The chat will start when you send the first message.
1Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza Waamoni, wakauzingira Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu.[#1 Nya 20:1]
2Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari la jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho.[#Kum 22:8; Mwa 34:2; Ayu 31:1; Zab 119:37; Mt 5:28]
3Naye Daudi akatuma mtu akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bathsheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti?[#2 Sam 23:29]
4Basi Daudi akatuma wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake.[#Kut 20:17; Law 18:20; 20:10; Ebr 13:4; Yak 1:14; Law 15:19; 18:19]
5Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka habari na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja mzito.[#Law 20:10]
6Ndipo Daudi akapeleka habari kwa Yoabu, akisema, Mtume kwangu Uria, Mhiti. Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi.
7Uria alipomwendea Daudi, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, na habari za watu, na habari za vita.
8Daudi akamwambia Uria, Haya, shuka nyumbani kwako, ukanawe miguu yako. Basi Uria akatoka katika nyumba ya mfalme, na tunu ya vyakula ikamfuata, iliyotoka kwa mfalme.[#Zab 44:21; 55:21; Mwa 18:4; 19:2]
9Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake.[#Ayu 5:12-14]
10Watu walipomwambia Daudi ya kwamba, Uria hakushuka nyumbani kwake, Daudi akamwambia Uria, Je! Hukutoka safarini? Mbona hukushuka nyumbani kwako?
11Naye Uria akamwambia Daudi, Sanduku, na Israeli, na Yuda, wanakaa vibandani; na bwana wangu Yoabu, na watumishi wa bwana wangu, wamepiga kambi waziwazi uwandani; nami niende nyumbani kwangu, kula na kunywa, na kulala na mke wangu? Uishivyo, na kama roho yako iishivyo, mimi sitafanya jambo hili.[#2 Sam 7:2,6; 1 Sam 4:4; 2 Sam 20:6; Mt 10:25; 2 Tim 2:3]
12Basi Daudi akamwambia Uria, Ngoja hapa leo tena, na kesho nitakuacha kwenda zako. Basi Uria akakaa Yerusalemu siku ile, na siku ya pili yake.[#Ayu 20:12-14; Yer 2:22,23,37]
13Naye Daudi akamwalika, akala, akanywa mbele yake; naye akamlevya; hadi wakati wa jioni akatoka kwenda kulala kitandani mwake pamoja na watumishi wa bwana wake, lakini hakushuka nyumbani kwake.[#Mwa 9:21,22; 19:33,35; Kut 32:21; 1 Fal 20:16-21; Mit 20:1; 23:29-35; Hos 4:11; Gal 5:21]
14Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu barua, akaituma kwa mkono wa Uria.[#1 Fal 21:8; Zab 19:13; 62:9; Mhu 8:11; Yer 9:1-4; 17:9; Mik 7:3-5]
15Akaandika katika barua hiyo, akasema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe.[#2 Sam 12:9]
16Ikawa, Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa.
17Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria, Mhiti, naye akafa.
18Ndipo Yoabu akapeleka ujumbe na kumwarifu Daudi habari zote za vita;
19akamwagiza yule mjumbe, akisema, Ukiisha kumpa mfalme habari zote za vita,
20kisha, ikiwa hasira ya mfalme itawaka, akakuambia, Kwa nini mliukaribia mji namna ile ili kuupiga? Je! Hamkujua ya kuwa watapiga mishale toka ukutani?
21Ni nani aliyempiga Ahimeleki, mwana wa Yeru-beshethi? Je! Si mwanamke aliyemtupia jiwe la kusagia la juu kutoka ukutani? Hata akafa huko Thebesi? Kwa nini mliukaribia ukuta namna ile? Ndipo utakaposema, Mtumishi wako Uria, Mhiti, amekufa naye.[#Amu 9:53; 2 Sam 20:21; Ayu 31:3]
22Basi yule mjumbe akaenda, akafika na kumwonesha Daudi yote aliyomtuma Yoabu.
23Yule mjumbe akamwambia Daudi, Watu hao walitushinda, wakatutokea nje hata uwandani, tukashindana nao hadi mahali pa kuingilia langoni.
24Wapiga mishale wakatupiga sisi, watumishi wako, toka juu ya ukuta; na baadhi ya watumishi wa mfalme wamekufa, na Uria, Mhiti, mtumishi wako, amekufa naye.
25Basi Daudi akamwambia yule mjumbe, Basi, mwambie Yoabu maneno haya, Jambo hili lisiwe baya machoni pako, maana upanga hula huyu kama unavyomla huyu; zidi kutia nguvu vita vyako juu ya mji ukauangushe; nawe mtie moyo.
26Na yule mke wa Uria alipopata habari ya kuwa Uria mumewe amekufa, akamwombolezea mumewe.
27Hata maombolezo hayo yalipokwisha, Daudi akatuma mtu, akamtwaa, akamtia nyumbani mwake; naye akawa mkewe, akamzalia mtoto wa kiume.[#2 Sam 12:9; Ayu 10:14; 11:11; Zab 5:4; 45:7; Mit 15:9; Hab 1:13]
Lakini jambo lile alilolitenda Daudi likamchukiza BWANA.