The chat will start when you send the first message.
1Moyo wa mfalme ni kama vijito vya maji mkononi mwa Bwana,
humpeleka pote panapompendeza.
2Njia zote za mtu hunyoka machoni pake,
lakini Bwana huijaribu mioyo.
3Kufanya wongofu na kupiga mashauri yaliyo sawa
humpendeza Bwana kuliko kutoa vipaji vya tambiko.
4Macho yajivunayo na moyo ujitutumuao
ndio taa zao wasiomcha Mungu, nazo hukosesha.
5Mawazo yake ajikazaye kufanya kazi humpatia mengi,
lakini mwenye haraka hujipatia ukosefu tu.
6Kujipatia malimbiko kwa ulimi uongopao
ni kama pumzi ipoteleayo angani tu,
wayatakao hujitafutia kufa.
7Uangamizi wao wasiomcha Mungu huwapokonya,
kwa kuwa hukataa kufanya yaliyo sawa.
8Njia ya mtu akoraye manza hupotoka sana,
lakini matendo yake anyokaye hutakata.
9Kukaa darini pembeni ni kwema
kuliko kukaa na mwanamke mgomvi katika nyumba moja.
10Roho yake asiyemcha Mungu hutamani mabaya,
mwenziwe hapati huruma machoni pake.
11Mfyozaji akitozwa fedha, mjinga huerevuka,
naye mwerevu wa kweli akifundishwa hupata ujuzi zaidi.
12Yuko mwongofu aiangaliaye nyumba yake asiyemcha Mungu,
naye huwapotoa wasiomcha Mungu, wapatwe na mabaya.
13Alizibaye sikio lake, lisisikie kilio cha mnyonge,
naye atakapolia hatajibiwa.
14Kipaji kipenyezwacho hutuliza ukali,
nayo matunzo yafichwayo penye kujua huzima nao moto mkali.
15Furaha ya mwongofu ni kufanya yaliyo sawa,
lakini wafanyao mapotovu hukuwazia kuwa mwangamizo.
16Mtu apoteaye kwa kuiacha njia ya ujuzi
hupata kupumzika katika mkutano wao waliokufa.
17Apendaye michezochezo huwa mtu akosaye vyote,
apendaye mvinyo na vinono hatapata mali.
18Asiyemcha Mungu hana budi kumkomboa mwongofu,
naye avunjaye agano hulipa mahali pao wanyokao.
19Kukaa katika nchi ya nyika ni kwema
kuliko kukaa na mwanamke mgomvi mwenye matata.
20Limbiko lipendezalo na mafuta yamo katika makao ya werevu wa kweli,
lakini mtu mjinga huyameza.
21Afanyaye bidii kuufuata wongofu na upole
hupata uzima na wongofu na utukufu.
22Mwongofu hupanda na kuuingia mji wa wenye nguvu,
nalo boma lao gumu, walilolitegemea, huliangusha.
23Akiangaliaye kinywa chake na ulimi wake
hujiangalia mwenyewe, asisongwe na maneno.
24Mtu ajitutumuaye kwa majivuno, aitwaye mfyozaji
hufanya mambo, anayofundishwa na majivuno yake yafurikayo.
25Tamaa za mvivu humwua,
kwa kuwa mikono yake hukataa kufanya kazi.
26Kila siku yako yanayotamaniwa kwa tamaa,
lakini mwongofu hutoa mali, hawanyimi wamwombao.
27Wasiomcha Mungu wakitoa vipaji vya tambiko humtapisha,
zaidi wakivitoa na kuyaficha mawazo yao mabaya.
28Shahidi ya uwongo huangamia,
lakini mtu asikiaye kwanza atasema siku zote.
29Mtu asiyemcha Mungu huushupaza uso wake,
lakini yeye anyokaye huishupaza njia yake.
30Hakuna werevu wa kweli, wala utambuzi,
wala shauri njema mbele ya Bwana.
31Farasi huwekwa kuwa tayari siku za mapigano,
lakini wokovu hutoka kwa Bwana.