The chat will start when you send the first message.
1Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha nenda ukaseme na wana wa Israeli.[#Eze 2:8,9; Ufu 10:9-10]
2Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo.
3Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali.
4Akaniambia, Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli ukawaambie maneno yangu.
5Maana wewe hukutumwa kwa watu wa lugha isiyoeleweka, ama wa lugha ngumu, bali kwa nyumba ya Israeli;
6si kwa watu wa kabila nyingi wenye usemi usioeleweka, na lugha ngumu, ambao huwezi kufahamu maneno yao. Bila shaka, kama ningekutuma kwa watu hao, wangekusikiliza.
7Bali nyumba ya Israeli hawatakusikiliza wewe; kwa kuwa hawanisikilizi mimi; maana nyumba yote ya Israeli wana vipaji vigumu, na mioyo yenye ukaidi.[#Yn 15:20]
8Tazama, nimeufanya uso wako kuwa mgumu juu ya nyuso zao, na kipaji cha uso chako kuwa kigumu juu ya vipaji vya nyuso zao.
9Kama almasi ilivyo ngumu kuliko gumegume, ndivyo nilivyokifanya kipaji chako; usiwaogope, wala usifadhaike kwa sababu ya nyuso zao, wajapokuwa ni nyumba ya kuasi.[#Yer 1:18]
10Tena akaniambia, Mwanadamu, maneno yangu yote nitakayokuambia, yapokee moyoni mwako, na kuyasikia kwa masikio yako.
11Haya! Nenda uwafikie watu hao waliohamishwa, kwa wana wa watu wako, ukaseme nao, na kuwaambia, Bwana MUNGU asema hivi; iwe watasikia au hawataki kusikia.
12Ndipo roho ikaniinua, nami nikasikia nyuma yangu sauti kama mshindo wa radi kuu, ikisema, Na uhimidiwe utukufu wa BWANA tokea mahali pake.[#Eze 8:3; Mdo 8:39]
13Nikasikia mshindo wa mabawa ya vile viumbe hai, walipogusana, na mshindo wa yale magurudumu kando yao, mshindo wa radi kuu.
14Basi roho ikaniinua, ikanichukua mahali pengine; nami nikaenda kwa uchungu, na hasira kali rohoni mwangu, na mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu kwa nguvu.[#2 Fal 3:15]
15Ndipo nikawafikia watu waliohamishwa, huko Tel-abibu, waliokuwa wakikaa karibu na mto Kebari, nikafika huko walikokuwa wakikaa; nikaketi huko miongoni mwao muda wa siku saba, katika hali ya ushangao mwingi.[#Ayu 2:13; Zab 137:1]
16Hata ikawa, mwisho wa siku saba, neno la BWANA likanijia, kusema,
17Mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi wa nyumba ya Israeli; basi, sikia neno hili litokalo katika kinywa changu, ukawape maonyo haya yatokayo kwangu.[#Wim 3:3; 5:7; Isa 21:6,8,11,12; 52:8; 56:10; Yer 6:17]
18Nikimwambia mtu mwovu, Hakika utakufa; na wewe usimpe maonyo, wala kusema na huyo mtu mwovu ili kumwonya, ili kusudi aache njia yake mbaya na kuiokoa roho yake; mtu yule mwovu atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.[#Rum 1:16; 1 Tim 4:16; Eze 33:6]
19Lakini ukimwonya mtu mwovu, wala yeye hauachi uovu wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako.[#Mdo 20:26]
20Tena mtu mwenye haki aiachapo haki yake, na kutenda uovu, nami nikaweka kikwazo mbele yake, atakufa; kwa sababu hukumwonya, atakufa katika uovu, wala matendo yake ya haki aliyoyatenda hayatakumbukwa; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.[#Eze 18:24; 2 Pet 2:20]
21Bali ukimwonya mwenye haki, kwamba yule mwenye haki asitende dhambi, tena ikawa yeye hatendi dhambi, hakika ataishi, kwa sababu alikubali kuonywa; nawe umejiokoa roho yako.[#Rum 2:7; Mdo 18:6]
22Na mkono wa BWANA ulikuwako juu yangu huko; akaniambia, Ondoka, nenda bondeni; nami nitasema nawe huko.[#Eze 8:4]
23Basi, nikaondoka, nikaenda bondeni, na tazama, utukufu wa BWANA ulisimama huko, kama utukufu ule niliouona karibu na mto Kebari; nami nikaanguka kifudifudi.[#Eze 1:1,28]
24Ndipo roho ile ikaniingia, ikanisimamisha kwa miguu yangu; akasema nami, akaniambia, Nenda ukajifungie nyumbani mwako.[#Eze 2:2]
25Lakini wewe, mwanadamu, tazama, watakutia pingu, nao watakufunga kwazo, wala hutakwenda nje kati yao;[#Eze 4:8]
26nami nitaufanya ulimi wako ugandamane na kaakaa lako, hata utakuwa bubu, wala hutakuwa mwonyaji kwao; kwa kuwa wao ni nyumba yenye kuasi.[#Eze 24:27; 2:5,6; Lk 1:20-22]
27Lakini hapo nitakaposema nawe, nitafumbua kinywa chako, nawe utawaambia, Bwana MUNGU asema hivi. Yeye asikiaye na asikie; naye akataaye na akatae; maana wao ni nyumba yenye kuasi.[#Eze 24:27; 33:22; 12:2,3]