Mifano 12

Mifano 12

Matendo yao werevu nayo yao wajinga.

1Apendaye kuonywa hupenda ujuzi,

lakini achukiaye kukanywa hupumbaa kama nyama.

2Mwema hujipatia upendeleo kwake Bwana,

lakini mwenye mawazo mabaya humpatiliza.

3Hakuna atakayeshupaa vema kwa kuacha kumcha Mungu,

lakini mashina ya waongofu hayatang'oleka.

4Mwanamke mwema ni kilemba cha mumewe,

lakini ampatiaye soni ni kama ugonjwa wa ubovu mifupani mwake.

5Mawazo ya waongofu huyataka yanyokayo,

lakini mashauri yao wasiomcha Mungu hutaka kudanganya tu.

6Maneno yao wasiomcha Mungu huotea damu za watu,

lakini vinywa vyao wanyokao huwaponya.

7Wasiomcha Mungu wanapofudikizwa hawako tena,

lakini nyumba za waongofu husimama.

8Mtu husifiwa, kama akili zake zilivyo,

lakini mwenye moyo mpotovu hubezwa.

9Kunyenyekea na kujitumikia mwenyewe ni kwema,

kuliko kujitukuza na kukosa vilaji.

10Mwongofu huzijua roho za nyama wake, afugao

lakini huruma zao wasiomcha Mungu ni ukali tu.

11Alilimiaye shamba lake hushiba vilaji,

lakini akimbiliaye mambo yaliyo ya bure amepotelewa na akili.

12Asiyemcha Mungu hutamani mateka ya wabaya,

lakini mashina ya waongofu huchipuka.

13Mapotovu ya midomo ni kama tanzi baya,

lakini mwongofu huponyoka akisongwa.

14Kila mtu hushiba vema mazao ya kinywa chake,

mikono ya mtu iliyoyafanya, humrudia mwenyewe.

15Njia ya mjinga hunyoka machoni pake,

lakini mwerevu wa kweli husikia shauri la mwingine.

16Mjinga hujulikana kwa kukasirika papo hapo,

lakini aerevukaye huziba masikio akitukanwa.

17Asemaye yaliyo kweli hutangaza yaongokayo,

lakini shahidi ya uwongo hudanganya.

18Wako wapuzi wachomao mioyo ya watu kama upanga,

lakini ndimi zao walio werevu wa kweli huponya.

19Midomo yenye kweli hukaa kale na kale,

lakini ndimi za uwongo hukaa kitambo kidogo tu.

20Udanganyifu umo mioyoni mwao watungao mabaya,

lakini wenye mshauri ya utengemano hufurahisha.

21Mwongofu hapatwi na mapotovu yo yote,

lakini wasiomcha Mungu hujaa mabaya.

22Midomo ya uwongo humtapisha Bwana,

lakini wafanyao yaliyo kweli humpendeza.

23Mtu aerevukaye huyaficha, anayoyajua,

lakini mioyo ya wapumbavu huutangaza ujinga.

24Mikono yao wajihimizao kufanya kazi hupata ufundi,

lakini mikono ilegeayo hujipatia utumwa.

25Majonzi yaliyomo ndani ya moyo wa mtu huulemeza,

lakini neno jema huufurahisha.

26Mwongofu humwongoza mwenzake,

lakini njia zao wasiomcha Mungu huwapoteza.

27Mwenye uvivu hamkimbizi nyama wake wa kuwinda,

lakini mali za mtu zilizo na kima ni kujihimiza kufanya kazi.

28Katika njia ya wongofu ndipo, uzima ulipo;

njia hiyo inapopitia, kifo hakipo hapo.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania