosua akachagua watu 30000 walio mafundi wa vita wenye nguvu, akawatuma kwenda usiku

4alipokwisha kuwaagiza kwamba: Tazameni, ndivyo mwuvizie huu mji upande wa nyuma ya mji! msiupite mji kwenda mbali sana, nyote mpata kuwa tayari!

5Nami pamoja na watu wote walio kwangu tutaukaribia mji. Tena watakapotoka, watujie kama ile mara ya kwanza, tutakimbia mbele yao.

6Ndipo, watakapotoka, watufuate, mpaka tuishe kuwafungia njia ya kurudia mjini, kwani watasema: Wanatukimbia kama mara ya kwanza; nasi tunataka kweli kuwakimbia.[#Yos. 7:5.]

7Ndipo, ninyi mtakapoondoka hapo pa kuvizia, mwuteke mji, kwani Bwana Mungu wenu amaeutia mikononi mwenu.

8Hapo mtakapouteka mji, mwuteketeze kwa moto, mfanye, kama Bwana alivyosema! Yaangalieni, niliyowaagiza!

9Kisha Yosua akawatuma, nao wakaenda mahali pa kuvizia, wakakaa katikati ya Beteli na ya Ai upande wa baharini wa Ai. Naye Yosua akalala usiku huo katikati ya watu.

10Kesho yake Yosua akaamka na mapema, akawakagua watu wake, kisha akapanda yeye pamoja wa wazee wa Waisiraeli na kuwaongoza watu kwenda Ai.

11Nao wapiga vita wote waliokuwa naye wakapanda kuukaribia mji; walipofika ng'ambo ya huku ya mji wakalala upande wa kaskazini wa Ai, napo hapo katikati yao na mji wa Ai palikuwa bonde.

12Akachukua kama watu 5000, akawaweka pa kuvizia katikati ya Beteli na Ai upande wa baharini wa mji.

13Kisha wakayapanga majeshi yote ya watu waliokuwako upande wa kaskazini wa mji nao wale washambuliaji waliokuwako upande wa baharini wa mji. Kisha Yosua akaenda usiku huo kuja katikati ya bondeni.

14Mfalme wa Ai alipoviona, watu wa mji wakajidamka kwa upesi kuwaendea Waisiraeli kupigana nao, yeye na watu wake wote, mahali palepale mbele ya mbuga. Naye hakujua, ya kuwa wako wanaomvizia nyuma ya mji.

15Ndipo, Yosua na Waisiraeli wote walipojifanya kuwa kama watu waliopigwa nao, wakakimbia na kushika njia ya kwenda nyikani.

16Nao watu wale waliokuwamo mjini wakaitana kwenda kuwakimbiza, nao walipomkimbiza Yosua wakajitenga na mji wa kwao.

17Hakusalia mtu mle Ai wala Beteli asiyetoka kuwakimbiza Waisiraeli, nao mji wao wakauacha wazi wakiwakimbiza Waisiraeli.

18Ndipo, Bwana alipomwambia Yosua: Mkuki uliomo mkononi mwako, uunyoshee mji wa Ai! Kwani nitautia mkononi mwako. Yosua akaunyosha mkuki uliokuwamo mkononi mwake na kuuelekezea huo mji.

19Alipounyosha mkono wake, ndipo, wale waliouvizia walipoondoka upesi mahali pao na kupiga mbio, wakaingia katika mji, wakauteka, wakajihimiza kuuteketeza kwa moto.

20Watu wa Ai walipogeuka nyuma yao kutazama, mara wakaona, moshi wa mjini unavyopanda mbinguni juu, nao kwa kulegea mikono hawakuweza kukimbia, wala huko, wala huko; ndipo, wale watu waliokimbia nyikani walipowageukia wao waliowakimbiza.

21Yosua na Waisiraeli wote walipoona, ya kuwa waviziaji wameuteka mji, kwa kuwa moshi wa mjini ulipanda juu, nao wakarudi, wakawapiga watu wa Ai.

22Nao wale wa mjini wakatoka kuwaendea nao; ndivyo, hao walivyokuwa katikati ya Waisiraeli, hawa huku nao wale huko, wakawapiga, wasisaze hata mmoja aliyekimbia na kujiponya.

23Lakini mfalme wa Ai wakamkamata, yu hai, wakampeleka kwake Yosua.

24Nao Waisiraeli walipokwisha kuwaua mashambani na nyikani wenyeji wote wa Ai waliowakimbiza, basi, hao wote walipokwisha kuuawa kwa ukali wa panga, mpaka waishe kabisa, Waisiraeli wote wakarudi Ai, wakawaua wote waliokuwamo kwa ukali wa panga.

25Nao wote waliouawa siku hiyo, waume kwa wake, walikuwa 12000, ndio watu wote wa Ai.

26Kwani Yosua hakuurudisha mkono wake ulioshika mkuki, mpaka akiwaangamiza kabisa wenyeji wa Ai wote pia.[#2 Mose 17:11-13.]

27Ni nyama wa kufuga tu na vitu, Waisiraeli walivyoviteka humo mjini, wakajichukulia kwa lile neno la Bwana, alilomwagiza Yosua.

28Kisha Yosua akauteketeza mji wa Ai, akaugeuza kuwa chungu tupu kale na kale mpaka siku hii ya leo.

29Naye mfalme wa Ai akamtungika mtini na kumwacha huko mpaka jioni; lakini jua lilipokuchwa, Yosua akaagiza, waushushe mzoga wake mtini, wautupe pa kuliingilia lango la mji, kisha wakakusanya juu yake chungu kubwa la mawe lililoko hata siku hii ya leo.[#Yos. 10:27; 5 Mose 21:23.]

Yosua anawasomea watu wote Maonyo ya Mose.

30Kisha Yosua akajenga juu ya mlima wa Ebali pa kumtambikia Bwana.[#5 Mose 27:2-8.]

31Kama Mose, mtumishi wa Bwana, alivyowaagiza wana wa Isiraeli, kama vilivyoandikwa katika kitabu cha Maonyo ya Mose, alipajenga pale pa kutambikia kwa mawe mazima yasiyochongwa kwa chuma cha mtu, akamtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, wakachinja hata ng'ombe za tambiko za shukrani.

32Kisha akaandika hapo penye yale mawe mwandiko wa pili wa Maonyo ya Mose, aliouandika machoni pa wana wa Isiraeli.

33Nao Waisiraeli wote, wazee wao na wenye amri na waamuzi wao walikuwa wamesimama huku na huko penye lile Sanduku na kuwaelekea watambikaji Walawi waliolichukua Sanduku la Agano la Bwana, wageni pamoja na wazalia, nusu yao waliuelekea mlima wa Gerizimu, nusu waliuelekea mlima wa Ebali, kama Mose, mtumishi wa Bwana, alivyowaagiza kale kuubariki ukoo wa Waisiraeli.[#5 Mose 11:29; 27:12-13.]

34Baadaye akayasoma maneno yote ya Maonyo, ya mbaraka nayo ya kiapizo, sawasawa kama yalivyoandikwa katika kitabu cha Maonyo.

35Katika yale yote, Mose aliyoyaagiza, halikuwamo hata moja, Yosua asilolisoma masikioni pa mkutano wa Waisiraeli wote, wakiwa pamoja na wanawake na wana wa wageni waliokwenda kukaa nao.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania