Mifano 6

Mifano 6

Msijitoe kuwa dhamana!

1Mwanangu, kama umejitoa kuwa dhamana ya mwenzio,

ukampa mwingine mkono wako,

2kama umejifunga kwa maneno ya kinywa chako,

ukanaswa na maneno ya kinywa chako,

3basi, mwanangu, fanya hivi, upate kujiokoa,

kwa kuwa umejitia mkononi mwa mwenzio:

nenda kumwangukia mwenzio na kumlalamikia!

4Usiache, macho yako yalale usingizi,

wala kope zako zisinzie!

5Ponyoka mkononi mwake kama paa,

au kama ndege anavyoponyoka mkononi mwa mtega tanzi!

Msiwe wavivu!

6Nenda kwao siafu, wewe mvivu,

uzitazame njia zao, uerevuke kweli!

7Hao hawana mkuu wala msimamizi,

wala mtawalaji hawana.

8Hujitengenezea pamba za siku za vuli,

hulimbika vyakula penye siku za mavuno yao.

9Wewe mvivu, unataka kulala mpaka lini?

utaamka lini katika usingizi wako?

10Unataka kulala bado kidogo na kupumzika bado kidogo

na kukunja mikono kitandani bado kidogo.

11Kisha umaskini utakujia kama mpiga mbio

pamoja na ukosefu ulio kama mtu aliyevaa mata.

Msifanye mabaya!

12Mtu asiyefaa kitu, mtu mwenye maovu

ndiye atembeaye mwenye upotovu wa kinywa.

13Hukonyeza kwa macho yake, huparapara kwa miguu yake,

tena hupungia watu kwa vidole vyake.

14Huwaza mapotovu moyoni mwake akitunga mabaya pasipo kukoma,

huchokoza, agombanishe watu.

15Kwa hiyo mara mwangamizo wake utamjia,

asipoviwazia atavunjwa, asione atakayemponya.

16Yako mambo sita yamchukizayo Bwana,

tena yako mambo saba yauchafuaye moyo wake:

17macho yenye majivuno, ulimi wenye uwongo,

mikono imwagayo damu ya mtu asiyekosa,

18moyo utungao maneno maovu,

miguu ipigayo mbio kukimbilia penye mabaya,

19shahidi ya uwongo asemaye ya kuongopa

naye achokozaye, agombanishe ndugu.

Msizini!

20Mwanangu, lilinde agizo la baba yako,

wala usiyabeue maonyo ya mama yako!

21Yafunge siku zote moyoni mwako,

kayavae shingoni pako!

22Ukitembea, na yakuongoze! Ukilala na yakulinde,

ukiamka, na yaongee na wewe!

23Kwani hilo agizo ni taa, hayo maonyo nayo ni mwanga,

ni njia ya kwenda uzimani, ukionyeka kwa kukanywa nayo.

24Yakuangalie, usitazame mwanamke mbaya,

wala usiyasikilize maneno yatelezayo ya mwanamke mgeni!

25Usiutamani uzuri wake moyoni mwako!

wala asikunase na kukukonyeza kwa kope za macho yake!

26Kwani kwa ajili ya mwanamke mgoni mtu hutoa mali,

mpaka akose hata kipande cha mkate;

naye mwanamke wa mwingine huotea,

mpaka aipate nayo roho ya mtu isiyolipika.

27Je? Mtu anaweza kupaa moto, auweke kifuani pake

pasipo kuzichoma nguo zake?

28Au mtu anaweza kukanyaga makaa yenye moto,

nyayo zake siziungue?

29Ndivyo, mtu alivyo akiingia kwa mke wa mwenziwe,

kwao wote wamgusao hakuna atokaye pasipo kukora manza.

30Watu hawambezi mwizi aibiaye kujishibisha tu,

kama alikuwa na njaa.

31Akikamatwa hulipa mara saba,

ijapo atoe mali zote, alizo nazo nyumbani.

32Mtu akivunja unyumba na mke wa mwingine amepotelewa na akili,

maana hujiangamiza mwenyewe kwa kufanya hivyo.

33Hupata mapigo na matusi,

wala hakuna awezaye kuyafuta yaliyomtia soni.

34Kwani wivu ni kama moto wa mtu wa kiume,

haoni huruma anapojilipiza.

35Hatazami kabisa makombozi yo yote,

ingawa mtolee matunzo mengi, hayataki.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania